Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, December 17, 2015

Sekta za tisa za uwekezaji zitakazolipa zaidi mwaka 2016


Mwananchi
Tunakaribia mwishoni mwa mwaka 2015. Hakuna jipya tena unaloweza kufanya ndani ya wiki moja zaidi ya kujipanga kwa mwaka ujao.
Tofauti na miaka 10 iliyopita, mipango mingi ya kibiashara kwa sasa huenda ikabadilika ili kwenda na sera za Rais John Magufuli ukiachana na viashiria vya kisoko, sekta na uchumi kwa jumla.
Gazeti hili lilifanya mahojiano na baadhi ya watendaji wa kampuni za uwekezaji na wataalamu wa biashara na uchumi nchini ambao walibainisha sekta tisa ambazo zinaweza kulipa zaidi iwapo zitawekezwa mwaka 2016.
Sekta hizo ni kilimo, utalii, ujenzi, nishati, masoko ya mitaji na hisa, Tehama, viwanda, huduma za kifedha na miundombinu.
Kwa mujibu wa wataalamu hao, sekta hizo zinaweza kuwalipa wawekezaji, kwa kuwa mahitaji ya huduma zake ni makubwa na ndiyo mwelekeo wa sera za Serikali ya Awamu ya Tano.
Utalii
Kwa miaka mitano iliyopita sekta ya utalii imekuwa ikikua kwa kasi kiasi cha kuchangia kwa kiwango kikubwa fedha za kigeni kuliko dhahabu kama ilivyoezoeleka hapo awali.
Mhadhiri wa Shule ya Biashara wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Wineaster Anderson, anasema Tanzania ina utulivu wa kisiasa na vivutio vingi vya kitalii ambavyo vinaonyesha kuwa idadi ya watalii itazidi kuongezeka.
“Kwa vyovyote vile mtu atakayewekeza huko atapata faida na biashara yake itakuwa kwa haraka,” anasema.

Hoja hiyo inaungwa mkono na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya ZanSecurities, Raphael Masumbuko anayeeleza kuwa mataifa yote hivi sasa yanamzungumzia Rais Dk Magufuli kwa mazuri, jambo litakalovuta watalii wengi kwa kuwa wengi hutembelea nchi yenye amani na utawala bora.
Benki na huduma za kifedha
Kwa wale wenye nia ya kuwekeza kwenye sekta ya benki na fedha bado ina fursa kubwa mwaka 2016.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa (DSE), Moremi Marwa anasema kwa takriban muongo mmoja uliopita sekta hiyo imekua juu ya wastani wa ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) ambao kwa sasa ni asilimia saba.
“Viashiria vinaonyesha kuwa sekta hiyo itaendelea kukua kwa kasi, kwa sababu benki zinaongeza huduma na bidhaa mpya na kuwajumuisha wananchi wengi zaidi katika huduma za kifedha,” anasema Moremi ambaye pia ni mchambuzi wa masuala ya fedha na biashara.

Viwanda
Hii ni moja ya sekta ambazo bado zinachechemea licha ya kuonyesha viashiria vyema vya ukuaji katika miaka ya hivi karibuni, kiasi cha kuwamo katika sekta tano bora zinazochangia pato la Taifa kwa takriban asilimia 10.
“Wakati huu ni muhimu kutumia fursa ya sekta ya viwanda kukua kibiashara na kiuchumi. Watanzania wanaweza kuwekeza kwenye viwanda vikubwa na vidogo vya usindikaji kutokana ukubwa wa mitaji yao,” anasema Profesa wa Uchumi, Humphrey Moshi kutoka Idara ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Anasema malighafi zipo za kutosha nchini za kuweza kusaidia ukuaji wa viwanda na Rais Dk Magufuli ameshaonyesha nia ya kugeuza Tanzania kuwa nchi ya viwanda, hivyo kutakuwa na nguvu kubwa ya Serikali nyuma yake.
“Wekeza hata kwenye viwanda vidogo vya kufyatua tofali ,kutengeneza madirisha, kushona nguo na viatu, kusindika vyakula kwa sababu kuna soko kubwa siyo lazima uwe na mabilioni,” anasema.

Tehama
Kwa Profesa Anderson, Tehama ni moja ya sekta za kuweka fedha ili upate faida na ukuaji wa kuridhisha wa biashara yako.
Anasema asilimia 60 ya Watanzania ni vijana ambao sehemu kubwa ya maisha yao yanategemea Tehama na pia shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa sasa zinaunganishwa na teknolojia hiyo.
“Kwa sababu ya kizazi hiki cha Tehama na viashiria vya ukuaji wa sekta kwa miaka iliyopita, mtu akiwekeza fedha zake huko itamlipa na biashara itakua kwa haraka,” anasema.

Kilimo cha biashara
Hii huenda ndiyo sekta inayolipa kuliko zote kwa kuwa wataalamu wote wanashauri uwekezaji mkubwa na mdogo ungefanyika huko ili kukuza uchumi wa taifa na kipato cha mtu mmoja mmoja.
“Iwapo changamoto za miundombinu na sera zitatuliwa kuongeza ufanisi wa matumizi bora ya reli na barabara, uhakika wa upatikanaji wa masoko, mnyororo imara wa thamani wa kilimo na uwepo wa maeneo bora ya kuhifadhi mazao, bila shaka sekta ya kilimo na bishara-kilimo zitalipa sana,” anasema Marwa.
Profesa Moshi anasema uamuzi wa Rais kuunda wizara ya maji na umwagiliaji, unaonyesha neema katika sekta hiyo kwa kuwa ujenzi wa mabwawa utaisaidia kilimo kukua kwa kasi kwa kutotegemea mvua pekee.
Anasema iwapo mazao ya kilimo yatazalishwa kwa kiwango kikubwa cha ubora, yatapata soko la kutosha kwa kuwa viwanda vitakuwa vinahitaji malighafi.

Masoko ya mitaji na hisa
Hii ni moja ya sekta ambayo bado Watanzania wengi hawana mwamko nayo, lakini imeonekana kulipa zaidi miaka ya hivi karibuni licha ya kuhusisha wawekezaji zaidi ya 200,000 pekee.
Masumbuko anasema Watanzania wenye nia ya kuwekeza katika sekta hiyo wanaweza kununua hisa za kampuni zilizopo kwenye soko la hisa na kujipatia faida kubwa ndani ya muda mfupi.
“Tumeona kampuni nyingi zimekuwa zikitoa gawio kubwa kila mwisho wa mwaka kwa wawekezaji wake na thamani ya hisa katika kampuni nyingi zilizoorodheshwa imeongezeka zaidi ya asilimia 100,” anasema.
Anatolea mfano kampuni ya bia ya TBL na kampuni ya sigara (TCC) kuwa thamani ya hisa zake zimekua maradufu ambapo miaka mitano iliyopita hisa moja ilikuwa ikiuzwa Sh3,000 lakini sasa ni Sh15,000.

Maendeleo ya makazi
Sekta ya ujenzi inakua kwa haraka na katika ripoti ya ukuaji wa uchumi wa robo ya pili ya mwaka, kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), imechangia kwa kiasi kikubwa kasi ukuaji wa pato la taifa kufikia asiliamia 7.9.
Marwa anasema kuwa sekta ya makazi inakua na kuongeza wawekezaji japokuwa anashauri ili kasi hiyo ikue wawekezaji wanatakiwa kutumia mfuko maalumu wa mitaji ya sekta hiyo uitwao Real Estate Investment Trust (REITs).
Anasema pia uwekezaji huo utafanikiwa iwapo watatumia mikopo ya makazi kupitia benki na taasisi nyingine za kifedha, hasa pale riba zitakapokuwa rafiki na muda wa kurejesha mikopo hiyo utakapoongezwa.
“Tanzania hatuna nyumba za kutosha na kwa kipindi cha hivi karibuni tumeshuhudia mfumo wa bei za makazi.
“Pia, idadi ya watu wanaohama vijijini kuja mijini ni kubwa na kutengeneza mahitaji zaidi ya makazi, hivyo akitokea mwekezaji atakayewekeza kwenye makazi ya bei nafuu, itamlipa sana,” anasema Profesa Anderson.

Ujenzi
Sera ya Serikali kuwekeza katika miundombinu ili kufungua fursa nyingine za kiuchumi, imechangia kukua kwa sekta ya ujenzi.
“Naweza pia kushauri uwekezaji katika shughuli na miradi mbalimbali ya miundombinu kama ya nishati, bandari, na huduma za jamii za maji na umeme.
“Mahitaji ya huduma zitakazonazo na miundombinu hiyo ni makubwa kuliko kiwango cha huduma zilizopo,” anasema Marwa.

Nishati
Neema ya ugunduzi wa kiasi kikubwa cha gesi asilia nchini hadi kufikia futi za ujazo 55.03 trilioni, inaonyesha dalili za wazi kuwa katika mnyororo wa thamani wa sekta hiyo kuna fursa zaidi.
Profesa Anderson anasema uchumi wa nchi unategemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa umeme wa kutosha lakini Tanzania bado inategemea umeme wa maji, hivyo atakayekuja kuwekeza kwenye vyanzo mbadala vya nishati kama gesi asilia, upepo na jua bila shaka atapata soko la kutosha.
Hata hivyo, Anderson anasema ili wananchi wawekeze vyema katika sekta hizo zote wanahitaji zaidi uwezeshaji kutoka serikalini, kwa kuwa baadhi ya sekta kama ya nishati na ujenzi zinahitaji mitaji mikubwa ambayo siyo rahisi Watanzania kuimudu.
“Tusikubali kuacha asilimia 50 ya uwekezaji utawaliwe na wageni ni hatari kwa maendeleo ya nchi yetu. Ni lazima tuwawezeshe wananchi wetu kwa kuwapatia ujuzi maalumu na kuwakopesha mitaji inapobidi, ‘’ anaeleza.

No comments :

Post a Comment