Upinzani ni upinzani. Upinzani ni kutofautiana kwa msimamo, fikra na mitazamo. Baada ya ukimya wa Rais Magufuli wa kuunda Baraza la Mawaziri, hatimaye limetangazwa. Walioteuliwa wameteuliwa. Walioachwa wameachwa. Kuna walioteuliwa na kushangaza. Si hoja yangu hapa.

Namuona Rais Magufuli akialika upinzani Serikalini mwake. Amesogeza mwenyewe tofauti ya misimamo, fikra na mitazamo. Rais yuko njiani kukwama. Wakati alipozungumza na wafanyabiashara Ikulu, Dar es Salaam, Rais Magufuli aliwahakikishi wafanyabiashara wazawa kuwa watakuwa na uhuru na uwezo wa kuwekeza kwenye jambo lolote, likiwamo la mafuta na gesi, kwenye utawala wake.

Rais ana msimamo, fikra na mtazamo kuwa wazawa wanaweza. Lakini,uteuzi wake wa Waziri wa Nishati na Madini leo umepingana na lengo lake. Upinzani. Prof. Sospeter Muhongo haamini kama wazawa wanaweza kuwekeza popote,hasa kwenye mafuta na gesi. Amewahi kusema kuwa wazawa wana pesa za kuwekeza kwenye sharubati/juice tu na si gesi!

Prof. Muhongo amerudi. Na misimamo yake juu ya wazawa imerudi. Upinzani. Rais anakaribisha mabishano na kuwaacha solemba, kinyume na ahadi yake,wafanyabiashara wazawa? Upinzani utaanzia hapo! Au ndiyo mambo ya usiyempenda kaja?
Mzee Tupatupa wa Lumumba, Dar es Salaam.