Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, October 18, 2015

Zanzibar! MAALIM SEIF AWAONDOA HOFU WAKIRISTO!

Maalim Seif Sharif Hamad
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amesisitiza nia yake ya kuendelea kuwaunganisha wananchi visiwani hapa bila kujali itikadi za kisiasa, udini, ukabila au eneo mtu husika anakotoka.

Maalim Seif ambaye pia ni mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), alitoa kauli hiyo juzi alipokutana na viongozi wa dini ya kikristo waliopo Zanzibar katika Kituo cha Utengamano Welezo.

Alisema akiwa kiongozi wa nchi, atahakikisha wananchi wote wanapata haki sawa na hakuna atakayebaguliwa au kuonewa kwa misingi yoyote.

Katika mazungumzo na viongozi hao ambao pia walipata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali kuhusiana na ustawi wao, Maalim Seif alisema atahakikisha kuwa anailinda Katiba ya Zanzibar ambayo inatoa uhuru wa kuabudu kwa wananchi wote.

Alisema msingi mkubwa wa chama chake ni haki sawa kwa watu wote, na kubainisha kuwa suala la chama hicho kuhusishwa na udini ni propaganda ambazo hazina ukweli wowote.
Naye Askofu Daniel Kwilemba, aliahidi kuufikisha ujumbe huo kwa waumini wa dini ya Kikristo waliopo Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, ili waweze kuelewa ukweli kutokana na mitazamo ya watu mbalimbali kuhusiana na CUF na mtazamo wa kiongozi wao juu ya mustakabali wa Wakristo waishio Zanzibar.

Kwa upande wa Mufti Mkuu wa Zanzibar, Shekh Omar Kabi, akifungua mkutano wa kamati ya viongozi wa dini na wadau wa uchaguzi kuhusiana na mwenendo wa kampeni na uchaguzi mkuu, aliwataka viongozi wa dini ya Kiislamu na Kikristo pamoja na waumini wao kujenga tabia ya kuvumiliana na kupendana hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu.

Alisema uchaguzi mkuu usiwe chanzo cha waumini wa pande hizo mbili kufarakana na badalada yake waishi kwa upendo, amani na utulivu.

Kamati ya viongozi wa dini Zanzibar pamoja na wadau wa uchaguzi, walitoa maadhimio saba yanayohusiana na mwenendo wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Maadhimio hayo yametokana na kikao cha pamoja kilichowakutanisha viongozi hao wa dini na wadau wa uchaguzi pamoja na taasisi mbalimbali zikiwamo Tume ya Uchaguzi, vyombo vya vya dola, taasisi za vijana, asasi za kiraia na waandishi wa habari.

Akisoma maadhimio hayo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Ismali Asakheir, alisema wameadhimia kutoa maadhimio hayo baada ya kuzingatia na kutafakari juu ya hali halisi ya nchi na mustakbali wake na kuona umuhimu wa amani na utulivu.

Aliyataja baadhi ya maadhimio hayo kuwa ni wadau wa uchaguzi wapewe elimu kuhusu urai, sheria za nchi na zile za uchaguzi zifuatwe na kuheshimiwa kikamilifu, vyombo vya ulinzi na usalama vitumie sheria na busara na si kutumia nguvu kupita kiasi kwa raia kabla na baada ya uchaguzi, Tume ya Uchaguzi iwe huru na isibanwe na pia isiwe na upendeleo kwa chama chochote ili kuepusha migogoro.

Maadhimio mengine ni kauli na vitendo vitumiwavyo na wagombea, wanachama na mashabiki wa vyama mbalimbali ziwe nzuri zisizoleta uchochezi na uvunjifu wa amani, vyombo vya habari vitoe fursa kwa usawa kwa vyama vyote vya siasa, wadau wa uchaguzi kutoka pande zote wawe tayari kukubali matokeo baada ya kupiga kura na baada ya kupiga kura watu wawe huru kuendelea na shughuli zao zilizo halali.

Alisema kuwa wote kwa ujumla wanatambua upendo, mshikamano, na haki ni nguzo kuu katika kuimarisha na kudumisha amani katika nchi yao.

“Tunatambua na kuthamini rehema za Mola wetu kutuzawadia amani katika nchi yetu na kwa hiyo tuna wajibu wa kuilinda kwani ikipotea hakuna atakayesalimika,” alisema.

Hata hivyo, alisema kuwa katika kipindi hiki wanapaswa kuwa makini na kufanya kazi kwa bidii kuitunza amani ya nchi kwani kuzembea au kufanya kinyume cha matarajio kwa mmoja wao, iwe kwa bahati mbaya au kwa makusudi, kunaweza kuwa na madhara makubwa katika nchi.

“Bado tunatiwa moyo kuwa tunaweza kukaa pamoja na kutafakari kwa nia ya kuwezesha uchaguzi huu uwe huru, wa haki na amani licha ya tofauti zetu za kidini, kisiasa, rika na majukumu,” alisema.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments :

Post a Comment