Mwanasiasa Mkongwe Zanzibar na waziri wa zamani wa mambo ya ndani, Ali Ameir Mohamed, amesema haikuwa muafaka kwa mawaziri wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kutoka Cuf kujivua nyadhifa zao kutokana na mgogoro wa kikatiba ulioibuka visiwani humo baada ya kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28, mwaka huu.
Alisema hayo wakati akizungumza na Nipashe mjini Zanzibar jana kuhusu hatua ya mawaziri sita na manaibu waziri watatu kujivua nyadhifa zao kwa madai serikali awamu ya saba imefikisha ukomo wa kuendelea kubakia madarakani Novemba 2, mwaka huu.
Alisema serikali ya Zanzibar ni ya Umoja wa Kitaifa (SUK), hivyo viongozi wa vyama vinavyounda serikali hiyo kwa maslahi ya Zanzibar na wananchi wanapaswa kukaa pamoja na kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo, badala ya kujivua nyadhifa zao.
“Kwenye migogoro viongozi wanatakiwa kusimama imara kusaidia wananchi, uamuzi walioufanya ni sawa na nahodha kukimbia abiri ndani ya meli baada ya kupata dhuruba baharini, ” alisema Amer.Alisema mgogoro wa Zanzibar unaweza kutafutiwa ufumbuzi kwa mazungumzo na kuepuka mivutano ya maslahi ya kisiasa.
Alisema kama mawaziri hao wa Cuf waliweza kuitumikia Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa muda wa miaka mitano wanashindwa vipi kukaa na Rais na kutafuta njia muafaka za kumaliza matatizo yaliyojitokeza na kusababisha uchaguzi kushindwa kukamilika.
“Tatizo la uchaguzi wa Zanzibar linaweza kupatiwa ufumbuzi kwa kufuata Katiba. Baadhi ya wanasheria waache kufanya tafasiri ya vifungu kwa utashi wao kisiasa kwani wanawachanganya wananchi wanaotaka kuujua ukweli,” alisema.
Amer alisema wanasiasa wanatakiwa kuangalia chanzo cha kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi huo na kuangalia njia bora za kuukamilisha bila ya kuweka mbele maslahi binafsi ya kisiasa.
Alisema sababu kubwa ya muundo wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) kubadilishwa na kuingizwa wajumbe kutoka vyama vya siasa wakiwamo Cuf na CCM lengo lake kubwa ilikuwa ni kuondoa mazingira ya kutokuaminiana.
“Haiwezekani kiongozi unataka kuongoza wananchi wakati wa raha, wakati wa shida unakimbia, hiyo siyo sifa ya uongozi,” aliongeza kusema.
Hata hivyo, alisema kitendo cha mawaziri hao kujivua nyadhifa zao wakati tayari wakiwa wamelipwa mafao yao ni sawa na usanii na wameshindwa kutatua mgogoro uliojitokeza kwa maslahi ya Zanzibar na wananchi wake.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment