FEDHA zinazodaiwa kutolewa katika kanisa moja Dar es Salaam na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, zimezua kizaazaaa kanisani hapo.
Nyalandu anaelezwa alichanga Sh milioni 50 kuunga mkono ujenzi wa Kanisa la ‘Holy Ghost Anglican Church’ la Kimara Resort.
Hatua hiyo imetokana na msimamo wa waumini wa kanisa hilo jana, kuibua hoja baada ya ibada ya asubuhi kanisani hapo.
Walihoji hatua ya Mchungaji wa kanisa hilo kushindwa kutoa hesabu ya mapato na matumizi.
Fedha hizo inadaiwa zilikabidhiwa na Nyalandu, Septemba 6 mwaka huu kuunga mkono juhudi za waumini kujenga kanisa hilo.
Jana waumini hao walimtuhumu Mchungaji wao, John Solomon wakidai amekuwa akitumia madaraka yake kwa kusimamia kila kitu yeye mwenyewe.
Baada ya kumalizika ibada jana, mmoja wa waumini alichukua kipaza sauti huku Mchungaji Solomon na wenzake wakiwa katika chumba cha kubadilishia nguo.
Muumini huyo alisema ana jambo analotaka kuzungumza la moyoni mwake.
Hata hivyo, Mchungaji Solomon alitoka na kumnyang’anya kipaza sauti.
Waumini wengine walinyanyuka wakitaka kijana huyo aachwe azungumze huku wengine wakitaka azuiwe.
“Hii madhabahu inatumika vibaya huko nje na mimi ndiye niliyeibua mada humu kanisani… sasa nataka kusema yaliyo ndani ya moyo wangu…,” alisema.
Hapo Mchungaji Solomon alimtaka kijana huyo kufuata utaratibu wa kwenda ofisini kwake na kuwasilisha malalamiko yake.
Kitendo hicho kilisababisha waumini wengine kutaka kutoka nje huku mzozo mkubwa wa maneno ukiibuka.
“Jamani huu si utaratibu wa kanisa letu… malalamiko yanapaswa kuwasilishwa ofisini, tulieni Mchungaji atoke ndipo nanyi mtoke,” alisikika muumini mmoja.
Waumini hao walitulia na kuanza kuimba wimbo wa kutoka lakini kijana huyo aliendelea kulalamika huku akizongwa na baadhi ya viongozi wa kanisa hilo.
Wakati waumini wakiendelea kulumbana mlangoni, waandishi wa habari walimsogelea Mchungaji wakitaka kumuhoji lakini alirudi ndani ya kanisa.
Aliporudi kanisani mlango ulifungwa na baadaye ilielezwa kuwa alikuwa ameondoka katika eneo hilo.
Akizungumza na wandishi wa habari, kijana huyo ambaye alijitambulisha kwa jina la Daniel Katumbi alisema amechoshwa na vitendo vya Mchungaji Solomon.
Katumbi alisema baadhi ya waumini sasa wanataka aondolewe.
“Mchungaji anatumia madaraka yake vibaya, tangu amehamia hapa anaendesha kanisa vibaya, amevunja kamati ya ujenzi iliyoteuliwa na kanisa.
“Amewaweka watu wake, hatusomewi taarifa ya mapato na matumizi.
“Tulipoleta hoja hii kanisani alitutuhumu kuwa sisi ni wachawi na alimtolea maneno ya kejeli Mhazini wa kanisa Mathayo Makundi,” alisema.
Muumini mwingine, Salome Mhina, alisema mgogoro huo ulianza mwishoni mwa Oktoba mwaka huu baada ya waumini kutaka wasomewe taarifa hiyo.
Mhina alisema baada ya kuhoji matumizi ya Sh milioni 50 Novemba mosi, mwaka huu, Mshauri wa Mchungaji, Yuda Mtweve aliwasomea.
Alisema Mtweve aliwaeleza kuwa Sh milioni 18 zimekwisha kutumika jambo ambalo liliwashangaza na kujiuliza zimetumikaje huku ujenzi ukiwa umesimama.
“Tangu Mchungaji Solomon ahamie hapa Kimara Januari 15 mwaka jana akitokea kanisa la Mtakatifu Nicolaus la Ilala, kanisa letu limekumbwa na mgogoro.
“Ametuvuruga, viongozi wengi wamejiuzuru kwa sababu hashauliki.
“Kila kitu anataka akisimamie na kukiendesha mwenyewe na hata vitabu vya fedha anatunza yeye… Mhazini wa kanisa yupo kama ushahidi tu.
“Waumini wengi wamehama na hata moyo wa kutoa umepungua. Awali watu walikuwa wanatoa sadaka hadi milioni mbili leo hii tunakusanya Sh laki moja,” alisema.
Alisema mara kwa mara wamekuwa wakiomba kukaa kikao na Mchungaji huyo lakini amekuwa akikataa.
“Tumeomba kikao cha majadiliano mara kadhaa amekataa na amekuwa akitutolea lugha mbaya ikiwa ni pamoja na kutuita wachawi.
“Tumeshaandika barua kwa Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk. Valentino Mokiwa atusaidie lakini bado hatujajibiwa.
“Tunaomba huyu Mchungaji ahamishwe sisi hatumtaki tena,” alisema.
MTANZANIA lilimtafuta Askofu Dk. Mokiwa kuzungumzia mgogoro huo lakini simu yake ya mkononi haikuweza kupatikana.
No comments :
Post a Comment