Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Dk. Philip Mpango.
KIMENUKA tena! Wakati Rais John Pombe Magufuli ‘JPM’ akiendelea kusimamia zoezi la kutumbua majipu katika sekta na idara za umma kote nchini, imebainika kuwa baadhi ya vigogo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wamewamilikisha watoto wao wenye umri wa miaka mitatu hadi saba, majumba yenye thamani ya mabilioni ya shilingi, Uwazi linaripoti.
TUJIUNGE NA CHANZO
Chanzo makini kilicho ndani ya TRA kimeliambia gazeti hili kuwa vigogo wengi wa mamlaka hiyo, walio makao makuu jijini Dar es Salaam na mikoani, wamekuwa wakiwaandikisha watoto wao kuwa wamiliki halali wa majumba na vitega uchumi vyenye thamani ya mabilioni ya shilingi vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini.
Mfano wa majumba wanayomiliki.
“Wanafanya hivyo ili kukwepa mkono wa sheria kama wataambiwa kutaja mali walizonazo. Kwa hiyo unakuta jengo kama lile la… (anatajwa kigogo wa TRA anayemiliki jengo la ghorofa sita, lililopo Masaki jijini Dar) hati yake imeandikwa kumilikiwa na mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka saba.
“Serikali isikubali kudanganywa kirahisi namna hii. Hawa wamiliki wa majengo ya watumishi wa TRA watafutwe, kama mtoto wa miaka saba anaweza kumiliki jengo la mabilioni kama lile, aeleze alizipata wapi fedha hizo katika umri mdogo kama huo huku bado anasoma. Huku ni kuingizana chaka, yaani wanaiba mpaka wenyewe wanajihisi vibaya.”
WATOTO WAMILIKI PIA MAKAMPUNI
Licha ya watoto hao wengine wa miaka mitatu, minne hadi saba kumiliki majengo na vitega uchumi vingine, imedaiwa pia watoto hao wa vigogo, ni wamiliki wa kampuni mbalimbali za baba zao zilizosajiliwa na ambazo nyingi zinafanya biashara na serikali kwa njia ya udanganyifu.
“Kitu ambacho watu wa serikali wanapaswa kujua ni kwamba, hawa vigogo wana kampuni nyingi wanazomiliki, zingine zinafanya kazi za Clearing and Forwarding (kutoa na kuingiza mizigo nchini).
“Hizi kampuni zinafanya biashara na serikali na mara nyingi ndizo zinazohusika kufanya udanganyifu unaosaidia ukwepaji wa kodi,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:
“Kwa kuwa hawa baadhi ya vigogo wa TRA wanashirikiana na vigogo wa idara nyingine, kampuni za watoto wao zinafanya biashara katika sehemu hizo pia. Hapa ndipo ile sheria ya manunuzi ya serikali inapotumika kutoza ada kubwa ya huduma ambazo zipo chini ya kiwango.”WAKE, NDUGU NAO WAMO
Mbali na watoto hao wa vigogo, taarifa zinaonesha kuwa hata wake wa wafanyakazi hao nao ni wamiliki halali wa majengo yao ya kifahari ambayo watumishi hao wamejenga katika maeneo mbalimbali, yakiwemo mahoteli katika mbuga za wanyama, katika fukwe na sehemu nyingine zenye hadhi. Pia wake hao, mitaani wanaonekana wakiendesha magari ya kifahari.
“Wake zao wanatanua na magari ya kifahari, ya kisasa, kumbe ni pesa ya serikali. Lakini ukiacha wake zao, wako pia ndugu wa karibu wa watumishi wenyewe, kama kaka na dada zao, ambao wameandikishwa kama wamiliki, lakini wote tunajua kuwa hiyo ni ‘bosheni’ tu, wenye mali wenyewe wanajulikana,” kilisema chanzo hicho.
WANATUMIA KIGEZO CHA SHERIA
Inadaiwa kuwa, baadhi ya vigogo hao wanajua endapo serikali itawatokea kwenye majumba hayo na kukuta majina ya wamiliki si yao, ni vigumu kwa wao kufilisiwa kutokana na sheria za nchi ambapo ushahidi usio na shaka unatakiwa ili kumtia mtu hatiani.BOSI TRA ATANGAZA KIAMA
Wakati hali ikiwa hivyo, Desemba 2, mwaka huu, Mkurugenzi wa Mambo ya Ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Stella Cosmas, alitoa waraka maalum kwa wafanyakazi wote kutakiwa kuwasilisha tamko la mali na madeni waliyonayo kabla ya leo (Desemba 15, mwaka huu).
Katika waraka huo, mkurugenzi huyo alionya kuwa mtumishi yeyote atakayekiuka, ikiwa ni pamoja na kuwasilisha maelezo ya uongo, atachukuliwa hatua kali za kinidhamu kama zilivyoainishwa katika kanuni za utumishi za serikali na TRA.
WAFANYAKAZI MATUMBO MOTO
Kufuatia amri hiyo na uwezekano mkubwa wa kufilisiwa mali zao, inadaiwa kuwa, baadhi ya wafanyakazi wa mamlaka hiyo hivi sasa ‘matumbo yanawauma’ wakiwa hawajui nini kitatokea baada ya kuwasilisha mali wanazomiliki ambazo nyingi ni za mabilioni ya shilingi.
“Yaani ninakuambia hivi sasa hapa ofisini kunawaka moto, tena nasikia hadi huko mikoani nako usiseme, kila mtu hajui hatima yake ni nini kwa sababu karibu kila ofisa ana zaidi ya nyumba tatu au nne anazomiliki. Sasa ukichanganya na ukweli kwamba thamani ya nyumba hizo hazifanani na vipato, hali inatisha.
“Hatujui nini kitatokea, kila mmoja anamwomba Mungu wake kwa imani yake, lakini ukweli ni kwamba maofisa wa TRA wana ukwasi wa kutisha na majengo ya thamani pengine kuliko idara zingine za serikali,” kilisema chanzo hicho.
Gazeti hili lilijaribu mara kadhaa kuwasiliana na Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Dk. Philip Mpango (pichani) ili kupata maelezo yake juu ya sakata hilo, lakini mara zote simu yake haikupatikana hewani.
GPL
No comments :
Post a Comment