Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah
Dodoma. Taasisi ya Bunge na Jeshi la Magereza mkoani Dodoma, zinatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa madai ya kushindwa kuwalipa Sh850 milioni makandarasi wa ujenzi wa jengo la utawala.
Bila kutaja kiasi cha fedha, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah amethibitisha taasisi yake kudaiwa huku akisema anawatambua Magereza na siyo makandarasi hao wanaotaka kuiburuza mahakamani.
Hata hivyo Dk Kashililah alisema Magereza watalipwa katika kipindi cha wiki moja kuanzia sasa.
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma, Antonino Kilumbi naye alithibitisha kudaiwa na makandarasi hao na kutaja sababu zinazokwamishwa wasilipwe kuwa ni kutokana na madai yake kwa Bunge.
Deni hilo linatokana na kazi ya ujenzi wa jengo la utawala katika kipindi cha Bunge la Katiba ambalo makandarasi hao wanadai kuwa walijenga sehemu za benki, ofisini, hospitali, maegesho ya magari na maeneo mengine.
Wawakilishi wa makandarasi hao 21, Hassan Mvungi na Muhidini Kyaburani walisema wamekamilisha taratibu za kuziburuza mahakamani taasisi hizo, ikiwamo kumpata wakili wa kuwatetea ili wapate haki yao.
Kyaburani alisema fedha hizo wanadai kwa muda mrefu tofauti na makubaliano yaliyokuwapo awali na kusababisha baadhi yao kuishi kwa hofu ya kunyang’anywa nyumba zao walizoweka rehani benki ili wapate mkopo wa ujenzi huo.
“Tumepanga kwenda mahakamani, kama itakuwa vipi itabidi tujikusanye wote hata kuandamana sisi na watoto wetu, maana tulifanya kazi kwa moyo wa kizalendo baada ya kuambiwa tuunganishe nguvu kuisaidia Serikali yetu, lakini tunaanza kufilisiwa tukijiona,” alisema Mvungi.
No comments :
Post a Comment