Dar es Salaam. Zimesalia saa 144 za kampeni ambazo wagombea wa vyama vyote vya siasa watazitumia kutupa karata zao za mwisho wakilenga kupata ushawishi wa mwishomwisho na hatimaye kunyakua ushindi.
Saa hizo za majeruhi zimesababisha wagombea urais wa CCM, Dk John Magufuli, Edward Lowassa wa Chadema na Anna Mghwira wa ACT – Wazalendo kujikita katika mikoa “ya kimkakati” na ile yenye wapigakura wengi.
Dk Magufuli ndiye aliyefungua pazia la kampeni Agosti 23 kwenye viwanja wa Jangwani, Dar es Salaam na kufuatiwa na Lowassa hapohapo Jangwani kabla ya Mghwira kuzindua huko Mbagala.
Wagombea hao ambao wameshazunguka mikoa yote nchini, watazitumia siku sita zilizobaki kabla ya siku ya kupigakura kujiwekea mazingira mazuri ya ushindi.
Akizungumzia mikakati ya mwisho ya kampeni, Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu alisema mikoa yote nchini ni ya kimkakati kwa chama hicho na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), huku akieleza jinsi Lowassa atakavyohitimisha siku zilizobaki.
“Kwa sasa, mgombea anaendelea na mikutano ya kampeni mkoani Mbeya. Akimaliza huko atarejea Dar es Salaam kwa ajili ya kufunga kampeni ila atapita katika mikoa ya Iringa na Morogoro.
“Tupo katika hatua za mwisho, hivyo tunaweza kuangalia pia ni wapi mgombea wetu anaweza kwenda ukiacha maeneo hayo,” alisema Mwalimu.
Mjumbe wa kamati ya kampeni ya CCM, January Makamba alisema mgombea urais wa chama hicho atazitumia siku sita zilizobaki kupita majimbo ambayo aliyaruka katika baadhi ya mikoa.
“Lengo letu ni kwenda kwenye majimbo yote, hivyo siku hizi zilizobaki atapita huko. Kuhusu wapi tutafunga kampeni zetu tutatangaza siku yoyote kuanzia leo,” alisema Makamba.
Lowassa jana aliendelea na kampeni mkoani Mbeya huku Dk Magufuli akiwa katika Wilaya ya Magu mkoani Mwanza.
Mikoa ya kimkakati na yenye wapigakura zaidi ya milioni moja kila mmoja ambayo huenda wagombea hao wakaitumia kunadi sera zao za mwishomwisho ni Morogoro, Tabora, Dodoma, Kagera, Tanga, Arusha, Mara, Geita, Kilimanjaro, Kigoma, Shinyanga, Ruvuma, Mtwara na Simiyu.
Mambo yasiyosikika
Akizungumzia ahadi za wagombea hao, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Nicolaus Mgaya alisema wagombea wengi wa urais wanazungumzia kuongeza mishahara wafanyakazi, lakini wanasahau kuzungumzia jinsi watakavyoongeza marupurupu ya wafanyakazi hao.
“Hapa nazungumzia kodi ya nyumba, fedha za usafiri na malipo ya likizo,” alisema Mgaya alipoulizwa kuhusu ahadi za wagombea.
Ardhi na Katiba
Pamoja na wagombea hao kuahidi kutatua migogoro ya ardhi, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (Sua), Profesa Damian Gabagambi anaona jambo hilo halijatolewa maelezo ya kutosha.
“Ardhi ni jambo ambalo halijapewa kipaumbele kwa maana ya kupimwa na matumizi yake kuidhinishwa na kulindwa kisheria. Mwingiliano wa matumizi ya ardhi ni moja ya matatizo makubwa nchini,” alisema Profesa Gabagambi.
Alisema wagombea hao hawajagusia suala la Watanzania kupata Katiba Mpya, ambayo mchakato wake ulikwama kabla ya hatua ya Kura ya Maoni.
“Suala la kusaidia wakulima kupata masoko ya uhakika halijafafanuliwa kwa kina wala jinsi ya kuanzisha na kuendeleza viwanda vidogovidogo kwa sababu ndiyo vinaajiri wananchi wengi kuliko vikubwa, ambavyo kila mgombea anasema atavianzisha akiingia madarakani,” alisema.
Itikadi
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Penina Mlama alisema hakuna aliyesema akishinda ataongoza nchi kwa itikadi ipi.
“Tunajua kuwa Wamarekani wanatumia mfumo wa ubepari na Mwalimu (Julius) Nyerere alitumia ujamaa, sasa hawa wa sasa (wagombea) wanaamini mfumo upi?” alihoji Profesa Mlama.
Ahadi za Lowassa
Lowassa amekuwa akitumia ahadi ya elimu bure kuanzia msingi hadi chuo kikuu kama silaha yake kuu ya kupata kura kwa wananchi.
“Kipaumbele cha kwanza ni elimu, cha pili ni elimu na cha tatu ni elimu,” alisema Lowassa tangu kwenye uzinduzi wa kampeni zake na amekuwa akirudiarudia kuhakikisha kinaeleweka.
Pia, katika mikutano yake mingi waziri huyo mkuu wa zamani amekuwa akizungumzia jinsi ya kutatua tatizo la maji, ambalo linaonekana kuwa kubwa sehemu nyingi licha ya baadhi kuwa na vijito, mito na maziwa, akitoa mfano wa jinsi alivyoshughulikia mradi wa maji ya Ziwa Victoria, ambao unasaidia wakazi wa mikoa ya Mwanza, Tabora na Mara.
“Nitahakikisha maziwa na mito mikubwa kama Kagera inatumika kuondoa tatizo la maji,” alisema Lowassa alipozungumza na wananchi wa Nkenge, Kagera.
“Kama niliweza kutoa maji Ziwa Victoria nitashindwa vipi kutoa maji kutoka Ziwa Tanganyika ili wananchi mpate maji ya uhakika?” alisema Lowassa katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Mwanga Community Centre, Kigoma.
Lowassa, ambaye amekuwa akiwaita waendesha bodaboda, wamachinga na mamalishe kuwa ni marafiki zake, amekuwa akiahidi kuanzisha benki maalumu ya kuhudumia wajasiriamali wadogo.
“Tumetengeza ilani kiboko ambayo ndani ya miaka mitano Tanzania yetu itabadilika, lazima tupunguze tabaka kati ya tajiri na maskini kwa uchumi wa pamba, chai, dhahabu na gesi kwa nini tushindwe? Mkitupa ridhaa na Mungu akikubali, tutakwenda kasi na tutakuwa na maendeleo,” alisema Lowassa katika mkutano uliofanyika mjini Makambako.
Ahadi za Dk Magufuli
Kete kubwa tano za mgombea wa CCM, Dk Magufuli ambazo amekuwa akizinadi takriban kila mahali anapokwenda tangu alipozindua kampeni zake ni pamoja na kufuta utaratibu wa kuwakamata na kuwatoza ushuru usio na tija waendesha bodaboda na mama lishe na kuwabana wafanyabiashara wakubwa kulipa kodi.
Kutoka Mpanda Vijijini alikoanzia kampeni za mikoani hadi maeneo anayoyafikia sasa, Dk Magufuli amekuwa akipata zaidi shangwe pale anapowaahidi awananchi kutoa mikopo ya Sh50 milioni kwa kina mama na vijana kwa kila kijiji nchi nzima ili kukuza ujasiriamali na kusomesha watoto bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne.
Amekuwa akianisha mikakati yake ya kudhibiti ufisadi nchini akiahidi kuanzisha mahakama maalumu ya kuwafunga mafisadi, ahadi ambao imeonekana kumbeba kiasi cha kutoisahau kila anapofanya mikutano yake.
Katika kipindi hicho cha takriban siku 58 za kampeni, Dk Magufuli ambaye ni waziri wa ujenzi, amekuwa akiahidi kuinganisha nchi kwa kujenga barabara za lami katika kila mkoa na hata katika miji mikubwa isiyo na barabara hizo kwenye mitaa na wiki iliyopita wakati kampeni zilielekea ukingoni alisaini mkataba wa ujenzi wa barabara za juu jijini Dar es Salaam.
Ahadi hizo kubwa zimekuwa zikisindikizwa na mikakati ya kujenga Reli ya Kati, ya Kusini kuanzia Bandari ya Mtwara – Songea – Mbamba Bay kupitia Mchuchuma na Liganga na ile ya Kaskazini kwa kiwango cha kimataifa.
Dk Magufuli ameahidi kuboresha huduma za afya na kusambaza maji na umeme vijijini ili usaidie kufanikisha mkakati wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.
Mghwira wa ACT
Mpaka sasa mgombea urais wa ACT-Wazalendo, Anna Mghwira amefanya kampeni katika mikoa mbalimbali Bara na Zanzibar na ahadi zake kubwa zikiwa ni kumaliza tatizo la maji, ujenzi wa barabara, viwanda, migogoro ya ardhi na elimu.
Upatikanaji wa majisafi na salama umeonekana kuwa tatizo kuu katika maeneo karibu mengi aliyozunguka kufanya kampeni zake. Akiwa kwenye mikoa ya Kanda ya Kusini na Kaskazini na Dodoma, Tabora na Pwani aliahidi kuwa serikali yake itapambana kuondokana na tatizo hilo, kwa haoni sababu ya kuendelea hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania ni nchi yenye vyanzo vingi vya maji.
Akiwa Ruvuma kwenye majimbo ya Tunduru Kusini na Kaskazini, mgombea huyo aliahidi kuimaliza kero ya muda mrefu inayowakabili wakazi wa Tunduru na vitongoji vyake ya ukosefu wa barabara iliyodumu kwa kipindi cha zaidi ya miaka 54 ya Uhuru, kwa kuhakikisha inatengenezwa kwa kiwango cha lami.
Alirudia ahadi hiyo akiwa Lindi, Mtwara, Katavi, Kigoma, Rukwa, Dodoma na Tabora akisisitiza kuwa nchi haiwezi kuendelea ikiwa hakuna barabara zinazoungana na barabara kuu. Kuhusu viwanda, amekuwa akihoji ni nani walioviua vilivyokuwapo?
Akiwa katika mikoa ya Kusini, Mtwara Lindi Ruvuma, aliahidi Serikali yake itahakikisha inajenga viwanda vya korosho ili kuondokana na uuzaji wa korosho ghafi kunakoipunguzia mapato Serikali. Katika mikutano yake aliyoifanya Korogwe na Handeni, Tanga alisema ACT itawajengea viwanda vya kusindika matunda ili kuongeza ajira na pato kwa serikali.
Akiwa Mbulu mkoani Manyara, aliahidi kujenga kiwanda cha pareto pamoja na viwanda vidogovidogo vya usagaji wa mazao ya ngano, dengu na mahindi yanayopatikana kwa wingi kwenye maeneo hayo.
Maoni ya wananchi
Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Ruco), alisema ahadi hizo zinaonekana kuwa nzuri na kujibu vilio vya wananchi lakini tatizo kubwa linatokea katika utekelezaji wake kutokana na mfumo mzima wa kiuchumi.
Alisema rais yoyote atakayepita ili atekeleze ahadi za elimu bure, afya na maji bure atatakiwa kupambana zaidi na mfumo wa uchumi wa dunia ambao hauungi mkono sera hizo za kijamaa.
Mkazi wa Kigogo, Salim Juma alisema ahadi za Dk Magufuli ni nzuri na kwa utendaji zinaweza kutekelezwa lakini tatizo lipo kwenye chama chake ambacho kimekithiri ufisadi na hakipo tayari kwa mabadiliko hivyo kupunguza kasi ya utekelezaji.

No comments :
Post a Comment