Zikiwa zimetimia siku 47 sasa tangu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha, kufuta matokeo ya uchaguzi huo, vikao hivyo vimekuwa vikifanyika huku umma ukiwa njia panda juu ya kinachozungumzwa kutokana na kugubikwa na usiri mkubwa. Jana viongozi hao wakuu wa kitaifa walikutana kwa mara ya saba Ikulu mjini hapa, huku waandishi wa habari wakizuiwa kupata taarifa yoyote kuhusiana na mazungumzo ya kikao hicho.
Viongozi waliokutana jana ni Rais Dk. Ali Mohammed Shein, Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais, Balozi Seif Ali iddi, Makamu wa Pili wa Rais na marais wastaafu, Amani Abeid Karume na Ali Hassan Mwinyi, ambao walikutana kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 8:00 mchana. Alipoulizwa na Nipashe kuhusiana na mazungumzo hayo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai (hashiriki mazungumzo hayo), alisema chama chao hakijui chochote kinachozungumzwa katika vikao hivyo kwani havihusiana na chama.
“Vikao vinavyoendelea kufanyika Ikulu ambavyo vinawakutanisha viongozi wa kitaifa havihusiani na vyama na ndio maana hakuna mwakilishi wa CCM wala Cuf, isipokuwa viongozi wa serikali,” alisema Vuai.
Hata hivyo, licha ya kutopatikana kwa taarifa yoyote kuhusiana na mazungumzo hayo, hali ya amani na usalama visiwani hapa imezidi kuimarika, huku wananchi wakiendelea na shughuli zao za kiuchumi na kijamii kama kawaida.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment