SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amesema afya yake ni njema na anaendelea na majukumu yake ya kila siku kama kawaida.
Amesema hivi sasa yuko India alikokwenda kufanya uchunguzi wa afya yake katika Hospital ya Apollo na kwamba madaktari wake bado wanaendelea kumfanyia uchunguzi wa macho.
Akizungumza na MTANZANIA jana kupitia simu yake ya kuganjani kutokea nchini India, Spika Ndugai alizungumzia afya yake, aliondoka nchini Desemba 3, mwaka huu kwenda kuwaona madaktari wake ili kufanyiwa uchunguzi wa afya yake.
Alisema, mara ya kwanza alikwenda India mwezi Machi mwaka huu kwa ajili ya uchunguzi wa afya na madaktari walimtaka arejee tena mwezi Septemba lakini alishindwa kutekeleza matakwa hayo ya kitabibu kwa sababu ya kushiriki kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Spika Ndugai alisema baada ya kumaliza uchaguzi mkuu na mkutano wa kwanza wa Bunge la 11, madaktari wake walimshauri aende kwenye uchunguzi jambo ambalo amelitekeleza.
“Niko ngangari, nadhani unanisikia ninavyoongea. Nimekuja India kwa uchunguzi wa afya yangu kama daktari wangu alivyonitaka lakini majukumu yangu yote muhimu nayatekeleza huku nilipo, kila kitu niko vizuri isipokuwa nimeshauriwa pia nifanyiwe uchunguzi wa macho na huo unaenda taratibu kidogo lakini ukikamilika tu narejea nyumbani na nina hakika sikukuu ya krismass nitaisherehekea nyumbani,” alisema Spika Ndugai.
Akizungumzia taarifa kuwa anasumbuliwa na figo na kwamba kabla hajaondoka kwenda India alianguka baada ya kuishiwa nguvu na kukimbizwa uwanja wa ndege akiwa hajitambui, alisema jambo hilo si la kweli.
“Nimeondoka nikiwa natembea mwenyewe na wasaidizi wangu wa Bunge waulizeni watawaambia hilo. Nimefika hapa India nikiwa na nguvu zangu, nahudhuria uchunguzi kwa mujibu wa ratiba kisha narejea hapa nilipofikia na nimekuwa nikiwatembea Watanzania wenzangu waliolazwa hapa kila mara. Hao wanaoeza uongo huo wana lengo la kupotosha wananchi tu,” alisema Spika Ndugai.
Awali Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah alikaririwa na vyombo vya habari akieleza kuwa Spika Ndugai aliondoka nchini kwenda India kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake na kwamba hali ya afya yake ni njema.
No comments :
Post a Comment