Rais Jakaya Kikwete
Dar es Salaam. Wakati sintofahamu juu ya hatima ya uchaguzi visiwani Zanzibar ikiendelea, Rais Jakaya Kikwete ameiamuru ofisi yake kusaidia kufanikisha mazungumzo baina ya mgombea wa urais wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad na Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama, Jenerali Davis Mwamnyange.
Kwa mujibu wa taarifa ilitolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu kwa vyombo vya habari jana, hatua hiyo ilifuata baada ya uongozi wa CUF kumuomba Rais Kikwete afanikishe mazungumzo na Mwamnyange juu ya masuala yanayoendelea visiwani humo.
Hata hivyo, undani wa mazungumzo yanayotarajiwa kufanyika baina ya pande hizo mbili hayakuelezwa kwa kina.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa awali Rais Kikwete alipokea malalamiko juu ya utendaji wa baadhi ya polisi visiwani humo wakati huu wa uchaguzi na kwamba amemuagiza Mkuu wa jeshi hilo, Ernest Mangu kuchunguza madai hayo na kutoa mrejesho baada ya uchunguzi.
Kwa kipindi cha siku sita sasa Zanzibar imeingia kwenye sintofahamu na mgogoro wa kikatiba baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 na kuamua urudiwe upya.
Siku mbili zilizopita, Maalim Seif aliwaambia wanahabari kuwa baada ya uamuzi huo wa ZEC, amekuwa akifanya juhudi za kutafuta ufumbuzi kwa kukaribisha mazungumzo na viongozi wanzake wa kitaifa wakiwamo Rais Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein, lakini wamekuwa wakimpiga chenga.
Dk Shein ni mgombea wa urais wa CCM visiwani humo.
Hata hivyo, Ikulu jana ilieleza kuwa madai ya Maalim Seif siyo ya kweli kuwa Rais Kikwete alikataa mazungumzo bali maombi aliyoyapelekewa kutoka CUF ni malalamiko juu ya vitendo vya polisi na kuomba mazungumzo na Mwamunyange.
Taarifa hiyo iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu, Salva Rweyemamu ilisema Rais anaguswa na hali ya kisiasa na kiusalama inayoendelea visiwani humo kama walivyo Watanzania wengine.
“Rais amekuwa akifanya kazi bila kuchoka kutafuta ushauri kwa siku kadhaa zilizopita katika kutafuta njia na suluhisho la amani juu ya hali inayoendelea Zanzibar,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
No comments :
Post a Comment