Wanawake hao walipewa talaka baada ya kutotii amri za waume zao ambao waliwataka kutokwenda kupiga kura kutokana na kutofautiana kwa itikadi za vyama.
Akizungumza na waandishi wa habari visiwani hapa mwishoni mwa wiki, Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Ofisi ya Zanzibar, Mzuri Issa, alisema katika uchaguzi huo ambao ulifutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), wanawake wengi walikumbwa na udhalilishaji wa kulazimishwa kupigia kura chama fulani kinyume na ridhaa yao.
Alisema Unguja na Pemba wanawake 47 walikatazwa kupiga kura na walipoamua kwenda, waume zao waliwapa talaka na ndoa zao kuvunjika.
Aisha Mzuri alisema wanawake wengine 24 walitishiwa kupewa talaka ikiwa watahudhuria mikutano ya kampeni ama watapiga kura na matokeo yake hawakwenda kupiga kura.
“Wanawake wanne waliambiwa wasipige kura na walipiga kura, lakini hawakuachwa, mmoja kati ya hao katelekezwa baada ya kukataa amri ya kuhudhuria mkutano wa kampeni,” alisema Mzuri.Aidha, alisema baadhi ya kauli za viongozi pia ziliwadhalilisha baadhi ya wanawake ikiwamo kiongozi mmoja wa juu wa chama fulani alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara wa kufunga kampeni za uchaguzi huko Gombani Pemba alitoa kauli ya kumdhalilisha mwanamke. Hata hivyo, alisema Tamwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwamo kitengo cha wanawake katika Shirika la Umoja wa Mataifa (UN Women), imetoa mafunzo kwa wanawake na wanaume 355 kutoka vyama 20 vya siasa. Alisema wanawake 30 wamegombea nafasi za uwakilishi majimboni na 87 udiwani.
“Ni muhimu kufahamu kuwa kati ya hao wanawake 10 nafasi za uwakilishi sawa na asilimia 33.3 na 20 wa udiwani sawa na asilimia 22.9, wamefaidika moja kwa moja na mafunzo yaliyotolewa,” alisema.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment