Na Jenerali Ulimwengu.
KWA mara ya kwanza tangu ufanyike Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba uliopita, nachukua fursa hii kuandika tena katika safu hii nikieleza fikra zangu kuhusu mambo yaliyotokea katika mchakato mzima.
Hii pia ni fursa mwafaka ya kumpongeza Rais John Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa rais wa “awamu ya tano,” na pia kuwapongeza wale wote waliochaguliwa katika nafasi mbalimbali. Hawa ni pamoja na Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, wabunge na madiwani.
Binafsi sikutaka John Pombe Magufuli ashinde, si kwa sababu simpendi au nina tatizo binafsi naye, bali kwa sababu za kimsingi ambazo nilikwishakuzieleza kinaganaga wakati tukielekea kwenye uchaguzi. Naamini kwamba kwa uzito wa historia na umri, si rahisi kupata mabadiliko ya maana yatakayotuletea maendeleo iwapo tunabaki chini ya uongozi wa chama-tawala tulichonacho leo, CCM.
Nchi hii inahitaji mabadiliko kama vile mtu aliyekabwa roho anavyohitaji hewa ya Oksijeni. Huyu akicheleweshwa kwa muda mrefu wa kutosha atakufa. Akicheleweshwa sana lakini si kwa kiasi cha kumuua, anaweza kuibuka akiwa na ubongo ulioumizwa na asiweze kufikiri vyema.
Kwa muda mrefu tumeishi katika kukabwa pumzi kwa namna nyingi, na baadhi yake nitazijadili hapa. Mojawapo ya mambo waliyonyimwa wananchi wa nchi hii ni kuwa na uongozi wenye dhati ya kuwatumikia, na badala yake wamekuwa wakiendeshwa na watawala ambao hata hivyo wamekuwa ni watawala wabovu.
Kila zilipofanyika jitihada za kufanya mabadiliko ya kweli, wamejitokeza wajanja waliowarubuni wananchi kwa kutumia njia mbalimbali na kupindisha malengo ya wananchi na viongozi wao waliotaka mabadiliko ya kweli. Silaha kubwa iliyotumiwa, na inayotumika hadi leo, kuzuia mabadiliko ni ile ya kuzuia kuwapo kwa mifumo mipya ya utawala na uongozi inayojali wananchi wanataka nini.
Kelele zilizopigwa kuhusu umuhimu wa kuwa na katiba mpya zimeishia ndani ya kiini macho cha serikali iliyopita, ambayo imechoma mabilioni ya shilingi kukimbiza kivuli kilichoitwa “katiba mpya” na mwishowe tukaishia kuwa hatuna katiba isipokuwa mikorogo iliyochanganywa na watu ambao hata sifa za kuandika katiba hawana kwani baadhi yao wangetakiwa kuwa gerezani kwa jinai walizotenda dhidi ya wananchi wa Tanzania.
Kila mara wananchi walipoonekana kuchoshwa na hali duni ya maisha na umasikini wa kutupa katika nchi yenye neema, imekuwa rahisi kuwadanganya kwa kuwarushia peremende wamung’unye huku wakibembelezwa kwa kuambiwa kwamba sasa, safari hii, tutapata “maisha bora kwa kila Mtanzania.” Tunawadanganya watu wetu kwa sababu tunadhani hawana uelewa wa kutosha na wataweza kutumaini kwa kila uongo tutakaowaambia.
Lakini huku ni kujidanganya kunakofanywa na watawala. Watu wetu si mbumbumbu kiasi hicho, na mambo mengi ambayo kwayo tunadhani kwamba tumefanikiwa kuwadanganya, wanayaelewa vizuri. Tatizo lao ni kwamba hawana jinsi ya kuweza kuyaondoa. Siku watakapopata uwezo wa kuyaondoa, watayaondoa, na inawezekana wasiyaondoe kwa njia za kiungwana, kwa sababu kwa kuwatendea tunavyowatendea hatujawatendea uungwana.
Ni dhahiri kwangu kwamba watu waliobuni ule mchakato mrefu wa “mabadiliko ya katiba,” wakasababisha kutumika kwa mabilioni ya shilingi, wakawahangaisha wananchi kila kona ya nchi waache shughuli zao wajitokeze kutoa maoni yao, kisha wakakabidhiwa rasimu ya katiba na baada ya hapo wakaitupilia mbali na kuruhusu mchakato pinzani ufanyike kupinga rasimu yao wenyewe, watu hao walifanya uhuni wa kisiasa ulioisabishia serikali hasara kubwa.
Leo hii tunao mawaziri wa zamani walioko gerezani kwa kosa la kuisababishia hasara serikali. Kama hawa mawaziri wanaweza kufungwa kwa kosa kama hilo, ni kwa nini waliosababisha hasara hii katika mchakato bandia wa katiba wasichukuliwe hatua? Ni kwa nini waliwadanganya wananchi na kutumia rasilimali zao katika jambo ambalo hawakuwa na nia ya kulipeleka hadi hatima yake?
Tumejijengea utamaduni wa uongo, watu kuambizana uongo, kudanganyana, kupangiana ghiliba, kufanyiana hadaa, kutapeliana na kuzuzuana kiasi kwamba haya mambo yanayofanywa na wahuni vijiweni (kwa kukoleza baraza) sasa tumeyakweza na kuyafikisha ngazi za juu za utawala wetu na kuyatumia kama njia za kupata manufaa ya “siasa” za kipuuzi, ambazo si siasa bali ni kejeli.
Ndiyo maana nilikubaliana na Rais mteule John Magufuli pale aliposema mbele ya mwenyekiti wake kuwa mwenyekiti Jakaya Kikwete alikuwa amezungukwa na wanafiki, lakini Magufuli angeweza kwenda mbali zaidi na kusema waziwazi kwamba mfumo mzima ni wa unafiki na hakuna anayepona katika hilo. Ni kama vile nguzo zenyewe zinaoushikilia mfumo huo zimetengenezwa kwa fito za unafiki, na ukiziondoa fito hizo, mfumo mzima utaporomoka.
Ndiyo maana naamini kwamba, yeyote anayesema anataka kuleta mabadiliko, hana budi na kuanzia kwenye misingi, na msingi mkuu ni katiba, na katiba hiyo haina budi kuwa ni katiba inayotokana na rasimu iliyoandaliwa kwa kusikiliza maoni ya wananchi.
Katiba inayoandikwa kwa kufuata maoni ya wanachama wa chama-tawala si katiba ya wananchi bali ni katiba ya chama-tawala. Hapa ndipo Kikwete alishindwa kabisa kuwa kiongozi wa Watanzania na kajikuta anakubali imla ya chama chake.
Kama nitakavyoeleza baadaye, hii ni nakisi ya uongozi iliyodhihirika katika mazingira aliyojitengenezea yeye mwenyewe bila kushurutishwa na mtu yeyote. Waziri wake alikwishakutangaza kwamba hakukuwa na haja ya kuandika katiba mpya. Mwanasheria Mkuu naye akasema hadharani kwamba hakukuwa na haja ya katiba mpya. Rais hakumkosoa hata mmoja wa hawa wasaidizi wake, bali yeye akaja na wazo lake peke yake kwamba angeteua tume ikiongzwa na “mwanasheria aliyebobea” kuandika katiba mpya.
Hii nayo ilikuwa ni hatua nyingine ya kuwadanganya wananchi, kwa sababu hatimaye tumeingia katika uchaguzi mwezi Oktoba tukitumia katiba ile ile ya mwaka 1977, bila hata mabadiliko ya kuiondoshea ile sura na ile ladha, na ule muonekano wa chama kimoja. Ni sisi peke yetu, kwa mfano katika ukanda huu bado hatuna wagombea huru na ambao bado tunakubali kwamba matokeo ya uchaguzi wa rais yakiisha kutangazwa , huo ndio mwisho na hakuna fursa ya kuyapinga.
Mimi naamini kwamba Jaji Damian Lubuva ana akili safi kabisa, na ni jaji mwenye maadili yasiyotiliwa shaka. Lakini, ingetokea kwamba, katika mazingira fulani, Jaji Lubuva ametamka kwamba mshindi wa uchaguzi wa urais ni Hashim Rungwe au Fahm Dovutwa, huyo ndiye angeapishwa tarehe 5 Novemba.
Yako mambo mengine ambayo nitayajadili huko mbele, lakini ukweli ni kwamba watawala wetu ni watu wa kufanya mizaha isiyo na maana kwa maslahi ya taifa huku wakijiliwaza kwa kudhani kwamba wanapata faida za kisiasa ambazo kwa kweli ni faida za muda mfupi na za kuwafurahisha wakubwa wenye maono finyu.
Faida ya kweli anayoweza kupata mwanasiasa, (na kwa kweli ni faida anayoweza kupata mtu yeyote anayefanya kazi yoyote kwa ajili ya watu wake), ni ile inayoweza kukubalika na vizazi vya baadaye kama kazi ya sifa na utumishi uliotukukuka. Yaliyobaki ni maandazi na soda za leo na kesho tu. Kwa bahati mbaya, haya ndiyo yanayowasumbua wengi miongoni mwa watawala wetu.
Kwa mtindo huu, tumekuwa tukipoteza muda mwingi kwa kusherehekea wanasiasa wa hadaa na mabarakala walafi. Tukiendelea hivi tutafikia wakati wananchi watachoka, na wanapochoka hakuna Mswalie-Mtume.
Pamoja na kwamba sikumuunga mkono Magufuli, nampongeza na kumuombea asije akawa kama wale waliomtangulia. Anachotakiwa ni kufanya kazi kwa weledi mkubwa, lakini bila kudhani kwamba anajua kila kitu. Afanye kazi kwa kutumia ujuzi mkubwa na akili nyingi za watu wake, ambao wako kila kona ya nchi, na hata nje ya nchi.
Miaka 10 iliyopita, baada ya Jakaya Kikwete kuchaguliwa kwa kishindo kuwa rais wetu, niliandika “Barua Ndefu ya Wazi kwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete”. Nitairejea barua hiyo na maudhui yake huku nikijadili ni wapi nadhani alipatia na wapi nadhani alikosea.
Kisha nitamrejea rais wetu wa sasa, John Pombe Magufuli kwa pongezi zenye maangalizo mawili au matatu.
- See more at: http://raiamwema.co.tz/tupunguze-hadaa-udanganyifu-upoteza-muda-na-siasa-bandia#sthash.brVdgc4q.dpuf
No comments :
Post a Comment