Rais mstaafu, Jakaya Kikwete
Utawala wa miaka 10 wa Jakaya Kikwete ulimalizika Novemba 5, 2015 baada ya mrithi wake Dk John Magufuli kuapishwa. Dk Magufuli anasifiwa, Kikwete analaumiwa.
Kila kona ni Kikwete (JK) namna alivyopambana na ufisadi, alivyosafiri kupita kiasi na kusamehe au kufumbia macho ukwepaji kodi, kuacha deni kubwa la taifa, kulea baadhi ya watendaji goigoi waliobatizwa jina la watendaji mizigo na kushinikizwa kuchukua hatua.
Kama ilivyo kwa Dk Magufuli (JPM) sasa, JK alisifiwa alipoingia madarakani mwaka 2005 akilinganishwa kiutendaji na Mwalimu Julius Nyerere. Mwandishi mmoja alitunga kitabu; “Kikwete: Tumaini lililorejea.” Leo wanadai “Kikwete ni tumaini lililopotea.”
Shujaa leo ni JPM ambaye kila analofanya, hasa anapotumbua ‘majibu’ yaani anavyofuatilia waliokwepa kulipa kodi enzi za utawala wa JK wananchi wanampongeza mtangulizi wake huyo aliyelea na kuwakingia kifua wakwepaji kodi na mafisadi.
Wanamsifu JPM wakidai ameifufua CCM. Hata JK mwenyewe ameendesha kikao cha Kamati Kuu kilichotoka na maazimio ya kumpongeza JPM kwa anayofanya. Kwani JK hakuambiwa kuhusu majipu haya?
Wananchi wanajiuliza JPM ameweza ana nini, JK ameshindwa hana nini? Wanamjadili JK na kuhoji kwa nini hakuchukua hatua thabiti kwa mafisadi? Kosa kubwa la JK ni kutaka kupendwa na kila mmoja, kuwa rafiki wa watakatifu (wazalendo) na watenda dhambi (mafisadi).
Alibeza waliomkosoa, alipuuza waliomshauri; hakuwasikiliza. Hata ajitetee, JK anabeba dhamana kwa mazuri na madudu yote yaliyofanyika akiwa madarakani 2005 – 2015 kama ifuatavyo.
EPA 2005: Katikati ya mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 baadhi ya viongozi na watendaji wakuu wa Benki Kuu Tanzania (BoT) walishiriki kuidhinisha uchotwaji kifisadi wa Sh133 bilioni kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).
Kampuni ya Uhasibu ya Deloite & Touche iligundua wizi huo mwaka 2007 lakini Serikali ilikanusha, badala yake iliiteua Kampuni ya Ernst & Young ambayo pia ilithibitisha wizi huo mwaka 2008.
Wafanyabiashara maarufu, makada wa CCM na maofisa wa BoT walihusika katika kashfa hiyo. Serikali ya JK ilipobanwa iliwaomba wahusika warudishe. Baadhi walirudisha lakini walioshtakiwa na kuhukumiwa kifungo jela ni Rajabu Maranda na ndugu yake, Farjala Hussein.
Richmond: Tabia ya Serikali ya JK kutetea ufisadi ilijitokeza tena katika kashfa kubwa ya kwanza iliyotengenezwa na utawala wake kuhusu zabuni ya kufua umeme iliyotolewa kwa kampuni ya Richmond iliyodaiwa kuwa ya Marekani. Aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa alituhumiwa kuhusika lakini JK alidai ni ajali ya kisiasa. Kuonyesha kuwa sakata la Richmond kweli ni “ajali ya kisiasa” Oktoba 24, JK alibadili kauli na kudai Lowassa alikuwa mhusika mkuu.
Kampuni hiyo, iliyosababisha kufutwa mara tatu kwa washindi wa zabauni hiyo, haikuwa na mtaji wala ujuzi huku mkataba ukisema ingekuwa inalipwa gharama za uwekezaji Sh152 milioni kwa siku bila kujali imezalisha umeme au la. Baada ya kushindwa kuingiza vifaa iliitafuta kampuni nyingine ya Dowans na kuirithisha mkataba huo kinyume cha taratibu, nayo baadaye ikauzwa na kuitwa Symbion Power na imepewa mkataba mnono.
Tegeta Escrow: Picha halisi ya JK ilijionyesha wazi lilipobuniwa kiustadi sakata la kampuni isiyojulikana ya Pan African Power Solutions Tanzania Limited (PAP) kuruhusiwa na Serikali kuchota Sh306 bilioni kutoka akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa BoT.
Akaunti hiyo ilifunguliwa kufuatia mgogoro wa kisheria kati ya wabia wa zamani IPTL (VIP Engineering and Marketing na Mechmar Corporation ya Malaysia) na Tanesco. Mgogoro huo ulitokana na Tanesco kupinga tozo za gharama za uwekezaji zilizokokotolewa na IPTL hivyo ilifunguliwa kesi mahakamani. Uamuzi ulifikiwa fedha ziwe zinawekwa katika akaunti hiyo hadi kesi itakapoisha.
Huku kesi ikiendelea ilielezwa Mechmar imefilisika, Piperlink ikajitokeza kununua hisa za Mechmar hivyo kuwa na haki ya kufanya ubia na VIP, mara ikadaiwa imeuzwa kwa PAP ambayo iliruhusiwa kuchota Sh306 bilioni. PAP ikaamua kununua asilimia 30 ya hisa za mbia mwenzake VIP ambaye aliamua kuwapa mgawo maofisa kadhaa waandamizi, mawaziri na wabunge kupitia benki ya Mkombozi. Kodi ya Serikali haikulipwa na maofisa wa Serikali waliolipwa fedha hizo kupitia benki ya Stanbic hawakujulikana.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alisema fedha hizo ni za serikali, Bunge lilisema fedha hizo ni za umma, lakini JK alisema hakuna ufisadi wowote huku akijua Ikulu iliidhinisha fedha zichukuliwe BoT.
Operesheni Tokomeza: Serikali inawajua majangili wote. Mfano, wakati Serikali iliruhusu dege la Jeshi la Qatar kuja nchini kwa “shughuli za uwindaji”, ilijifanya haijui. Ilifumbia macho hata ndege na wanyama hai akiwamo twiga waliposwaga toka mbugani hadi kutoroshwa na dege hilo mwaka 2010. Badala yake mwaka 2013 ilianzisha Operesheni Tokomeza Ujangili iliyosababisha mateso, majeruhi na vifo kwa wananchi wasio na hatia.
Baadaye JK alidai anawajua majangili 40 na kinara wao anaishi Arusha. Serikali haikuwahi kuomba radhi kwa janga lile isipokuwa iliwafukuza kazi mawaziri wanne ambao wizara zao zilihusika katika operesheni ile. Hadi leo hakuna askari wala ofisa ambaye amechukuliwa hatua.
Safari za anasa: Eneo jingine ambalo JK amewaudhi wananchi tangu alipoingia madarakani ni kuwa mtu wa safari kila siku tena nyingine za kwenda kujitambulisha tu kwa mataifa makubwa kiuchumi kama Marekani, Ujerumani, Ufaransa na Uingereza.
Ripoti ya CAG kuhusu matumizi mabaya ya Serikali ilisema kuwa ziara za Rais nje ya nchi zilisababisha upotevu wa fedha nyingi. Kuonyesha kwamba safari za nje ni kero Novemba 20 JPM alipozindua Bunge alisema ziara za nje zimetafuna fedha za kigeni (alificha safari za Rais), na kwamba kuna maofisa wamefanya ziara nyingi kuliko walivyokwenda kuwasalimia wazazi wao.
Wakati Dk Magufuli hajasafiri anahangaika kusaka fedha, JK amefanya ziara Uingereza, Ethiopia, Comoro na Afrika Kusini.
Deni la Taifa: Serikali ya JK ilifurahia mambo mawili; kukopa bila kikomo, na kusamehe au kuachia wafanyabiashara kukwepa kodi. Mwaka 2005 alipoingia madarakani alikuta Deni la Taifa likiwa Sh10 trilioni lakini hadi anaondoka madarakani lilifikia Sh40 trilioni. Upande wa pili aliacha fedha za kigeni zinazotosha kuendesha Serikali kwa miezi miwili tu.
Kichekesho ni kwamba pamoja na kukopa sana bado Serikali yake ilishindwa kupeleka fedha za maendeleo hadi alipoingia madarakani Dk Magufuli.
Kashfa nyingine: JK alikuwa miongoni mwa maofisa waliotetea ufisadi kupitia ununuzi wa rada. Japokuwa ufisadi huo ulifanyika enzi za Serikali ya Awamu ya Tatu, uliibuka kipindi chake na kutikisa nchi hasa pale ilipobainika zaidi ya Sh73 bilioni zilikuwa zimeongezwa katika ununuzi huo. Je, nani aliongeza fedha hizo na kwa malengo gani? Serikali ya JK ilikataa kuwaadhibu waliosababisha ongezeko hilo.
Pia, Serikali ya JK ilitoa ufafanuzi kuhusu wizi wa Dola za Marekani 118,396,460.36 zilizochotwa BoT kwa ajili ya mradi uliodaiwa wa Meremeta. Wapinzani walipotaka maelezo zilikokwenda fedha hizo Serikali ilidai zilikuwa kwa matumizi ya Jeshi wakati haikuwa kweli. Vilevile, utawala wa JK umemwachia JPM kazi ya kufuatilia undani wa mikataba mbalimbali, wizi na ubadhirifu wa fedha serikalini.
No comments :
Post a Comment