Mbunge mteule wa Jimbo la Mikumi, Joseph Haule, maarufu Profesa Jay
Mbunge mteule wa Jimbo la Mikumi, Joseph Haule, maarufu Profesa Jay amesema vijana ndiyo watakaoleta mabadiliko nchini.
Akizungumza mwanzoni mwa wiki hii, Profesa Jay, ambaye ni mbunge mteule wa Jimbo la Mikumi kwa tiketi ya Chadema, alisema vijana wanatakiwa kujituma ili kuwa chachu ya mabadiliko katika taifa lao.
Alisema jambo hilo wanatakiwa kulifanya sasa bila kujali itikadi za vyama vyao.
Profesa Jay, ambaye alipata umaarufu kutokana na kibao chake cha kisiasa cha “Ndio Mzee”, alisema kukaa vijiweni na kulalamika hakuwezi kuwa suluhu ya matatizo yao, hivyo wakijituma kufanya kazi kwa pamoja watawezesha Taifa kusonga mbele.
Profesa Jay alisema kuwa na malengo ni njia mojawapo itakayomwezesha kijana kujitambua na kujituma katika kile anachokifanya, ili kutimiza malengo aliyojiwekea kwa kipindi mwafaka.
“Ukiangalia vijana maeneo ya vijijini wanakuwa na malengo ya kuhakikishe wanafanya mambo kadhaa kama ‘kujenga nyumba yangu ya kuishi ndipo nioe mke’. Hii ni tofauti na vijana wengi wa mijini. Naamini hata wao wakiweka malengo Taifa litasogea mbele kutoka hapa tulipo,” alisema Profesa Jay.
Alieleza kuwa kijana yeyote anayeona ana uwezo wa kufanya mabadiliko anatakiwa kufahamu kuwa siasa imeisha na huu ni wakati wa kufanya kazi.
Alisema kwa sasa mabadiliko ni lazima ili kuyavuta maendeleo kwani ndiyo kitu cha msingi zaidi, akibainisha kwamba ni kwa vijana wote nchini na si Mikumi pekee.
“Mimi ni kijana nimefikiria kufanya kazi itakayowakwamua vijana wote nchini, nathamini uamuzi na namna walivyoniamini wananchi wa Mikumi kwa kunipa nafasi niwaongoze, lakini natambua uwapo wa vijana Tanzania nzima,” alisema Profesa Jay.
Alisema anachoweza kufanya sasa ni kuwasaidia wasanii wenzake kuwasemea na kutafuta njia za kuwakomboa.
Hata hivyo alisema licha ya kuingia katika siasa hana mpango wa kuachana na muziki.
“Wapo wachungaji ambao waliingia katika siasa hawakuacha kuhubiri, wapo wafanyabiashara ambao nao waliingia huko hata nao hawakuacha biashara zao, kwa upande wangu siwezi kuacha nitaendelea kufanya muziki mpaka mwisho wa maisha yangu,” alisema Profesa Jay.
No comments :
Post a Comment