Sababu nyingine ya kuondolewa kwa Dk. Hoseh ni kushindwa kukabiliana na vitendo vya rushwa hususan kwenye upotevu wa mapato ya serikali katika Bandari ya Dar es Salaam.
Taarifa ya kutenguliwa kwa wadhifa wa Dk. Hosseah, ilitolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa jana.
Utenguaji wa Dk. Hoseah umekuja zikiwa zimepita siku nne tu toka ulipofanyika mdahalo uliofanyika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), kujadili hotuba ya Rais Magufuli iliyotolewa Novemba 20, mwaka huu wakati akizindua Bunge.
Katika mdahalo huo, mmoja wa wachangia mada, Bob Chacha Wangwe, mwanafunzi wa Sheria wa Shule ya Sheria UDSM, alihoji kwanini taasisi za kiuchunguzi kama Takukuru na Jeshi la Polisi zimeshindwa kubaini ufisadi mkubwa uliokuwa unafanywa na baadhi ya vigogo wa Mamlaka ya Bandarai (TPA) na Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA) na kulisababishia taifa hasara ya mabilioni ya fedha hadi Rais Magufuli na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa walipobaini.Wakati mdahalo huo ukiendelea, ndipo muongozaji wa mdahalo huo, Dk. Ayoub Ryoba, aliposoma ujumbe alioupokea muda huo huo kutoka kwa Rais Magufuli aliyekuwa anaufuatilia uliosomeka `Suala hilo (kuhusu Takukuru) na mengineyo, ni moja ya hoja zenye mashiko na kwamba zote ‘zitashughulikiwa.’
Kutokana na maelezo hayo ya Rais Magufuli, huenda utenguaji wa Dk. Hoseah umetakana na malalamiko hayo na ahadi aliyoitoa wakati wa mdahalo huo kuwa atashughulikia.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema kufuatia kutenguliwa kwa uteuzi huo, Rais Magufuli amemteua aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola, kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru.
Kadhalika, Balozi Sefue alisema Rais Magufuli amechukua hatua hiyo baada ya kujiridhisha kuwa utendaji kazi wa Takukuru chini ya Dk. Hosseah hauwezi kuendana na kasi anayoitaka.
“Eneo mojawapo la upotevu mkubwa wa mapato ya serikali ni Bandarini na katika Mamlaka ya Mapato Tanzania, hivyo Rais amesikitishwa na kitendo cha taarifa za kuwapo kwa vitendo vya rushwa katika eneo hilo kwa muda, lakini kasi ya Takukuru kuchukua hatua haiendani na kasi anayoitaka,” alisema Balozi Sefue.
Aidha, Balozi Sefue alisema kuwa Rais Magufuli ameagiza kusimamishwa kazi mara moja kwa watumishi waandamizi wanne wa Takukuru ambao walisafiri nje ya nchi licha ya Rais Magufuli kupiga marufuku safari za nje kwa watumishi wa umma ambao ni Mary Mosha, Ekwabi Mujungu, Doreen Kapwani na Rukia Nikitas, ambao walisafiri nje ya nchi licha ya kunyimwa kibali cha safari kutoka kwa Rais ama Katibu Mkuu Kiongozi.
Balozi Sefue aliwataka watumishi wengine wa umma kutii agizo la Rais na kuonya kuwa atakayekiuka atachukuliwa hatua kali.
KAULI YA DK.HOSEAH
Nipashe lilipomtafuta Dk. Hosseah kuhusu utenguzi wa nafasi yake, alisema kuwa hajapata taarifa yoyote ya kuondolewa nafasi hiyo.
“Mimi ndiyo nakusikia wewe sasa hivi. Unaniambia kuwa nimeondolewa, hata sijui. Kama umesikia au kuambiwa na mtu, basi muulize vizuri atakuambia. Mimi ninachojua bado ni Mkurugenzi wa Takukuru,” alisema Dk. Hosseah.
Alisema suala hilo hajalisikia wala hajapewa taarifa yoyote na endapo kama ameondolewa kweli katika nafasi hiyo, angeeleza wala asingeficha.
DK. HOSEAH NI NANI?
Alizaliwa Julai 8, mwaka 1958. Alipata Shahada ya Uzamivu ya Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2007.
Mwaka 1989 alipata Shahada ya Uzamili ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Queen’s, Canada na kabla ya hapo alitunukiwa Shahada ya Sheria UDSM mwaka 1985.
Mwaka 2007, alipata Astashahada ya Uchumi na masuala ya Rushwa kutoka Chuo Kikuu cha Passau cha Ujerumani.
Mwaka 2003 alipata Astashahada ya Utawala Bora, Maadili na Kupambana na Rushwa kutoka Chuo Kikuu cha Birmingham, Uingereza.
Kuanzia Julai 22, mwaka 1995 hadi Novemba, 2006, alikuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Takukuru na baada ya hapo alikuwa Mhadhiri wa Sheria Chuo cha Deplomasia na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kati ya mwaka 1995 na 2006.
Pia aliwahi kuwa Wakili wa Mahakama Kuu na mahakama nyingine na kwamba ana wadhifa wa Mwenyekiti wa Kituo cha Utatuzi wa Migogoro.
Kadhalika, ni mwanachama wa Chama cha Wanasheria wa Afrika Mashariki. Aidha, Dk. Hoseah aliandika machapisho mbalimbali katika utumishi wake yaliyokuwa yanahusu masuala ya rushwa, ushahidi na utawala wa sheria.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment