Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, November 5, 2015

Kila la kheri Dk. John Magufuli, kwaheri JK!

NA EDITOR

5th November 2015.
Katuni.
Rais wa awamu ya tano wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, leo anaapishwa rasmi kushika wadhifa huo.
 
Hatua hiyo inafuatia ushindi wake kwenye Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
 
Tunapenda kumpongeza Dk. Magufuli kwa ushindi huo na pia anaingia kwenye vitabu vya historia kama miongoni mwa waliowahi kushika wadhifa huo wa juu nchini Tanzania.
 
Tanzania ni miongoni mwa nchi na hasa kwenye Bara la Afrika ambazo zimejenga utamaduni wa viongozi wake wa juu kuachiana madaraka kwa amani.
 
Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, ndiye aliyeasisi utaratibu huo alipong’atuka mwaka 1985 na kumwachia kijiti Ali Hassan Mwinyi.
 
Rais Mwinyi alipomaliza muda wake mwaka 1995, nafasi yake ilichukuliwa na Benjamin Mkapa, ambaye aling’atuka mwaka 2005.
 
Rais Kikwete alichaguliwa kushika wadhifa wake katika mwaka huo na leo anaachia madaraka kwa Dk. Magufuli kwa amani bila kumwaga damu.Nchi nyingi hasa katika Bara la Afrika, zina matatizo ya viongozi kung’ang’ania madaraka na hata kuwapo mapinduzi ya kijeshi, hali ambayo husababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe kutokana na baadhi yao kuwa na uchu wa madaraka.
 
Kitendo cha Tanzania kujenga utamaduni wa kupokezana vijiti kwa viongozi wenzake, ni jambo la kupongezwa.
 
Pia tunampongeza Rais Kikwete kwa kuongoza taifa hili kwa miaka 10 na kung’atuka kwa njia ya kidemokrasia.
 
Rais Kikwete amefanya mengi tu mazuri, lakini pia utawala wake ulikabiliwa na changamoto nyingi ambazo sasa zinapaswa kufanyiwa kazi na utawala mpya wa Dk. Magufuli.
 
Dk. Magufuli anapokea nchi huku wananchi wake wakiwa na kiu ya mabadiliko, jambo ambalo lilidhihirika wakati wa mikutano ya kampeni.
 
Pia bahati nzuri wagombea wa vyama mbalimbali walipigania uongozi kwa kuahidi jambo hilo, ambalo linapaswa kufanyiwa kazi katika uongozi mpya chini ya Dk. Magufuli.
 
Dk. Magufuli ana deni la kulipa Watanzania kwa imani waliyoonyesha kwake na kumpa dhamana ya kuongoza taifa hili.
 
Baada ya zaidi ya miaka 50 ya Uhuru, Watanzania wanataka kuona vita dhidi ya maadui watatu; umaskini, ujinga na maradhi vikimalizika.
 
Bila shaka baada ya kuzungukia sehemu mbalimbali za Tanzania, Dk. Magufuli atakuwa anaelewa vizuri changamoto anayokabiliwa nayo ya kupambana na maadui hao.
 
Pia kero nyingine ambayo inawaumiza Watanzania, ni ya rushwa na ufisadi.
 
Vita dhidi ya rushwa na ufisadi, isiishie majukwaani tu, bali vyombo vinavyotakiwa kukabiliana na matatizo hayo, lazima vipewe meno.
 
Tunamshauri Dk. Magufuli atekeleze ahadi yake ya kuunda mahakama maalum ya kushughulikia kesi za rushwa na ufisadi.
 
Hata hivyo, ni mategemeo yetu kuwa moja ya majukumu ya mwanzo ya Dk. Magufuli itakuwa kuhakikisha mvutano wa sasa kuhusiana na Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar inamalizika.
 
Siyo jambo zuri kuona upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa na mvutano wa kisiasa wakati upande wa pili ukiwa umetulia.
 
Tunaelewa kuwa Dk. Magufuli anapokea mzigo mzito kutoka kwa mtangulizi wake, hata hivyo, tunaamini atatimiza imani na matarajio ya wananchi wake.
 
Aidh, tunamtakia kila la kheri Rais Kikwete mapumziko mema na maisha mazuri ya kustaafu baada ya utumishi uliotukuka wa miaka 10.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment