Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, ilieleza kuwa Rais Kikwete ameamua kuitangaza Novemba 5, mwaka huu (leo), kuwa sikukuu na pia siku ya mapumziko.
“Rais Kikwete amefanya uamuzi huo ili kuwawezesha Watanzania kushiriki sherehe za kuhitimisha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne na kuingizwa madarakani Mheshimiwa Dk. John Magufuli, kuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Ikifafanua, taarifa hiyo ilikariri taarifa nyingine iliyotolewa Dar es Salaam jana (Jumatano, Novemba 4) na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi (KMK), Balozi Ombeni Sefue, ikieleza kuwa Rais Kikwete ametoa uamuzi huo kwa mujibu wa mamlaka aliyo nayo chini ya Kifungu cha 3 cha Sheria ya Sikukuu za Kitaifa.
Dk. Magufuli (56) aliyekuwa akipeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), anaapishwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo kuwa Rais wa Tano wa Tanzania baada ya kushinda katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25.Alivuna asilimia 58.46 ya kura halali zilizopigwa na Watanzania zaidi ya milioni 23 na kuwazidi wagombea wengine saba, akiwamo Edward Lowassa, aliyepata asilimia 39.97 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambaye pia aliwakilisha muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya NLD, NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF).
Wengine waliojitosa katika kinyang’anyiro cha kuwania urais na kuachwa mbali na Magufuli ni Anna Mghwira wa ACT Wazalendo, Hashim Rungwe wa Chaumma, Chifu Lutalosa Yemba wa ADC, Macmillian Lyimo wa TLP, Janken Kasambala wa NRA na Fahmy Dovutwa wa UPDP.
NI HISTORIA
Uamuzi wa Rais Kikwete kutangaza sikukuu ya kitaifa katika siku ya kuapishwa kwa mrithi wake unaelezewa kuwa ni wa kihistoria kwani kumbukumbu zinaonyesha kuwa jambo hilo halikuwahi kutokea hapo kabla.
“Hii ni heshima kubwa. Nadhani siku hii ya Magufuli ni ya kihistoria kwa taifa… binafsi sikumbuki kama marais waliopita akiwamo huyu wa awamu ya nne (Kikwete), waliwahi kuenziwa namna hii katika siku ya kuapishwa kwao,” mstaafu mmoja wa nafasi ya juu katika ofisi nyeti ya serikali aliiambia Nipashe jana kwa sharti la kutotajwa jina.
Kabla ya awamu mpya ya Magufuli inayotarajiwa kuanza baada ya kuapishwa kwake leo, marais waliotangulia ni Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Kikwete aliyeingia madarakani baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.
MARAIS NANE KUSHUHUDIA
Katika hatua nyingine, Marais Robert Mugabe wa Zimbabwe, Paul Kagame wa Rwanda na Jacob Zuma wa Afrika Kusini ni miongoni mwa wakuu wa nchi nane wanaotarajiwa kushuhudia shughuli ya kuapishwa kwa Dk. Magufuli leo.
Taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ilithibitisha jana kuwa wakuu hao watakuwapo, na wengine ni Yoweri Museveni wa Uganda, Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uhuru Kenyatta wa Kenya, Philipe Nyusi wa Msumbiji na Edger Lungu wa Zambia.
“Kenyatta na Mugabe wanatarajiwa kuingia nchini leo (jana) jioni… wengine watawasili kesho (leo) asubuhi,” alisema mmoja wa maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje.
Juzi, taarifa rasmi ya Wizara ya Mambo ya Nje ilieleza kuwa katika shughuli hiyo, Malawi itawakilishwa na Makamu wa Rais, Saulos Chilima, Namibia itawakilishwa na Naibu Waziri Mkuu, Netumbo Nandi-Ndaitwah.
Kadhalika, nchi nyingine zitakazokuwa na wawakilishi wake katika shughuli ya leo ni Burundi, Comoro, Angola, Botswana, Lesotho, Madagascar, Mauritius, Norway, Oman, Sudan Kusini, Sweden na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Nyingine ni Marekani, Shelisheli, Swaziland, Uingereza, Algeria, Misri, Benin, Denmark, Ethiopia, Finland, Ufaransa, Ghana, India, Japan, Kuwait, Uholanzi na Nigeria.
Aidha, wakuu wa mashirika ya kimataifa na kikanda watakaohudhuria ni Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Ulaya na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Wengine wanaotarajiwa kuhudhuria shughuli hiyo ya leo ni wabunge wateule wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambao walishinda katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25. Hao wametakiwa na Ofisi ya Bunge kufika wakiwa na vyeti vyao vya ushindi.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment