Uchunguzi uliofanywa na Nipashe ukihusisha pia mahojiano na baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa, umebaini kuwa, mwenendo wa serikali ya Rais Magufuli ambayo hadi sasa bado haijawa na Baraza lake la Mawaziri umekuwa ukiwapa matumaini makubwa Watanzania wengi kutokana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa kwa nia ya kumaliza kero mbalimbali katika siku 32 tu za kuwapo madarakani na kuzidi maradufu kasi ya serikali kamili ya Rais Kikwete iliyokuwa na jumla ya mawaziri 55 na kudumu madarakani kwa miaka mitano, sawa na siku 1,825 (mwaka mmoja ni siku 365).
“Hii kasi ya Serikali ya Rais Magufuli inaibua mambo mengi sana. Kwanza inawapa matumaini makubwa Watanzania kwa kuamini kuwa miaka mitano ijayo, kama kasi hii itadumishwa, maana yake taifa litapiga hatua kubwa za maendeleo,” mmoja wa wachambuzi wa masuala ya siasa aliiambia Nipashe.
“Hata hivyo, kasi hii inaibua maswali mazito kuhusiana na kile kilichofanywa na serikali kamili ya awamu ya nne katika kipindi chake cha mwisho ikiwa na mawaziri 30 na naibu mawaziri 25… kwa nini ilishindwa kushughulikia baadhi ya mambo yaliyokuwa wazi kabisa na ambayo Magufuli na wenzake watatu wamefanikiwa kuyafanya katika kipindi kifupi cha mwezi mmoja?. Kwakweli kuna mengi ya kujiuliza,” mchambuzi huyo alihoji wakati akizungumza na Nipashe.
Mchambuzi mwingine aliiambia Nipashe kuwa, utendaji wa serikali ya Magufuli inayoundwa na viongozi wakuu watatu tu, yaani Rais mwenyewe (Magufuli), makamu wake Samia Suluhu na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, tena katika siku 32 tu za kuwa madarakani, unaibua maswali mengi mazito kuhusiana na ufanisi wa serikali ya iliyokuwa na mawaziri 55, huku ikitumikia wananchi kwa miaka mitano.
“Yapo mengi yanayoibua maswali haya, kwa mfano, Magufuli na wenzake wawili wamefanikiwa kufichua mianya ya ukwepaji kodi mkubwa katika Bandari ya Dar es Salaam. Kulikuwa na matumizi makubwa holela ya fedha za umma kupitia sherehe zisizo na idadi, semina, makongamano, posho za vikao visivyo na tija, utitiri wa safari na mambo mengi yaliyoshughulikiwa na Magufuli na wenzake ndani ya mwezi mmoja tu wakati mawaziri wa Rais Kikwete walishindwa kuyashughulikia kwa miaka yote mitano ya mwisho. Yapo mengi ya kujiuliza, kwamba je, ni kweli wote walikuwa wakifanya kazi kwa maslahi ya umma au ya kwao binafsi?”.
“Na je, ni kweli baadhi yao walizidiwa nguvu ya fedha za baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu au na wao wenyewe walikuwa ni sehemu ya mtandao wa hujuma dhidi ya mali za umma?. Kwakweli maswali ni mengi na mazito dhidi ya wasimamizi wa ofisi mbalimbali za umma katika serikali iliyomaliza muda wake,” mchambuzi mwingine aliongeza.
Aidha, katika uchunguzi wake, Nipashe imebaini kuwapo kwa mambo 10 makubwa ambayo Serikali ya Magufuli isiyokuwa na Baraza la Mawaziri imefanikiwa kuyatekeleza kwa mafanikio makubwa licha ya kuonekana kuwa yalishindikana katika kipindi chote cha miaka mitano iliyopita na kuigharimu serikali mabilioni ya fedha.
Baada ya ushindi wake wa asilimia 58.46 ya kura zote halali zilizopigwa katika uchaguzi mkuu Oktoba 25, 2015, Magufuli aliapishwa Novemba 5, mwaka huu na kuanza kazi siku hiyohiyo kwa kumteua George Masaju kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
ALIYOFANYA MAGUFULI KWA SIKU 32
1.SAFARI ZA NJE
Mara baada ya kuingia madarakani, Rais Magufuli alifutilia mbali safari holela za nje alizodai zimekuwa zikiligharimu taifa mabilioni ya fedha kila uchao. Hili alilitolea uamuzi Novemba 6. Akaagiza kuwa safari zote muhimu ughaibuni ni lazima zipate ruhusa yake au ya Katibu Mkuu Kiongozi Ikulu, lengo ikiwa ni kuokoa fedha zinazoweza kutumiwa kwa shughuli nyingine za maendeleo kwa taifa. Akitolea mfano, alisema katika mwaka wa fedha wa 2013/2014 na 2014/2015, taifa lilitumia zaidi ya Sh. bilioni 356 kugharimia safari za nje; jambo ambalo yeye hayuko tayari kulishuhudia.
Hadi sasa, Magufuli ameshaonyesha mfano kwa kuamuru watu wanne tu kusafiri wakitokea ofisi ya ubalozi wa Tanzania Uingereza kwenda kumuwakilisha katika mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Madola kwenye visiwa vya Malta, badala ya watu zaidi ya 50 waliozoea kusafiri katika safari kama hii ya Rais.
Katika serikali iliyokuwa na jumla ya mawaziri na naibu mawaziri 55, jambo hili halikuwezekana hata kidogo, licha ya kelele nyingi zilizokuwa zikipigwa na wananchi mbalimbali akiwamo Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia aliyedai hali ni mbaya na kwamba, Rais Kikwete peke yake alishatumia muda mwingi wa kuwapo madarakani akiwa nje ya nchi na kuligharimu taifa wastani wa zaidi ya Sh. trilioni 4.5 katika miaka 10 ya kuwapo kwake madarakani.
2. UKWEPAJI KODI BANDARINI, TRA
Hili ni eneo mojawapo kati ya mengi yaliyofanywa kwa umahiri mkubwa na ‘jeshi la watu watatu’ la serikali ya Rais Magufuli. Kwa kurejea ahadi yake ya kuhakikisha kuwa Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA) inaongeza mapato na pia kukomesha vitendo vya ufisadi, tayari Magufuli na serikali yake wameibua gumzo kubwa baada ya kufichua ukwepaji kodi uliobaini kuwapo kwa makontenda 2,431 yaliyopitishwa katika Bandari ya Dar es Salaam bila kulipiwa kodi. Awali, yalinaswa makontena 349 yasiyolipiwa kodi na kulikosesha taifa takriban Sh. bilioni 80, hivyo wastani wa mapato yaliyokuwa yamepotea kwa makontena 2,431 ni zaidi ya Sh. Bilioni 557.
Hadi sasa, tayari watu 47 wamekamatwa na Polisi kuhusiana na tuhuma za kuhusika na ukwepaji kodi huo huku baadhi yao wakiwa tayari wamefikishwa mahakamani kukabiliana na mashtaka ya uhujumu uchumi, miongoni mwao wakiwa Ni maafisa wa vyeo vya juu TRA. Hatua kama hizi zilizochukuliwa na serikali ya Magufuli ndani ya siku 32 hazikuwahi kuonekana katika kipindi chote cha siku 1,825 (miaka mitano) ya serikali iliyomaliza muda wake ikiwa na jumla ya mawaziri 55.
3. VIPIMO CT-SCAN, MRI MUHIMBILI
Licha ya serikali iliyokuwa na mawaziri 55 ya Rais Kikwete kufanya kazi kubwa ya kununua mashine za vipimo vya CT-Scan na MRI, bado havikuwa vikitimiza malengo ya kutumikia wananchi kwa asilimia mia moja kwani muda mwingi zilikuwa mbovu. Hata hivyo, muda mfupi tu baada ya kuingia madarakani, Rais Magufuli alivamia Muhimbili na kutangaza maamuzi mazito ikiwa ni pamoja na kumuondoa Kaimu Mkurugenzi na kisha kuamuru mashine hizo zitengenezwe. Hadi kufikia jana, vipimo vyote viwili vilikuwa vikifanya kazi Muhimbili na kuwaondolea kero wananchi, jambo lililokuwa likionekana kuwa haliwezekani kufanyika katika serikali ya awamu iliyopita kwani licha ya ahadi kadhaa kuwahi kutolewa, bado hakukuwa na mabadiliko makubwa.
4.POSHO KAMATI ZA BUNGE
Kwa uda mrefu kumekuwa na malalamiko juu ya matumizi mabaya ya fedha za umma kwa kuwalipa posho wabunge hata katika vikao vya kazi zao za kila siku, vikiwamo vya kamati kuhusiana na mashirika mbalimbali ya umma. Katika siku zake 32, tayari Rais Magufuli kupitia Msajili wa Hazina, Lawrance Mafuru, ameshatangaza kufutwa kwa posho za vikao vya kamati za Bunge na hivyo kuokoa fedha ambazo sasa zinaweza kuelekezwa katika maeneo mengine ya maendeleo. Hili lilishindikana katika serikali ya awamu ya nne iliyokuwa na mawaziri 55.
5.GHARAMA SIKU YA UKIMWI, UHURU
Miongoni mwa maeneo yanayoligharimu taifa fedha nyingi ni sherehe, maadhimisho na pia sikukuu mbalimbali za mwaka.
Serikali ya Magufuli imeepuka gharama hizi baada ya kufutilia mbali gharama za zaidi ya Sh. milioni 200 zilizokuwa zitumike katika maadhimisho ya Siku ya Ukimwi mkoani Singida, zaidi ya Sh. bilioni zikaokolewa kutoka katika madhimisho ya Siku ya Uhuru na kuelekezwa katika kujenga barabara ya lami kutoka Mwenge hadi Morocco jijini Dar es Salaam, fedha nyingine Sh. milioni 215 zikaokolewa kutoka katika tafrija ya wabunge kujipongeza baada ya kuapishwa na kupelekwa kununulia vitanda 300 vya wagonjwa Hospitali ya Muhimbili na pia mamilioni mengine ya fedha yameokolewa na Rais Magufuli baada ya kufuta kadi za krismasi na mwaka mpya za mwaka huu kwa fedha za umma. Hatua zote hizi hazikuwahi kufanyika katika miaka mitano ya mawaziri 55 wa serikali iliyomaliza muda wake Novemba 5.
6. SAFARI ZA NDANI
Mbali na kudhibiti safari za nje, Rais Magufuli na serikali yake pia amedhibiti safari za ndani baada ya kuagiza kuwa vikao vyote vya kikazi baina ya viongozi wa mikoa vifanywe kupitia teknolojia ya video (video conference) na siyo kusafiri kutoka mkoa mmoja hadi mwingine au kukodi kumbi za mikutano. Hili halikuonekana katika serikali iliyomaliza muda wake.
7. MICHANGO SHULENI MARUFUKU
Hii ni moja ya ahadi za Rais Magufuli. Katika siku zake 32 akiwa madarakani, tayari ameshaagiza utekelezaji wa jambo hili na sasa wanafunzi wa darasa la kwanza watakaoanza mwezi ujao hawatakumbana na rundo la michango na pia wa sekondari pia watasalimika dhidi ya ada na michango. Kero hii ya michango kama ya ulinzi, jembe, madawati, kwanja, uji, na mingineyo ilikuwa sugu katika serikali ya mawaziri 55 iliyomaliza muda wake.
WASOMI WANENA
Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma wa Chuo Cha Kumbukumbu ya Mtakatifu Stefano Moshi (SMMUCo), Dk. Gasper Mpehongwa, anasema katika utawala wa Rais Kikwete, ripoti zilikuwa zinatolewa kwa watendaji wa serikali lakini haamini kwamba walikuwa wakizitendea haki.
Anasema utawala uliopita ulikuwa na baadhi ya viongozi ambao walikuwa hawachukui maamuzi ya haraka na hilo lilikuwa na athari kubwa katika utendaji.
“Mimi naamini Rais alikuwa akipewa summary (muhtasari) wa utendaji kazi katika kila wizara, ila watendaji wake walikuwa wanamuangusha. Hata hili suala la Kamishna wa TRA lingetokea enzi za utawala uliopita lingechukua muda mrefu kuchukuliwa maamuzi. Hii ndiyo tofauti iliyopo,” alisema Dk. Mpehongwa, akisisitiza kuwa aina ya utendaji kazi wa Rais Magufuli na Kikwete ni tofauti na kueleza kuwa katika nchi kama Tanzania, anachofanya Magufuli kwa kuchukua uamuzi wa haraka ndiyo inayohitajika.
Alisema hata Rais Kikwete alipokuwa madarakani alikuwa anasema ana majina ya wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya lakini hadi anaondoka madarakani hakuwahi kuwataja wala kutangaza kuwa amewachukulia hatua.
Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Iringa (IUCo), Essau Ntabindi, alisema kuna mambo mawili ambayo ana amini yanaweza kuwa yalitokea katika utawala wa mawaziri 55 wa Rais Kikwete.
Anasema jambo la kwanza uwezekano kuwa mambo ambayo Rais Magufuli anayafanya sasa, utawala uliopita wa Rais Kikwete ulikuwa hauyaoni ama ulikuwa unayaona lakini ulishindwa kuchukua hatua za haraka.
Anasema Rais Magufuli ameweza kufanya kazi kubwa kwa kipindi kifupi lakini ni lazima awe na Baraza la Mawaziri makini kwani hawezi kufanya mambo yote peke yake.
“Kwa mfano Rais hawezi kujua wizi wa chaki shuleni unavyofanyika au madudu katika halmashauri, lazima atahitaji wasaidizi,” alisema Ntabindi.
Mkurugenzi Mkuu wa Sikika, Irenei Kiria, alisema mambo anayofanya Rais Magufuli kwa sasa hayajawahi kutokea wala kufanywa hapo kabla.
Anasema Rais Magufuli amefanya kazi iliyowashinda mawaziri waliokuwapo katika utawala wa Rais Kikwete na kwamba, hayo yanayofanyika sasa ndiyo waliyokuwa wakiyataka wananchi.
“Kwakweli anayoyafanya sasa Rais Magufuli yameshitua hadi baadhi ya watu wa chama chake kwa sababu sidhani kama walitarajia angeyafanya haya,” alisema Kiria.
Anasema maouvu anayoyafichua Rais Magufuli kwa sasa yalikuwapo kwa muda mrefu na viongozi walikuwa wanayaona lakini walikuwa hawayachukulii hatua, mfano ni ufisadi na ukwepaji kodi bandarini ambao haukuwa jambo la siri.
Mwenyekiti wa Wafanyabishara, Johnson Minja, alikuwa anawaeleza wakuu wa TRA, Bandari na hata mawaziri wa serikali ya Rais Kikwete juu ya namna wafanyabishara wakubwa wanavyokwepa kodi bandarini, lakini mara zote alikuwa akipuuzwa.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment