Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, December 12, 2015

China: Rafiki wa Afrika au mkoloni mpya?

Image result for flag of china

Siku chache zilizopita, kulikuwa na mkutano kati ya China na nchi za Afrika ujulikanao kama Forum on Africa China Coo-peration uliofanyika jijini Johannesburg nchini Afrika ya Kusini.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi wa nchi za Afrika wakiwemo marais na mawaziri wakuu. Rais John Magufuli hakuhudhuria labda ni katika kutekeleza ahadi ya kupiga marufuku safari za nje ya nchi.
Uhusiano kati ya China na Afrika haukuanza leo. China ina historia ya kufanya biashara na Afrika karne nyingi kabla ya wakoloni kutoka Ulaya kutia mguu barani Afrika.
Katika kipindi cha karne moja iliyopita, uhusiano wa China na Afrika umekuwa katika awamu tatu. Mosi, China kama mfadhili na rafiki wa vyama vya ukombozi Afrika.
Pili, China kama mshirika katika umoja wa nchi zisizofungamana na upande wowote zama za vita baridi wakati huo nchi za Afrika na zile za Asia zikiitwa nchi zinazoendelea.
Tatu, awamu hii China yenye nguvu kubwa iliyoendelea kiviwanda, kiuchumi na kijeshi inaigeukia Afrika iliyo bado masikini kama mshirika kibiashara.
Katika hali hii, China inaiijia Afrika ikiwa na sifa moja sawa na nchi za Magharibi, ima kama muwekezaji, mshirika kibiashara au mfadhili wa miradi ya maendeleo barani Afrika.
Katika medani ya kimataifa, nchi yoyote inapoijia nchi nyingine kwa sura hizi sheria zinazotawala kwenye uhusiano huo ni zile za mnyonge na mwenye nguvu.
Ndiyo maana tunauliza, China inapoisogelea Afrika kupitia hicho kinachoitwa China-Afrika Forum inafanya hivyo kama rafiki au mkoloni mpya kwa Afrika?
Afrika ni bahari ya rasilimali
Katika andiko ‘China is both a tantalizing opportunity and a terrifying threat’, Moeletsi Mbeki anasema “Mabadiliko makubwa ya kiuchumi na viwanda yanayotokea China yanahitaji kiasi kikubwa cha maliasili.
“Africa, a very resource-abundant continent is now of greatest interest to China hence the basis for current economic and diplomatic ties.”
Kwamba bara la Afrika ambalo ni tajiri wa rasilimali hivi sasa linaivutia zaidi China na ndiyo msingi wa uhusiano uliopo baina ya China na Afrika kiuchumi na kidiplomasia.
Miaka ya hivi karibuni, China imekuwa muwekezaji, mnunuzi, muuzaji na mfadhili mkubwa wa nchi za Afrika hasa zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara na kuipiku Marekani na nchi za Ulaya.
Kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia, biashara kati ya China na Afrika inakua kwa kiwango cha asilimia hamsini kwa mwaka. Mwaka 2014 pekee, biashara hiyo ilifikia Dola 50 bilioni za Marekani.
Kwa kiasi kikubwa, biashara kati ya China na Afrika inahusu ununuzi wa rasilimali kutoka Afrika. Kwa mfano mwaka 2008 pekee, asilimia thelathini ya mafuta ya China yalinunuliwa kutoka Afrika.
Nchi za Angola, Sudan na DR Congo ndiyo wauzaji wakubwa wa mafuta kwa China huku Angola ikitoa asilimia 13, Sudan asilimia saba na DR Kongo asilimia 4.4 ya mafuta yaliyoingizwa China kutoka Afrika.
Kwa upande wake, China inajihusisha na ujenzi wa miundombinu barani Afrika kama vile barabara za lami, majengo makubwa makubwa, reli, viwanda huku ikiziuzia nchi za Afrika bidhaa mbalimbali za bei nafuu.
Katika mkutano uliofanyika hivi karibuni kati ya China na nchi za Afrika nchini, China iliahidi kuzisaidia nchi za Afrika Dola 60 bilioni ndani ya miaka mitano ijayo.
Bara tajiri kwa rasilimali linasaidiwa Dola12 bilioni kwa mwaka na China halafu viongozi wake wanafurahia na kushangilia huku wakimpongeza na kumshukuru Rais wa China, Hu Ji Tao kwa ukarimu wake.
Kwangu mimi, hii ni fedheha kwa bara la Afrika kwa sababu utajiri wake unatosha kulifanya bara hili lijitegemee bila kuhitaji msaada, ukarimu wala ufadhili wa nchi yotote ile si Marekani, nchi za Ulaya wala China.
Zaidi ya nusu karne nchi za Afrika bado zimeshindwa kujitegemea zikisubiri misaada au mikopo inayoitwa ya uwekezaji kutoka China, Marekani, Umoja wa Ulaya na Japan.
Mkoloni au mkombozi?
Zama za ukombozi wa bara la Afrika, China pamoja na nchi nyingine za kijamaa na kikomunisti kama Cuba na Urusi zilikuwa zikivisaidia vyama mbalimbali vya ukombozi. Wakati huo China ilikuwa rafiki wa kweli wa Afrika.
Lakini hivi sasa China hii yenye njaa ya rasilimali kutoka Afrika kwa ajili ya kuendesha uchumi na viwanda vyake siyo tena ile China ya zamani. Uhusiano kati ya Afrika na China ni uhusiano kati ya aliye nacho na asiyenacho.
Tukubali tusikubali, China sasa ni mkoloni mpya kwa Afrika angalau kwa maana ya kiuchumi kama zilivyo Marekani na nchi za Ulaya zinavyoitazama Afrika kama shamba la rasilimali.
China yenyewe haijioni kama mkoloni kwa sababu haitafuti kuzitawala nchi za Afrika au kuzilazimisha kufuata matakwa yake na sera zake kwa kuwa haiweki masharti yoyote yale katika uhusiano wake na nchi za Afrika.
Viongozi wa Afrika wamepumbazwa na ‘uungwana’ huu wa China kiasi kwamba zinaiona China kama mkombozi wao kiuchumi pasipo kujua kwamba nchi zao zinavyotazamwa na China ni kama zinavyotazamwa na Ulaya na Marekani-makoloni ya rasilimali.
China kutokuingilia mambo ya ndani hakuifanyi nchi hiyo yenye uchu na njaa ya rasilimali za Afrika iwe rafiki wa bara hili. Ushahidi wa maneno hizi ni kampuni za China kulaumiwa kwa tabia kama za kibeberu barani Afrika.
Kuweka mbele masilahi ya China, ufisadi, kuingiza wafanyakazi kutoka China hata kwa kazi zinazoweza kufanywa na wazawa wa nchi za Afrika.
Tuhuma nyingine ni kunyanyasa wafanyakazi wazawa, kuwafanyisha kazi katika mazingira magumu kwa malipo kiduchu, kushiriki kuiba rasilimali za Afrika kama vile mafuta kule Angola, Nigeria na Sudan au magogo kule DR Kongo.
China hivi sasa ni mshindani mkubwa wa Marekani na nchi za Ulaya kugombea rasilimali za Afrika. Nchi za Afrika zinapendelea uhusiano nayo kuliko nchi nyingine kwa kuwa hauna masharti kama vile kuwapo kwa uwazi, demokrasia na kupiga vita rushwa na ufisadi.
Kwa sababu hiyo, viongozi wengi wa nchi za Afrika ambao wanasifika kwa udikteta nchi mwao wanaona China ndiyo rafiki wa kweli kwa kuwa haiwabani kuwatendea haki raia wao hivyo kuendelea na tabia zao.
Katika mazingira haya, matendo mengine mabaya yanayofanywa na kampuni za Kichina katika nchi za Afrika hufumbiwa macho. Kuna nchi wachina wamewapiga risasi na kuwaua wafanyakazi wazao kwa kudai haki zao.
Uharibifu wa mazingira, ukiukwaji wa sheria na taratibu za nchi za Afrika unaofanywa na Wachina hata hapa Tanzania ni dalili tosha kwamba China tuliyoijua kama rafiki siyo hii inayokuja kufanya biashara na kuvuna rasilimali za Afrika.
Ukarimu usigeuke sumu
Kama tulivyoona China imejipambanua kama ‘mshirika mwema’ wa Afrika kwa kuwa hafanyi kama kaka mkubwa. China imeteka au tuseme imekonga nyoyo za viongozi wa Afrika.
Wadadisi wa mambo wanatahadharisha kwamba uhusiano baina ya China na Afrika usipoangaliwa unaweza kugeuka sumu kwa bara hili.
Serikali za nchi za Afrika hazifanyi juhudi kuzibana kampuni ya Kichina zisizinyonye nchi zetu na yaheshimu sheria za ajira na utunzaji wa mazingira.
Kwa mfano, Naibu Waziri wa Jimbo la Kusini nchini Zambia, Elijah Muchima alipotembelea mgodi wa makaa ya mawe wa Collum Desemba 2009 na kukuta hali mbaya inayowakabili wafanyakazi alisema;
“We would rather be poor than to subject our citizens to inhuman conditions. Government will not tolerate such attitudes of enslaving our own people.”
Jambo la ajabu mwaka mmoja baadaye yaani 2010 wamiliki wa mgodi huo walipowapiga risasi wafanyakazi waliokuwa wakiandamana kupinga kufanya kazi katika mazingira magumu, kiongozi huyo huyo alisema, “Zambia inaheshimu uwekezaji kutoka China.”
Rais wa Angola, José Eduardo Dos Santos aliwahi kukataa bei ya juu iliyotolewa na kampuni moja ya China iliyotaka kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta (Oil refinery) nchini humo. Rais Dos Santos aliwaambia, “Tunao washirika wengine.”
Uhusiano sawa, lindeni masilahi yetu
Viongozi wa Afrika wasifurahie uhusiano na China pekee bila kulinda masilahi ya nchi zao na raia wao pamoja na kuhimiza uhawilishaji wa teknolojia kutoka China ili Afrika isiendelee kuwa tegemezi kwa nchi hiyo kama ilivyodumu kuwa tegemezi kwa Marekani na za Ulaya.
Kwanza kibiashara, kinachofanyika ni China kununua malighafi kutoka Afrika na kutuuzia vitu vya bei ya chini kulinganisha na bidhaa za Marekani na Ulaya pia viwango vyake ni vya chini.
Kuongezeka kwa kampuni za Wachina barani Afrika kunakwenda sanjari na ongezeko la wafanyakazi Wachina jambo ambalo linaathiri soko la ajira barani Afrika.
Kufurika kwa bidhaa za viwango na bei za chini kutoka China barani Afrika na kwa upande mwingine Afrika kusafirisha malighafi kwenda nchini humo kunaweza kuuwa viwanda vyetu na hivyo kuathiri ukuaji wa uchumi wetu.
Afrika itakuwa imepata laana ya rasilimali au kwa rasilimali zake kuvunwa na China kama zinavyovunwa na mataifa ya Ulaya na Marekani huku tukiachiwa ardhi isiyo na misitu na mashimo ya migodi.
Kwa kumalizia, hatupaswi kuona yanayofanywa na China barani Afrika kama uhisani kwa bara hili na watu wake.
Tunapaswa tuangalie uhusiano wetu na nchi hiyo kwa umakini wa hali ya juu kwani waswahili walisema ‘kikulacho ki nguoni mwako’.     

No comments :

Post a Comment