dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, October 15, 2015

Mwalimu Nyerere: Ikulu ni mahala patakatifu

Mwalimu Julius Nyerere akizungumza katika moja ya mikutano yake.
Huu ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu, tunapoadhimisha kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Nyerere, ni jambo la busara kwa Watanzania kujikumbusha mawazo na mitazamo yake kuhusu chaguzi. Makala haya yanarejea moja ya hotuba alizotoa Mwalimu Nyerere kuhusu uchaguzi na sifa za wagombea.
‘‘...Tunataka rais Mtanzania. rais tunayemtaka ni Mtanzania. Hatuwezi kupata rais Mtanzania asitoke ama Zanzibar ama Tanganyika. Lakini hatumchagui kwa sababu ya Uzanzibari wake na hatumchagui kwa sababu ya Utanganyika wake.
Akiweka mbele uzanzibar wake, akiweka mbele utanganyika wake, tunajua huyu hatufai. Hiyo ndiyo sifa mama. Kwa sababu tunayemtaka ni rais wa Tanzania.
Mimi niko hapa kuzungumzia rais wa Tanzania. Tunaye wa kwanza, tunaye wa pili na sasa watatu.
Tunataka rais wa Tanzania. Hiyo ndiyo sifa yake ya kwanza, ndiyo sifa mama, hana hiyo, hatumtaki hata kama angekuwa na sifa nyingine za namna gani. Atavunja nchi yetu. Hatufai.
Hiyo ya kwanza. Ya pili, inafuatana kidogo na hiyo. Rais wa nchi yetu, anachaguliwa kutokana na katiba ya Tanzania. Na akisha kuchaguliwa, anaapishwa. Kama ni Mkristo, kwa Biblia, kama ni Muislamu, kwa Quran. Hatujachagua mtu asiyeamini Mungu.
Lakini tukimchagua, tutatafuta utaratibu wa kumwapisha. Ataapa. Hata asiyekuwa muumini, tutamwapisha, kwamba atailinda na kuitetea Katiba ya Tanzania.
Hapa katikati kumetokea na kupuuza puuza Katiba. Ufa wetu wa pili. Hatuwezi kuendelea kupuuza Katiba. Katiba ndiyo sheria ya msingi.
Sheria nyingine zote zinatokana na Katiba, haiwezi kupuuzwa. Hatuwezi kuendelea na utaratibu wa kupuuza Katiba ya nchi yetu. Au rais anayeionea haya kuitetea Katiba, naye amechaguliwa kwa mujibu wa Katiba hiyo, ameapa kuilinda Katiba hiyo halafu anaona haya kuitetea Katiba hiyo.
Mtu ambaye hawezi kuitetea Katiba ya nchi yetu, hawezi kuilinda, hawezi kuisimamia, baada ya kiapo, hatufai. Hafai. Aende akaendeshe shamba lake hukooo.
Hawezi kuwa katika rais wa nchi yetu, tunamchagua kwa mujibu wa Katiba, tunamwapisha kwa Katiba, ailinde, aitetee kwa moyo thabiti kabisa bila woga. Hawezi, hatumtaki.
Hatutamchagua kuwa kiongozi wetu. Anaweza kuwa rafiki yetu sana, anaweza kuwa kabla hajafika kwenye vikao vyetu hatuanzi kunywa chai au brandy au whisky, hilo ni shauri jingine, lakini kwa urais wa nchi, hatufai. Tumeuona ufa huo, wa kutojali Katiba ya nchi.
Ufa wa tatu unafuatana kabisakabisa. Nchi zote duniani, zinaongozwa na watu. Mimi niliwahi kupata heshima ya kuiongoza nchi hii, sasa leo Rais Mwinyi anaiongoza, sasa hivi tunazungumza kuona nani baadaye, tutazungumza nani anafaa kutusaidia kuongoza, nchi zinaongozwa na watu, kumbe zitaongozwa na nani?
Hatuna malaika, hatuna nini, ndivyo alivyotaka Mwenyezi Mungu, nchi hizi tuziongoze wenyewe, sisi hawa hawa. Lakini haziongozwi kutokana na akili za mtu.
Zinaongozwa kutokana na sheria...sheria, ukweli nchi zinaongozwa na watu, lakini hao watu wanaongozwa na sheria.
Watu ni muhimu kabisa, ni lazima kuwa na viongozi imara, ndiyo maana niko hapa kuzungumzia viongozi imara, lakini wanaongozwa na sheria.
Haiwezekani mtu anapata ushauri kwa mkewe, kesho unakuta jambo fulani limetokea...Huko kucheka, kunaonyesha umuhimu wa sheria mmeelewa. Hamuwezi kutawaliwa, hata hamjui kesho mkewe atamwambia nini.
 Nimesema tunataka rais anayejua kwamba Muungano wetu umetikiswa, na hiyo inamkera...anakerwa na kwamba tukimpata, kazi yake moja atasimamia hilo.
Tunataka rais wetu anayejua tumechezeachezea Katiba kidogo na inamkera. Akipata nafasi, akipewa nafasi na wenzake, atalisimamia hili la kuchezacheza na Katiba.
Tumeona sheria za nchi, watu wanajaribu kuendesha nchi bila kujali sheria za nchi.
Kuendesha mambo bila kujali sheria. Tunataka mtu wa kuwa kiongozi wetu ambaye hilo linamkera. Huwezi kuendesha nchi bila utaratibu wa sheria, watu hawawezi kujua kesho kutatokea nini.
Na watu wanataka wajue, wanakaa katika majumba yao wanajua, wanatawaliwa na sheria kwa hiyo hawana wasiwasi.
Zamani kulikuwa na kitu kinaitwa miiko ya uongozi. Nyingine zilikuwa wakati wa Tanu zinaitwa kanuni za Tanu.
Na kanuni moja ya Tanu ambayo baadaye tukairithi katika CCM au tukarithisha CCM, inasema rushwa ni adui wa haki, sitatoa wala sitapokea rushwa.
Msije mkadhani kwamba wakati wa awamu ya kwanza palikuwa hapana rushwa. Ilikuwapo.
Lakini tulikuwa wakali...tulikuwa wakali sana, siku za mwanzo kabisa, tulitaka watu wajue kwamba tutakuwa wakali sana na wala rushwa ndani ya Serikali, au na watoa rushwa.
Mwanzo kabisa wa kujitawala, tulitaka kila mtu ajue. Tukapitisha sheria, kwamba mtu akila rushwa...kiongozi wetu unakula rushwa, aliyetoa, aliyepokea, Wazanaki wanasema wote manzilanyaze, wote watapata msukosuko, hatukuwa tunatania.
Tukatengeneza sheria ili tuwafundishe watu hawa kwamba hili jambo hatulipendi, akisha kuthibitika mahakamani, kwamba kala rushwa...katoa rushwa, hatukumwachia hakimu uamuzi wa adhabu, tukasema atakwenda ndani, muda usiopungua miaka miwili, atapata viboko 24, 12 siku anaingia na 12 siku anayotoka akamwonyeshe mkewe (kicheko)....
Tanzania inanuka rushwa. Tunataka kiongozi anayejua hilo ambaye atasema rushwa kwangu ni mwiko, mwaminifu kabisakabisa, na wanamjua na watoa rushwa watamjua hivyo, lakini hatutaki aishie hapo tu, wewe mwenyewe uwe mwaminifu, mambo haya yana matatizo.
Wewe mwenyewe unaweza kuwa mwaminifu kabisa, lakini ukawa na presha za ndugu zako, presha za jamaa zako presha za marafiki zako.
Si kwamba inatosha wewe uwe mwaminifu tu, lakini uwe na uwezo wa kuwaambia jamaa zako, na rafiki zako kwa kauli ambayo wataiheshimu na hawatarudia tena. Ikulu ni mahali patakatifu.
Unawaambia jamaa zako na marafiki zako  Ikulu ni mahala patakatifu. Mimi sikuchaguliwa na wananchi wa Tanzania kuja kupageuza pango la walanguzi.
 Ukishakuwaambia hivyo, ndugu zako na marafiki zako, na ikajulikana hivyo, mtu mwingine wala hakusogelei. Nafsi yake haimtumi kukusogelea.
Sasa nasikia mtu anakuja na pesa. Uchaguzi wa mwaka huu utakuwa uchaguzi wa pesa. Zamani katika CCM na katika Tanu, tunapochagua candidate wetu, kama ana mali tunamuuliza, hii mali umepata wapi, mali ilikuwa disqualification,mwaka huu mali itakuwa number one qualification, wamezipata wapi, huo tunadhani ni ufa watatu, ulitikisa na umetikisa..’’.
Imeandaliwa na Ibrahim Bakari

No comments :

Post a Comment