Jeshi la Polisi nchini, limeendelea kupiga marufuku maandamano yaliyokuwa yamepangwa kuanza kufanywa jana bila kikomo na wafuasi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupinga unyonywaji wa demokrasia dhidi ya aliyekuwa mgombea wao wa urais wake, Edward Lowassa, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Lowassa alishindwa katika uchaguzi huo kwa kupata kura asilimia 39.97 dhidi ya asilimia 58.9 za mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, aliyeibuka na ushindi katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi nchini, Paul Chagonja, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, (IGP) Ernest Mangu, aliwaeleza waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa maandamano hayo yalikuwa ni batili kwa sababu wafuasi wa vyama hivyo vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD walikiuka taratibu za uombaji wa kibali kwa kutuma barua ya maombi muda mfupi kabla ya maandamano.
Chagonja alisema kwa mujibu wa taratibu za uombaji wa kibali, unatakiwa kuomba siku mbili au saa 48 kabla ya maandamano.
“Kwanza tulibaini maandamano hayo yanaweza kuwasumbua wakazi wa Jiji wakashindwa kuendelea na shughuli zao, lakini pia walichelewa kutupatia barua za kuomba kibali licha ya kuwa zilikuwa zinasema waliomba Oktoba 31 na Jeshi la Polisi liliwanyima kibali,” alisema Kamishna Chagonja.
“Kwanza tulibaini maandamano hayo yanaweza kuwasumbua wakazi wa Jiji wakashindwa kuendelea na shughuli zao, lakini pia walichelewa kutupatia barua za kuomba kibali licha ya kuwa zilikuwa zinasema waliomba Oktoba 31 na Jeshi la Polisi liliwanyima kibali,” alisema Kamishna Chagonja.
Juzi, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, alipiga marufu maandamano hayo kwa madai kuwu barua hiyo haikubainisha muda wa kuanza na mahali watakapopita. Kamishna Kova alisema: “Kufanya maandamano yasiyo na kikomo haiwezekani kwani yataathiri shughuli za jijini hapa na kuwapa usumbufu mkubwa wananchi wa kushindwa kufanya shughuli zao. Vile vile, yanaweza kuleta uvunjifu wa amani, haiwezekani Polisi wakawa na kazi ya kulinda waandamanaji tu.”
KUMWAPISHA MAGUFULI
Sambamba na hilo, Kamishna Chagonja alisema jeshi hilo limejipanga kikamilifu kulinda usalama wa raia na mali zao katika tukio la kuapishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, kesho.
Dk. Magufuli alitangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kuwa mshindi wa urais Oktoba 29, mwaka huu na kukabidhiwa cheti cha ushindi Oktoba 30.
“Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, limejipanga vyema kuhakikisha usalama wa raia na mali zake unaimarishwa katika siku ya kuapishwa kwa Dk. Magufuli. Tunawaomba wananchi watupe ushirikiano kwa kutoa taarifa waonapo tukio la uvunjifu wa sheria,” alisema Kamishna Chagonja.
Mbali na hilo, Kamishna Chagonja aliwashukuru wananchi kwa kuwa watulivu katika kipindi chote cha uchaguzi na kuwataka kufanya hivyo hadi siku ya kuapishwa kwa Rais mpya.
Pia, alivishukuru vyombo vya habari kwa kutoa ushirikiano na kuhabarisha umma kwa weledi na kuimarisha amani ya nchi.
Kuhusu watu waliokamatwa wakati wa uchaguzi kwa makosa mbalimbali, Chagonja alisema jeshi hilo linaendelea kuwashikilia watu kadhaa, ambao hata hivyo, hakutaja idadi yao.
Alisema wengine wameshapelekwa mahakamani na wakapewa dhamana na wengine wanaendelea kukamatwa na kwamba hakuna takwimu sahihi za wanaoshikiliwa.
KAULI YA UKAWA
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitendo cha Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene, alisema barua za kuomba kibali cha kufanya maandamano ziliandikwa na uongozi wa kanda.
Alisema kwa sasa chama hicho kina jumla ya Kanda 10 hivyo kila kanda inaweza kuratibu shuguli zake. “Kuhusu masuala ya maandamano unapaswa kuzungumza na viongozi wa kanda ambao ndio walioandika barua, pia wanaweza kukueleza kama wameandamana ama la,” alisema Makene.
Nipashe ilimtafuta kwa njia ya simu Ofisa wa Kanda ya Pwani, ambayo ndio iliandika barua ya kuomba kibali kwenda kwa Jeshi la Polisi, bila ya mafaniko kutokana na simu yake yake kuita bila ya majibu.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment