Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Picha na Mpigapichawetu
Dar es Salaam. Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue amesema maagizo ya Rais John Magufuli ya kutaka fedha zilizokuwa zitumike kwa matumizi yasiyo ya lazima kupelekwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini, hayavunji Sheria ya Ununuzi, wala utaratibu mwingine wa kisheria.
Pia, amelitaka Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) kuwasilisha malalamiko serikalini iwapo linaona kuna baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya wanawabana watumishi na kuachana na utaratibu wa kutoa malalamiko kwenye vyombo vya habari.
Hivi karibuni, Dk Magufuli aliagiza Sh225 milioni zilizokuwa zimekusanywa kwa ajili ya hafla ya wabunge, zikanunua vitanda vya Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Pia fedha zilizokuwa zitumike katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru Desemba 9, Sh4 bilioni zitumike kufanya upanuzi wa Barabara ya Morocco - Mwenge.
Uamuzi huo ulipongezwa na wananchi, huku baadhi wakihoji kuwa ununuzi wa vitanda vya zaidi ya Sh200 milioni na upanuzi wa barabara si jambo la kufanywa ndani ya saa chache, huenda sheria ya ununuzi na utaratibu nwingine wa kisheria umekiukwa.
Akitoa ufafanuzi kuhusu upanuzi wa barabara, Balozi Sefue alisema kilichokuwa kinakwamisha kukamilika kwa mradi huo ni fedha.
“Ninavyojua mimi, upanuzi wa barabara ya Morocco kwenda Mwenge si mradi mpya, utaratibu ulikwishakamilika na kilichobaki ilikuwa ni upatikanaji wa fedha tu.
“Ikumbukwe kuwa watu waliokuwa wamejenga kando ya barabara hiyo tayari walishalipwa fidia na walishaondoka siku nyingi,” alisema Balozi Sefue.
Kuhusu kauli za baadhi ya wakuu wa mikoa kufuta likizo za watumishi, sakata la Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda kuwaweka rumande kwa saa sita maofisa ardhi baada ya kuchelewa kuwasili katika ziara ya kutatua migogoro ya ardhi, Sefue alisema: “Sina undani wa malalamiko hayo.”
“Napata tabu kuchangia kitu nisichokijua, ila niseme tu, tuna mawasiliano kati ya Serikali na wafanyakazi, hivyo kama kuna kitu kinafanyika ndani ya Serikali na Tucta wanaona si kizuri, wangekuja tuzungumze na si kuzungumza katika vyombo vya habari,” alisema.
Alisema Tucta ambayo ilipinga kauli na uamuzi wa viongozi hao wa wilaya na mkoa, wanapaswa kuwasilisha malalamiko yao ili yapatiwe ufumbuzi.
“Likizo ni haki ya mfanyakazi, ila lini aende likizo ni jambo la maelewano kati yao na mwajili. Mwajili anaweza kumtaka mfanyakazi asiende likizo kwa kwa sasa na akamruhusu baadaye.
Kama wana tatizo la msingi walilete, wanaweza kuniandikia barua au wakaliibua katika vikao vyetu,” alisisitiza Balozi Sefue.
No comments :
Post a Comment