Mkuu wa wilaya azuia safari za madiwani
NA RAMADHAN HASSAN, KONGWA, MTANZANIA.
MKUU wa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, Bitun Msangi, ametangaza kufuta ziara za mafunzo kwa madiwani wa halmashauri hiyo na badala yake amewataka waende kujifunza vijijini.
Onyo hilo amelitoa juzi, wilayani hapa alipokuwa akizungumza na wananchi wa vijiji vya Mseta, Manhweta na Mseta Bondeni Kata ya Chamkoroma, wakati akikabidhi vyeti na kombe kwa wananchi waliofanya vizuri katika utunzaji wa mazingira ikiwamo ujengaji wa vyoo vya kisasa .
Alisema badala ya kufanya ziara hizo katika halmashauri nyingine, watatakiwa kwenda kujifunza katika vijiji vyao ambako kuna changamoto nyingi na watajadiliana jinsi ya kuzitatua.
“Mfano ulio hai ni hapa kwenye kata hii ambapo kama madiwani wakiamua kuja kujifunza wanaweza wakapata elimu ya kuwaelimisha wananchi wa kata nyingine ambazo mazingira ya usafi bado ni dhaifu,” alisema DC Msangi.
Alisema wananchi wa vijiji vya kata hiyo wameweza kunufaika na mpango wa vyoo vya kisasa kwa asilimia 100 kwa kila kaya kuwa na choo cha kisasa, ikiwemo kibuyu chirizi, shimo la taka na kichanja cha kuwekea vyombo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mipango wa Mradi kutoka shirika la UMATA, Nyomzobe Malimi, alisema vijiji hivyo vimefanikiwa katika ujenzi wa vyoo ikiwemo uwekaji wa vibuyu mchirizo kwa aslimia 100 tofauti na vijiji vingine vinavyofadhiliwa.
Alisema mradi huo umewekewa mikakati ya miaka mitano kuhakikisha unawawezesha zaidi ya watu milioni moja katika wilaya tatu wanafikiwa.
No comments :
Post a Comment