NA EDITOR
Katika ziara yake hiyo kwenye hospitali hiyo kubwa kuliko zote za serikali nchini, Rais Dk. Magufuli alikutana na mambo mengi ambayo yamekuwa ni kero sugu kwa wagonjwa.
Kwanza, tunapenda kuchukua fursa hii kumpongeza Rais Magufuli kwa uamuzi wake wa kutoa kipaumbele katika ziara zake kwa hospitali hiyo ambayo kwa hakika ndiyo kimbilio la Watanzania wengi na wa kada mbalimbali.
Tunadhani Rais Dk. Magufuli anastahili kupewa pongezi hizo kutokana na ukweli kwamba angeweza kuamua kutembelea taasisi yoyote ile na kuacha matatizo makubwa yanayoikabili hospitali hiyo yaendelee kuwasumbua wananchi.
Tunaamini kwamba huu ni mwanzo mzuri kwa Rais huyu wa Awamu ya Tano na kwa hakika ameanza kuleta matumaini makubwa kwa wananchi hususan wanyonge na wa vipato vya chini ambao kwa vyovyote vile, hawana uwezo wa kwenda nchi za nje kufuata matibabu.
Katika ziara hiyo, Rais Dk. Magufuli pamoja na mambo mengine, alielezwa ubovu wa vifaa muhimu vya kupima magonjwa mbalimbali vya CT- Scan na MRI.
Aliambiwa kuwa vipimo hivyo vilipata hitilafu na kushindwa kufanya kazi kwa zaidi ya miezi miwili sasa.
Aliambiwa kuwa vipimo hivyo vilipata hitilafu na kushindwa kufanya kazi kwa zaidi ya miezi miwili sasa.
Baada ya kuelezwa hali hiyo na kupata maelezo kutoka kwa baadhi ya wagonjwa wanaoteseka hospitalini hapo wakisubiri kudra za Mwenyezi Mungu za matengenezo ya vifaa hivyo muhimu ndipo wapimwe na kuanza tiba, Rais Dk. Magufuli alionekana dhahiri kusikitishwa sana.
Na ndipo alipoagiza vifaa hivyo viwe vimetengenezwa ndani ya wiki moja na si zaidi ya wiki mbili na vianze kufanya kazi ya kutoa huduma kwa wagonjwa.
Kuonyesha jinsi alivyoguswa na kusikitishwa na jambo hilo, Rais Dk. Magufuli aliagiza mmoja wa wagonjwa waliokuwa wakisubiri majaliwa ya kutengenezwa kwa vifaa hivyo ambaye alivunjika uti wa mgongo, apelekwe popote pale haraka akahudumiwe na kama tatizo ni fedha, yuko tayari kutoa kutoka katika mshahara wake.
Rais Dk. Magufuli alikwenda mbali zaidi katika kuonyesha kusikitishwa kwake na suala hilo pale alipoonyesha kushangazwa na maofisa kwenda ziara za Ulaya huku wakiacha mashine hizo muhimu kwa wagonjwa, zikiendelea kubaki bila matengenezo. “Mnaharibu kwa makusudi vifaa vya serikali ili wagonjwa waende hospitali binafsi ambako mashine hizo haziribiki...Mnasema mashine hizo zimeharibika kwa zaidi ya miezi miwili, hazitengenezwi, lakini mnakwenda Ulaya!,” alisema Rais Magufuli kwa masikitiko.
Tumefarijika kuona kwamba tunaye Rais anayewajali wananchi wake kiasi hicho.
Kinachosikitisha vifaa hivyo muhimu ni kwamba viliharibika muda mrefu na gazeti hili mbali ya kuripoti, pia liliandika tahariri ikisisitiza mamlaka husika kuona umuhimu wa kushughulikia tatizo hilo, lakini halikufanyiwa kazi.
Rais Dk. Magufuli, uliyoyaona Hospitali ya Taifa Muhimbili iliyo karibu kabisa na Ikulu, ambayo pia ni kioo cha hospitali nyingine zote za serikali nchini, ni kielelezo tosha cha hali ya hospitali nyingi za serikali hapa nchini.
Tunajiuliza kama hali iko hivyo Muhimbili iliyoko jijini Dar es Salaam, walipo mawaziri na watendaji wote wa serikali, je; hali ya hospitali nyingine zilizoko pembezoni mwa nchi kama Namtumbo, Karagwe, Tunduru, Kakonko na kwingineko, ikoje? Tujisahahihishe; tusisubiri Rais afike ndipo tujirekebishe.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment