WIZARA ya Nishati na Madini imekamata vipande 264 vya madini aina ya Tanzanite yenye thamani ya Sh bilioni 2.5 katika Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA).
Kukamatwa kwa madini hayo kulielezwa jana na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalamani, katika mahojiano yake na MTANZANIA Jumamosi.
“Madini hayo yalikamatwa na Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) ambapo raia wa India, Jain Anarugi, alitaka kuyasafirisha nje ya nchi hivi karibuni lakini sasa tunamshikilia kwa ajili ya uchunguzi zaidi,” alisema.
Alisema madini hayo yametaifishwa na Kamishna wa Madini kwa mujibu wa kifungu namba sita cha Sheria ya Madini ya mwaka 2010 iliyofanyiwa marekebisho mwaka huu.
Alisema takwimu zinaonesha kwamba, katika kipindi cha kuanzia Julai 2012 hadi Novemba, mwaka huu ukaguzi wa madini unaofanyika kwenye viwanja vya ndege kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali likiwamo Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Idara ya Usalama wa Taifa na Idara ya Uhamiaji, umewezesha kukamatwa kwa madini ya aina mbalimbali.
“Hadi sasa tumefanikiwa kukamata madini aina ya Tanzanite, dhahabu, fedha na mengine ya vito yenye jumla ya uzito kilo 2,871.2 katika matukio 87 tofauti ambapo yana thamani ya jumla ya Sh bilioni 16.4 na watoroshaji walichukuliwa hatua.
“Hivyo Serikali haitamvumilia mtu yeyote anayejishughulisha na uchimbaji haramu wa madini, itamchukulia hatua hata kama ikibainika kuwa ni mtumishi wa umma,” alisema.
No comments :
Post a Comment