Rais Dk. John Magufuli, amewateua kuwa wabunge, Prof. Possi Abdallah, Balozi Dk. Augustino Mahiga na Prof. Makame Mbarawa na kisha kuwateua kuwa mawaziri na naibu waziri.
Rais Dk. Magufuli amewateua kuwa wabunge kupitia viti 10 vya rais ambavyo anaweza kumteua mtu yeyote anayeona anafaa kuwa mbunge.
Kwa uteuzi huo sasa Rais amebakiwa na nafasi sita za kuteua wabunge, baada ya hivi karibuni kumteua, Dk. Tulia Ackson kuwa mbunge kabla ya kuchaguliwa kuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
WALIOWANIA URAIS NAO WAMO
Kati ya walioteuliwa katika Baraza jipya la Mawaziri la Rais Dk. John Magufuli, wapo wanne ambao walijitokeza katika kinyang’anyiro cha kuomba ridhaa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea urais uchaguzi mkuu uliopita.
Hao ni Dk. Hamisi Kigwangalla, Mwigulu Nchemba, January Makamba, Prof. Sospiter Muhongo na Balozi Dk. Agustino Mahiga, ambao hata hivyo katika kinyang’anyiro hicho walishindwa na Dk. Magufuli aliyesimamishwa na CCM kugombea urais.
KUHAMIA DODOMA
Kuhusu lini serikali itahamia mkoani Dodoma, Dk. Magufuli alisema atatakeleza kama ilivyo kwenye Ilani ya CCM ambayo imeeleza kuwa serikali ya awamu ya tano ihatakikisha ofisi za serikali zinahamia mkoani Dodoma ambako ndiko yaliko makao makuu ya nchi.ATINGA NA MAJINA MFUKONI
Rais Dk. Magufuli aliingia katika ukumbi kwa ajili ya kuzungumza na waandishi wa habari huku akiwa ameambatana na Makamu wa Rais, Samia Hassan Suluhu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.
Baada ya kuingia aliwasalimia waandishi na kukaa kwenye kiti chake, huku akimtaka Balozi Sefue kusogea katika meza kuu na kukaa pamoja nao, tofauti na ilivyozoeleka kiongozi huyo na wengine hukaa kushoto kwa Rais kunapokuwa na hafla za kuapisha au kutangaza Baraza la Mawaziri kama jana.
Baada ya kusalimiana na waandishi alizungumzia udogo wa baraza lake la mawaziri, fedha alizookoa na kwanini alichelewa kutangaza.
Hata hivyo, kinyume na ilivyozoeleka, ulipofika wakati wa kutangaza baraza lake, alichomoa karatasi iliyokunjwa kutoka kwenye mfuko wa koti na kuanza kutaja wizara na majina ya aliowateuwa.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment