Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, October 3, 2015

Uongo, uzandiki na takwimu!


Na Ahmed Rajab
JE, tuziamini tafiti zenye kutegemea takwimu kutabiri nani atashinda, na kwa kiwango gani, katika uchaguzi? Taasisi zenye kutabiri mambo ya uchaguzi zinajinata kwamba utabiri wao ni tofauti na ule wa wapiga ramli kwa sababu wao ni wa “kisayansi” na, kwa hivyo, ni wa kuaminika. Wanalitumia neno “kisayansi” kama neno la kichawi la kutufanyia kiini macho tuamini wanayotuambia.
Hivi majuzi taasisi mbili zisizo za kiserikali, Ipso (ambayo zamani ikijulikana kwa jina la Synovate) iliyo Kenya na ile ya Tanzania iitwayo Twaweza, zilisema kuwa zilifanya tafiti zionyeshazo kwamba lau uchaguzi ungefanywa wakati zilipokuwa zikifanywa tafiti hizo basi Dk. John Magufuli, mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), angeshinda.
Taasisi ya Ipso, iliyofanya utafiti wake Septemba, ilisema kwamba Magufuli angeshinda kwa asilimia 62 na Edward Lowassa, mgombea urais wa Chama cha Demokrasia (Chadema) angepata asilimia 31 ya kura.
Ile ya Twaweza, iliyofanya utafiti wake Agosti na Septemba, ilituambia kwamba Magufuli angeshinda kwa asilimia 65 na Lowassa angemfuatia kwa asilimia 25 ya kura. Matokeo ya tafiti hizo mbili yanafanana. Hilo si jambo la kushangaza kwa sababu kumbe utafiti wa Twaweza ulifanywa na Ipso.

Siku chache baada ya taasisi hizo mbili kutoa matokeo ya tafiti zao, taasisi nyingine, ambayo pia si ya kiserikali na iitwayo Tanzania Development Initiative (TADIP), nayo ilitoa matokeo ya utafiti wake ilioufanya Septemba 4 hadi Septemba 23.
Matokeo yalikuwa tofauti kabisa.Kwa mujibu wa TADIP, Lowassa, ambaye anaungwa mkono pia na vyama vinne vingine vilivyoungana katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),ndiye angeibuka mshindi kwa asilimia 54.4 lau uchaguzi ungefanywa katika kipindi hicho cha utafiti. Magufuli angepata asilimia 40 ya kura.
Katika nchi zilizoendelea mara nyingi utabiri wa tafiti kama hizo huagulia. Tafiti za aina hiyo hutegemea kura za maoni ya idadi fulani ya watu wanaochaguliwa mahsusi kuulizwa maswali kama, kwa mfano, nani watampigia kura au wanakipendelea chama gani.
Takwimu hutumika sana katika tafiti kama hizo. Mara nyingine lakini utabiri waaina hiyo huwa haulingani na matokeo halisi, huenda kombo kabisa.
Mara nyingi ninaposikia matokeo ya tafiti kama hizi hukumbuka maneno aliyoyaandika mwandishi wa Kimarekani Mark Twain mnamo 1906 kwamba kuna uongo wa aina tatu: “Uongo, uzandiki na takwimu.”
Ingawa Twain alisema kwamba aliyanukuu maneno hayo kutoka maandishi ya Benjamin Disraeli, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza (Februari 1874 hadi Aprili 1880 naFebruari 1868 hadi Desemba 1868), kwa hakika hakuna ajuaye nani hasa aliyasema au kuyaandika mwanzo maneno hayo. Walioyapitia maandishi ya Disraeli hawakuyaona humo.
Lililo muhimu ni kwamba matamshi hayo yametumiwa kwa nia ya kuainisha nguvu ya nambari (ya takwimu) na jinsi takwimu zinavyoweza kutumiwa kuzipa nguvu hoja zilizo dhaifu.Wakati mwingine takwimu pia hutumiwa kuupinda ukweli.
Kwa sababu hizo, miongoni mwa nyingine kadhaa, ushauri wangu ni kwamba tusizitie sana maanani tafiti zenye kutabiri matokeo ya Uchaguzi Mkuu. Tusubiri mpaka matokeo halisi yatapotangazwa. Tukifanya hivyo tutaepukana na mengi hususan katika nchi kama za kwetu ambako hatuna uzoefu mkubwa wa namna ya kuzisarifu tafiti kama hizi zinazoweza kuzusha aina ya hofu katika jamii.
Aina nyingine ya hofu ni ile inayozushwa kwa makusudi na wanasiasa kwa kauli zao za kushtua. Mfano mzuri ni matamshi ya hivi karibuni ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya Magufuli. Bulembo alinukuliwa kusema kwamba CCM haitakubali kuiachia Ikulu Ukawa.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva, hakukosea aliposema kwamba matamshi hayo ni ya kushtua na kwamba kuyakataa matokeo ya uchaguzi ikiwa umeshindwa kihalali ni uhaini. Kwa hakika, matamshi kama hayo yanastahiki kulaaniwa na wote wenye kupenda amani.
Viongozi wa CCM wamekuwa wakijigamba kwamba nchi jirani zinaweza kujifunza mengi kutoka Tanzania na jinsi taifa hili lilivyoweza kudumisha amani na kuwa nchi pekee katika ukanda wa Afrika ya Mashariki isiyokumbwa na machafuko. Hoja hiyo ina ukweli. Anayeipinga atakuwa anaipinga kwa ukaidi tu.
La kushangaza ni kwamba miongoni mwa haohao wenye kujigamba na kujitakia sifa kwa amani iliyodumu Tanzania kuna akina Abdallah Bulembo na Nape Nauye, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, wanaoropoka maneno yatayoweza kulitumbukiza taifa kwenye janga la machafuko.
Nauye ndiye aliyesema Juni 22 kwamba CCM lazima ishinde uchaguzi hata kwa “bao la mkono”. Taifa linaweza likasambaratika kwa wepesi wa kufumba na kufumbua macho ikiwa wanasiasa wataachiwa kutoa matamshi kama hayo.
Wanasiasa wenye kustawisha demokrasia kwa kuzifuata kanuni za mfumo wa kidemokrasia, zikiwa pamoja na chaguzi za haki na za uwazi, ndio wanaoweza pia kustawisha amani na usalama. Wakifanya hivyo wanakuwa wanadumisha hali ya utulivu, hali ambayo ni kigezo muhimu kwa maendeleo ya jamii na ya uchumi wa nchi.
Kwa upande mwingine, wanasiasa wenye kuzikanyaga na kuzipondaponda kanuni za kidemokrasia ndio wanaovuruga amani kwa vitendo vyao vya kuzikiuka kanuni hizo. Mifano ya hivi karibuni ni ya wanasiasa wa Burundi na Burkina Faso.
Wanasiasa wa kwetu wanapokuwa wanaropoka maneno ambayo ni hakika yanaweza kuzusha vurugu mtu huduwaa na hujiuliza iwapo wanasiasa hao wamerukwa na akili na kughumiwa. Kama wana akili zao timamu haiwezekani kwamba watathubutu kufungua midomo na kulihatarisha taifa.
Sifikiri kama kuna wengi watakaokataa kwamba tangu uchaguzi wa 2005 chama cha CCM kimeanguka sana mbele ya macho ya Watanzania, wakiwemo hata wanachama na wafuasi wa chama hicho. Miongoni mwa sababu zilizopelekea hadhi yake iporomoke ni kushindwa kwa serikali ya chama hicho kutimiza ahadi ilizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi huo na ule wa 2010.
Bado wananchi wanakabiliwa na shida zisizokwisha za maji safi, za kukatiwa umeme mara kwa mara, za ukosefu wa ajira, bei ghali za vyakula, huduma duni hospitalini na viwango vya chini vya elimu.
Wananchi wa kawaida wanaamka na kulala nazo shida hizo siku nenda siku rudi huku wakiwaona wachache katika jamii, wakiwemo viongozi wa CCM na serikali yake, wakiishi maisha wasiyoweza wao kamwe kuyafikia. Wanawaona wakiwapeleka watoto wao kusoma nje ya nchi, wao wenyewe na walio wao wakenda nje kutibiwa na nyumba zao hazikosi umeme kwa sababu wanaweza kumudu kujinunulia majenereta.
Ile kaulimbiu ya “ari mpya, nguvu mpya kasi mpya” imegeuka povu. Badala yake ufisadi umekithiri, toka ule wa Richmond hadi wa Tegeta Escrow. Kashfa hizo za ufisadi, na kadhaa nyingine, zimewahusisha viongozi wa chama na wa serikali.
Na tusiisahau kashfa nyingine kubwa kabisa iliyowafanya wananchi wazidi kuidharau serikali ya CCM. Hii ni ile kashfa ya mchakato wa kulipatia taifa Katiba mpya. Mabilioni ya shilingi yalitumika kwa mchakato huo wa kuwataka wananchi wenyewe watoe maoni yao juu ya Katiba waitakayo.
Dhamira hiyo ilikuwa ya kusifiwa na ya kupigiwa mfano lakini yuleyule aliyeiagiza itimizwe, yaani mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano, ndiye yuleyule ambaye baadaye aliipiga mwereka na kuiangusha.
Angeweza kusamehewa ingekuwa mchakato wote ule ulikuwa wa tamthilia wa “sadiki, ukipenda”. Lakini kutumia mabilioni ya fedha za wananchi kuwadanganya wananchi ni kitendo kisichosameheka. Labda wenyewe wakubwa wanaona walichokifanya ni mzaha.
Kwa kweli, kama sisi tuna akili zetu timamu na tunayaangalia mambo kijituuzima ubadhirifu wa kiasi hicho cha fedha hausameheki. Kama sisi kweli tuna uchungu na nchi yetu iliyo na uwezekano wa kuwa tajiri lakini iliyofanywa izidi kuwa masikini na viongozi waroho lazima tutafakari kwa kina zaidi.
Kutumia ovyo mabilioni kwa mabilioni ya fedha za wananchi ni sawa na kuwaibia wananchi. Ni kitendo cha jinai. Sitostaajabu nikisikia siku zijazo wananchi wanajitokeza kuwafungulia mashtaka wakuu waliohusika na kashfa hii. Wanaweza wakawashtaki kwa ubadhirifu wa fedha za umma.
Yote hayo ni miongoni mwa yanayowashajiisha Watanzania wengi waunge mkono Ukawa wakitumai kwamba CCM ikishindwa kutapatikana mabadiliko katika mfumo wa utawala. “Mabadiliko” ndio kaulimbiu ya Ukawa katika kampeni za Uchaguzi mkuu ujao.
Tamko hilo baadaye lilichupiwa na kung’ang’aniwa na chama kinachotawala. Mgombea wake wa urais naye pia anasema anataka mabadiliko.
Tunasikia kuwa Rais Jakaya Kikwete ananung’unika faraghani kuwa anabezwa na Magufuli kwa vile mara kwa mara amekuwa akiponda namna serikali ilivyoendesha mambo fulani.
Inasemekana kwamba Kikwete akihisi kuwa Magufuli kwa kufanya hivyo amekuwa kama akimshambulia yeye binafsi. Nadhani baada ya habari hizo kuvuja ndipo Kikwete alipoona haja ya kujitoa kimasomaso na kusema kwamba Magufuli alikuwa na haki ya kuikosoa serikali yake na kwamba hajakosea, alifanya ndivyo.
Pengine hiyo ndiyo azma ya Magufuli, kujitenga na utendaji kazi wa Kikwete na serikali yake, serikali ambayo yeye mwenyewe alikuwa waziri wake kwa muda wa miaka 15 mtawalio.
Swali la kujiuliza ni iwapo Magufuli ataweza kuupa mgongo mfumo uliomuachia awe mgombea wa chama chake. Huu ni mfumo uliozoewa na chama hicho na ndio wenye kukipa uhai. Mfumo huo sio tena ule uliokuwa msingi wa chama hicho.
Hauwezi kuwa hivyo kwa sababu chama hicho hakina tena itikadi yenye kukiongoza. Siku hizi ukiwauliza wakereketwa wa CCM wakueleze yaliyomo kwenye Azimio la Arusha au Mwongozo nina hakika wengi wao watababaika. Hata Mwongozo ni nini hawajui. 

No comments :

Post a Comment