Japo kila mgombea urais anajitahidi kujinasibisha na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kwa na namna moja ama nyingine ili kuvutia kura za kutosha, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini wanasema bila shaka Mwalimu angekuwa na upande.
Wagombea watatu wa urais, Dk. John Magufuli wa CCM, Edward Lowassa wa Chadema na Anna Mghwira wa ACT – Wazalendo, wote wanatumia ushawishi wa Mwalimu Nyerere katika kampeni zao.
Kwa upande wa ACT – Wazalendo, kimetangaza rasmi kwamba kinasimamia sera za Unyerere (Nyerereism) na kwa kutekeleza hilo kimetangaza Azimio la Tabora, lenye kulenga kuhuisha Azimio la Arusha ambalo ndilo liliweka msingi wa itikadi ya aliyoisimamia Mwalimu Nyerere.
Chadema na hasa mgombea wake, Lowassa, amekuwa akitumia kauli ya Mwalimu Nyerere aliyoitoa mwaka 1995, wakati akizungumza na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo kwamba, wananchi wasipopata mabadiliko ndani ya CCM, watayatafuta nje ya CCM, kuhalalisha uamuzi wake wa kutoka CCM na kujiunga Chadema, alikoteuliwa kugombea urais baada ya kukatwa CCM.Wakati Lowassa akitamba na kauli hiyo ya Mwalimu, CCM mbali na kujiegemeza kwenye kauli ya Mwalimu aliyoitoa kwenye Mkutano Mkuu wa CCM 1995 kwamba, rais bora atatoka CCM, kimekuwa pia kikitumia hoja ya Lowassa kukataliwa na Mwalimu Nyerere kwenye uchaguzi huo wa 1995.
Swali la msingi linabaki halijajibiwa kwamba, ni nani kwa dhati, kati ya wagombea waliopo wa urais, anaweza kustahili kuwa chaguo la Mwalimu kwa kuangalia misingi aliyokuwa akiisimamia.
Mwalimu Nyerere ambaye Taifa
leo linaadhimisha miaka 16 tangu afariki dunia, alikuwa na ushawishi mkubwa katika kuamua mshindi wa Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, kwa kuweka misingi na sifa ambazo Rais wa Tanzania anapaswa kuwa nazo, na kuonya kuwa wapo baadhi ya wagombea wa kuogopwa kama ukoma.
Katika Kitabu cha Uongozi wetu na Hatma ya Tanzania, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, alihitimisha na utenzi wa kuonya na kushauri, “Ole wake Tanzania, Tusipoisaidia, niwezalo nimefanya: kushauri na kuonya.”
Akihadharisha kuhusu hatma ya Tanzania, na umuhimu wa kulinda tunu za taifa, jambo ambalo linaweza kuwa kipimo kizuri kwa wagombea urais katika uchaguzi huu,kama wanaweza kutimiza ndoto za Taifa.
Alitoa ushauri huo kwa jambo mahsusi, lakini ukizingatia dhamira yake ya tangu Uhuru, kujenga Taifa lenye umoja, ushauri huo una umuhimu wa kipekee kwa Tanzania ya leo.
Katika hotuba yake kuliaga Bunge, Julai 29, 1985, kabla ya kustaafu wadhifu wa rais wa Tanzania, Mwalimu Nyerere alisema; “Kazi iliyokuwa muhimu kuliko zote kwangu mimi, na kwa wananchi wote, ambayo niliazimia katika hotuba yangu ya kwanza kabisa hapa bungeni mara baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Tanganyika ya mwezi Desemba 1962, ilikuwa ni kazi ya kujenga Taifa lenye umoja, kwa msingi wa heshima na usawa wa binadamu.”
Wakati huo Mwalimu Nyerere alijiridhisha kwamba kazi hiyo imefanyika kwa uhakika na ni jambo ambalo kama Taifa tunaweza kujivunia, “Nadhani leo naweza kusema bila kusita, kwamba; kwa shabaha hii kuu na ya msingi kabisa, tunayo haki ya kujivuna. Kwani sasa tunalo Taifa na Taifa lenye umoja,” alisema katika hotuba hiyo ya kuliaga Bunge.
Miaka 10 baadaye, wakati Taifa linaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi mwaka 1995, Mwalimu alishaona nyufa ambazo zilikuwa zinatishia kusambaratisha umoja wa Taifa.
Alisisitiza kiongozi wa Tanzania lazima aonyeshe kwamba anakerwa na rushwa kiasi kwamba watu wakimuangalia machoni wawe na imani kweli anaweza kupambana na rushwa, akitaja nyufa za udini na ukabila kama viashiria hatari vya umoja, akisisitiza kiongozi atakayechaguliwa lazima asiwe tu mdini wala mkabila lakini pia ajue kuwa vitu hivyo “ni upumbavu na hatari.”
“Mtu anayetaka kwenda Ikulu kupata faida yoyote Ikulu pale; hatufai hata kidogo! Wananchi, mimi nimekaa Ikulu pale kwa muda mrefu zaidi kuliko mtu mwingine yeyote. Mimi naijua Ikulu. Kwa mtu mwaminifu kabisa kabisa, Ikulu ni mzigo.
Hupakimbilii. Si mahali pa kukimbilia hata kidogo. Huwezi kupakimbilia Ikulu. Unapakimbilia kwenda kutafuta nini?” alihoji Mwalimu katika moja ya hotuba zake.
Upo uhusiano wa karibu kati ya Taifa kuendelea kuwa na umoja na mshikamano na uamuzi ambao Watanzania watatakiwa kuufanya wiki ijayo, Oktoba 25, watakapokwenda kuchagua Rais, mbunge na diwani, ndiyo maana katika hotuba zake hizo Mwalimu Nyerere alisisitiza sana umuhimu wa kuwa na kiongozi mwenye sifa zilizonukuliwa hapo juu.
Miaka 20 baada ya Mwalimu kutoa vigezo hivyo, bado vina umuhimu hata leo, kwa kuwa nyufa na changamoto zilizolikabili taifa wakati ule bado zipo na pengine zimeongezeka zaidi.
Je, Mwalimu angeweza kumuunga mkono mgombea gani, kama angekuwa hai, Dk. Bashiry Ally, wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anasema Mwalimu alikuwa mwanasiasa, mwanazuoni, mwanafalsafa na alikuwa binadamu. Kama binadamu angeelezea hisia zake, na utashi wake lakini kwa kuwa amefariki hilo haliwezekani, lakini kama mwanafalsafa na mwanazuoni amekuwa na msimamo katika mambo mengi ambayo ni muhimu Watanzania kuyatafakari.
“Mfano aliposema, mabadiliko nje ya CCM, hakumaanisha nje ya CCM popote pale, alimaanisha chama mbadala wa CCM, ninavyojua mpaka anakufa hakuona chama mbadala wa CCM, ndiyo maana aliamini Rais bora atatoka CCM, alisisitiza kuwa bila CCM madhubuti nchi hii itayumba.
“Na mimi ninaona sasa, Chama cha Mapinduzi kimeyumba, nchi inayumba. Mwalimu alitaka chama mbadala wa CCM chenye sura ya utaifa, sasa ukituambia mabadiliko nje ya CCM wapi, msituni, gizani mtaroni au wapi? Mabadiliko gani, yanaongozwa na misingi gani?”
Alisema kwa kungalia mfano wa mambo yaliyomkera na kumnung’unisha Mwalimu ni mengi ambayo haoni kama wagombea hawa wanaweza kuyasimamia au hata kuyaishi kwa robo tu.
“Mwalimu amekufa akinung’unikia ubinafsihaji wa hovyo wa vitega uchumi wa kimkakati, na kubinafsisha rasilimali ardhi, ambayo Mwalimu aliamini ni uhai, ni kielelezo cha utaifa na inatakiwa na kila mtu bila kujali uwezo wa fedha, ardhi ni mama wa maendeleo na kila kitu. Sasa hivi hata sisikii wakizungumzia falsafa na misingi aliyoisimamia Mwalimu hata kwa robo, wananukuu vipande vipande tu,” alisema Bashiru na kuongeza.
“Kauli za kifalsafa zinahitaji tafakari makini na akili tulivu bila mihemko ya kisiasa, sidhani tafsiri ya matamko ya Mwalimu inaweza kufanywa na jini mahaba pesa, wanasiasa wetu hawa siamini wanaweza kuzitendea haki.”
Alisema si busara kutumia nukuu za Mwalimu wakati maalumu ama uchaguzi au wakati wa matatizo, badala yake matamko na maandishi yake yanatakiwa kufanyiwa kazi na wanzuoni, kwenye sekta ya elimu na waandishi wa habari.
Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Profesa Penina Mlama, akizungumza na Raia Mwema kuhusu kumbukumbu ya Miaka 16 ya kifo cha Mwalimu na namna ya kuendelea kumuenzi katika mwaka huu wa uchaguzi, alisema kitu muhimu ambacho Taifa linahitaji ni itikadi inayoeleweka.
“Mwalimu aliongoza kwa kufuata itikadi, Tanzania lazima iwe na itikadi, Mwalimu alimuweka binadamu katikati ya maendeleo, hawa (wagombea na vyama) itakdi yao ni nini? Hata kama si Ujamaa waseme wanasimamia itikadi gani, ubepari au ni nini? Na kama ni ubepari ni wa namna gani?” alihoji Profesa Mlama.
Alisema kuwa ahadi zinazotolewa na wagombea hazitakuwa na maana kama hazijajengwa juu ya misingi ya itikadi, kwa sababu hazitakuwa na manufaa kwa maendeleo ya binadamu.
“Katika kampeni zao sijaona kama kuna dalili za kumuenzi Mwalimu, kama wana nia ya dhati warudi kwenye misingi ya Mwalimu,” alisema na kuwataka wagombea kujikita katika kumpigania Mtanzania wa kawaida.
“Waendeleze mambo ya Mwalimu, yeye alilenga kumhudumia mwamanchi wa chini, hawa wajielekeze huko,” alisema Profesa Mlama.
Akizungumzia namna kumuenzi Mwalimu katika uchaguzi huu, Dk. Benson Bana wa Chuo Kikuu cha Dar es Slaam, alisema Mwalimu aliweka misingi na sifa nzuri za kumpata kiongozi anayefaa kinachotakiwa ni kwa Watanzania kuzitafakari sifa hizo na kuzitumia kuwapima wagombea watakaowachagua.
Alisema kati ya wagombea waliojitokeza kuomba urais, wapo ambao sifa za Mwalimu zinawaangukia, japo si kwa asilimia mia moja.
“Sitaki kutaja majina, lakini ukiangalia kwa sifa utaona nani anaweza kufuzu kwenye sifa za Mwalimu, kwa mfano, suala la kutopageuza Ikulu kuwa mahali pa biashara, ukiangalia kati ya wagombea utaona nani amezungukwa na nani na nani anaweza kupageuza kuwa pango la biashara,” alisema Dk. Bana.
Alisema wapo miongoni mwa wagombea ambao wanakerwa na matatizo ya wananchi, na wana nia ya dhati ya kutaka kuyatatua na hawaendi huko kwa ajili ya kutaka kuwa raia tu.
“Mwalimu alitueleza uzoefu wake kuwa Ikulu ni kero tupu, nani kati ya wagombea hawa yuko tayari kubeba kero za Watanzania. Lakini pia wagombea wenyewe wamepatikanaje, kwa kuhonga au kwa haki. Tukiyatafakari haya naamini yatatusaidia kupata kiongozi mzuri,” alisema Dk. Bana.
Akimzungumzia Mwalimu Nyerere na uchaguzi, Profesa Honest Ngowi, wa Chuo Kikuu cha Mzumbe alisema Mwalimu alikuwa ni mtu aliyethamini umoja na amani na ndivyo Watanzania wanavyotakiwa kumuenzi.
“Tunajua Mwalimu alikuwa mtu wa amani, namna pekee ya kumuenzi katika uchaguzi huu ni kuhakikisha kuwa pamoja na ushindani mkali wa kisiasa, tufanye yote tunayofanya lakini tudumishe amani yetu, tusiruhusu ipotee, ” alisema.
Kuhusu sifa za rais anayeistahili Tanzania, alisema wananchi wanapaswa kuangalia kongozi anayeelewa changamoto zinazowakabili wananchi na anaelewa chanzo cha matatizo hayo ni nini, anawaelewa Watanzania, huyo anaweza kusadia kupambana na umasikini.
No comments :
Post a Comment