Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, December 12, 2015

Watanzania wanamatarajio makubwa kwa baraza la JPM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli akisalimiana na wanahabari baada ya kutangaza Baraza lake la mawaziri Ikulu jijini Dar es Salaam juzi. Picha ya Maktaba.
By Idd Hamis, Mwananchi
Bunge la Kumi na Moja chini ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli litaanza kazi rasmi Januari 26 mwakani takriban mwezi mmoja na nusu hivi kuanzia sasa. Kwa muda wa mwezi mmoja na siku tano tangu aapishwe, Rais Magufuli ametangaza baraza lake la mawaziri huku akiacha nafasi nne za mawaziri.
Kubwa ni kwamba kiu ya Watanzania kujua baraza lake la mawaziri litakuwaje sasa imemalizwa. Ni baraza dogo lenye mawaziri 19 ambalo mpaka sasa ni mawaziri saba tu waliokuwa kwenye Serikali ya Rais Jakaya Kikwete wameweza kurejea kazini.
Rais Magufuli amevunja baadhi ya wizara zilizokuwa katika Serikali ya Rais Kikwete, kuunganisha na kupata wizara mpya ili kutekeleza ahadi yake ya kuunda baraza dogo la mawaziri, hivyo kupunguza gharama kama alivyoahidi.
Jambo linalojadiliwa na watu wa kada mbalimbali ni uamuzi wake mwingine wa kuokoa gharama kwa kufuta semina elekezi kwa mawaziri ambayo ingetumia Sh2 bilioni. Je, uamuzi huu una masilahi mapana kwa Taifa?
Wako wanaosema kwamba siyo kila kitu itabidi kupunguza gharama kwa sababu rais ameteua mawaziri wapya wengi tu ambao hawajawahi hata kuwa manaibu waziri huko nyuma. Ilipaswa wapewe semina elekezi ili rais ajenge timu yake.
Hata hivyo, wengine wanasifu hatua hii ya rais kwani imeokoa fedha hizo ambazo ameelekeza zitumike kuhudumia wananchi. Itabidi wale ambao hawakuwahi kuwa mawaziri wajifunze kwa njia iitwayo ‘on job training’ au mafunzo kazini.
Miongoni mwa wizara ambazo bado Rais Magufuli hajateua mawaziri wake ni wizara nyeti ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano, ambayo imeunganisha wizara mbili; ya ujenzi aliyokuwa akiiongoza Rais Magufuli alipokuwa waziri na ile ya uchukuzi iliyowahi kuongozwa na Dk Harrison Mwakyembe kabla ya kuhamishwa wizara ya Afrika Mashariki. Kwa sasa Magufuli amemteua Edwin Ngonyani kuwa Naibu Waziri wa wizara hiyo.
Wizara nyingine ambayo bado kupatiwa waziri ni wizara nyeti ya Fedha ambayo        imejumuishwa na ile ya mipango ingawa inayo Naibu Waziri, Dk Ashatu Kijaji, Mbunge wa Kondoa Kaskazini aliyekuwa Mhadhiri Chuo Kikuu Mzumbe.
Wizara ya Utalii pia bado haijapatiwa waziri wala naibu waziri kama ilivyo ile ya Sayansi ambayo imepewa na Ufundi; uliokuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Naibu Waziri ni Mhandisi Stela Manyanya.
Hakuna semina elekezi
Rais Magufuli amesema hakutakuwa na semina elekezi. Kwa maoni yangu semina hii ilikuwa ni muhimu ili kupanga staratejia ya pamoja ya timu yake ya Serikali.
Mawaziri wote waliochaguliwa mimi ninaona wanafaa kwasababu hakuna aliyezaliwa na uwaziri. Waziri anayefaa ni yule awezaye kuyaelewa, kuyaelezea na kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sera za Serikali anayoiwakilisha.
Watu wanajiuliza Rais Magufuli ametumia kigezo gani kuteua hawa mawaziri? Kinachotakiwa kwa waziri ni elimu au ujuzi kuhusu wizara anayokwenda kuiongoza na pia uwezo wake wa kujifunza na kumakinika katika wizara hiyo kwa muda mfupi.
Lakini nadhani kubwa alilozingatia Rais Magufuli ni kupata Baraza la Mawaziri la watu waadilifu na anaowaamini. Katika kampeni zake alisikika akisema waziwazi watangulizi wake Rais Kikwete na Rais Benjamin Mkapa waliweka watu ambao waliwasaliti.
Kwa hiyo, nadhani kuchukua Rais Magufuli amechukua muda mrefu kabla ya kutangaza mabara hilo ili kutafuta watu atakaokuwa na imani kufanya nao kazi kwa falsafa yake ya Hapa Kazi Tu. Kwa maoni yangu, tumuamini rais kwa uteuzi alioufanya sasa tusubiri kuona utendaji wao.
Mawaziri waliochaguliwa bila shaka ni watu wenye uwezo wa kuweka malengo ya wizara na kuyaelezea, uwezo wa kufanya maamuzi ‘muhimu’ siyo maamuzi magumu.
Wanapaswa kuandaa mpango kazi wa wizara zao na kuweka vipaumbele vyao kwa mujibu wa falsafa ya Rais Magufuli ya Hapa Kazi Tu huku wakiitafsiri ilani ya chama chao ipasavyo katika kuwahudumia Wataznania.
Ili kuyatekeleza haya, inabidi wawe ni wasikilizaji wazuri na wenye kujifunza haraka majukumu yaliyo mbele yao hasa ikizingatiwa kwamba Rais Magufuli amesema hakutakuwa na semina elekezi kwa mawaziri awamu hii.
Waziri awe mbunifu na mchakarikaji (proactive)
Waziri asitegemee kutafuniwa kila kitu na rais ibaki yeye kumeza tu. Utendaji wa namna hiyo ndiyo uliozaa wale waioitwa mawaziri mizigo. Rais Magufuli amesema safari hii atawasainisha mawaziri mkataba wa kazi.
Mawaziri wa awamu hii wanapaswa wasiwe na makuu, wastahimilivu na wasiochoka kuwatumikia Watanzania, wenye kuchukua maamuzi yenye masilahi kwa Taifa.
Waziri atakayemudu kasi ya Rais Magufuli ni lazima awe mtu anayejua kuwasiliana na mawaziri wenzake na kujenga uhusiano mzuri na watumishi wizarani kwake.
Mawaziri wawe watu wanaojiamini mbele ya wabunge wanapokuwa bungeni, mbele ya wanahabari na Watanzania na waelewe kuwa jukumu lao ni kuwaletea Watanzania mabadiliko wanayoyasubiri kwa hamu.
Waziri awe ‘mwanasiasa’ na mtendaji mzuri
Katika kitabu ‘Making Policy better’ cha Andrew Adonis ambaye ni Mkurugenzi wa Institute for Government nchini Uingereza, ameeleza umuhimu wa kuwa na mawaziri wenye weledi upande wa siasa yaani ushawishi kwa watu na wakati huo huo wanaoweza kufanya kazi vizuri na watumishi wizarani.
Mawaziri wetu mara nyingi huwa wanasiasa wazuri, lakini si watendaji wazuri. Katika hali hiyo maneno yanakuwa mengi kuliko vitendo tabia ambayo wananchi wamechoka kuiona. Mawaziri wa Awamu ya Tano wajipambanue kwa utendaji wao na siyo siasa.
Kutokana na kuwa wanasiasa wazuri, lakini si watendaji wazuri, mawaziri wengi hawatoki kwenda kuwatembelea wananchi na kufahamu kero zao na kuzitatua.
Katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, Rais Magufuli na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wameonyesha wazi kuwa eneo la kazi ni ofisini na nje ya ofisi. Ni wajibu wao sasa kwenda na viwango vilivyowekwa na wakuu wao wa kazi.
Tunataka mawaziri watakaogeuza ndoto za Rais Magufuli alizokuwa akisema kuhusu Tanzania anayoitaka na inayotakiwa na Watanzania kuwa kweli ndani ya muda mfupi ili kurejesha matumaini ya wananchi kwa Serikali yao.
Kuongoza Serikali ni tofauti na kuongoza kampuni
Mara nyingi wale wasiojua hudhani kwamba kuwa waziri ni sawa na kuwa meneja wa kampuni. Ni kweli wote ni viongozi katika nyadhifa zao na kuna mambo ya kiuongozi wanafanana.
Lakini kutokana na mfumo wa utendaji kazi serikalini, huwezi kuhamishia ujuzi kutoka sekta binafsi na kuupeleka kuendeshea Serikali. Ndiyo maana kuna vyuo vya uongozi na masomo ya utawala serikalini.
Tofauti kati ya ulimwengu wa biashara na ule wa siasa na utawala ziko kwenye mambo mawili makubwa; mameneja hupatikana kwa kupima elimu, uzoefu na uwajibikaji.
Mawaziri wanatofautina na umeneja wa kampuni kwani wanapoteuliwa wengi huwa hawana uzoefu wa kuongoza wizara au uongozi wa taasisi kubwa ya kitaifa kama wizara.
Uzoefu wao kama wabunge unaweza kulinganishwa na mfanyabiashara binafsi au mjasiriamali. Huwezi kumchukua mtu kama huyo ukampa umeneja wa kampuni kubwa na kutegemea afanye miujiza.
Isitoshe mawaziri wanapambana na changamoto nyingi za kiutendaji kwa mujibu wa sheria na katiba na changamoto za kisiasa kutoka kwa wabunge wa upinzani na hata wale wa chama chake mwenyewe.
Kutofautisha na mameneja wa kampuni, mawaziri wako pale kutumikia watu na makundi ya aina tofauti, wenye mahitaji tofauti na zaidi ya yote kutekeleza maagizo ya Waziri Mkuu na Rais wa nchi.
Ni pale rais na baraza lake la mawaziri wanapoendesha Serikali kama mameneja wa kampuni ndipo nchi inapoingia katika matatizo. Mtiririko wa kiutawala hupotea, uwajibikaji hutoweka na ombwe la uongozi huibuka na nchi kupoteza mwelekeo.
Majukumu matano muhimu ya waziri wa Serikali
Waziri yeyote wa Serikali yoyote popote pale duniani anakabiliwa na majukumu matano muhimu. Kwanza, majukumu bungeni ambayo ni uwezo wa kujibu maswali kwa hoja zenye mashiko, kuelezea mambo mbalimbali, kuleta miswada bungeni na kuitetea.
Utawala na sera. Ingawa mawaziri si watendaji wakuu wa wizara, lakini wana jukumu la kuongoza wizara zao, kupitisha maamuzi yote muhimu, kutoa matamko ya Serikali, kuweka malengo, mipango na mikakati ya wizara na kuongoza watendaji wa wizara kwa vitendo.
Mtetezi wa wizara yake. Waziri anapaswa kuwa mtetezi mkuu wa wizara hivyo anapaswa kuwa ujuzi wa uraghibishi (advocacy) na stadi za majadiliano (negotiation skills) kujenga hoja kutetea wizara yake ili bajeti yake ipite katika kamati na hatimaye bungeni.
Uwajibikaji wa pamoja. Mawaziri hufanya kazi kwa uwajibikaji wa pamoja kama wajumbe wa baraza la mawaziri. Kwa hiyo waziri ni wakili wa kuitetea Serikali nzima katika kamati na bungeni.
Mtetezi wa wananchi – Waziri mzuri ni yule anayefanya kazi zake kama wakili au mtetezi wa wananchi wote hasa wanyonge na wasio na uwezo kwa sababu Serikali ni ya wananchi.
Hivyo waziri anapaswa awe na kawaida ya kuelemisha umma kuhusu kazi za wizara yake kupitia hotuba na mikutano ya hadhara au vyombo vya habari.
Hivi ndiyo vigezo vya kuwapimia mawaziri walioteuliwa kuunda baraza la mawaziri la Serikali ya Awamu ya Tano yenye kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu”. Kama watayashika haya, inatosha kuwa kama semina elekezi kwao.

No comments :

Post a Comment