Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu kesi aliyofungua kutaka kusitisha ubomoaji wa nyumba za wakazi Kinondoni. Picha na Omar Fungo
Dar es Salaam. Dar es Salaam. Sakata la bomoabomoa kwa wakazi wa mabondeni limechukua sura mpya baada ya mbunge wa Kinondoni (CUF), Maulid Mtulia kufungua kesi katika Mahakama ya Ardhi kupinga ubomoaji wa nyumba bila kutoa njia mbadala za makazi.
Kazi ya ubomoaji wa nyumba zilizojengwa mabondeni, maeneo ya wazi, kwenye kingo za mito na fukweni, ilisitishwa kwa muda hadi Januari 5, ukiwa ni mpango wa kuwapa muda wakazi kuhamisha vifaa vyao na kubomoa wenyewe nyumba zao, lakini sasa itakutana na kikwazo kipya.
Jana, mbunge huyo wa Kinondoni aliwaambia wanahabari kuwa shauri hilo linatarajiwa kusikilizwa leo na kitengo hicho cha ardhi cha Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam kuanzia saa 4:00 asubuhi, na itasikilizwa na Jaji wa Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi, Panterine Kente.
Alisema anachopinga ni kitendo cha Serikali kuwavunjia nyumba wakazi hao badala ya kuwahamishia eneo lenye usalama.
“Serikali ingekuwa inawahamisha mimi sina tatizo kabisa. Lakini unawavunjia makazi yao halafu haujui wataishi wapi na kuwaacha wanalala juu ya kifusi. Serikali ilitakiwa iwahamishie kwenye viwanja vilivyopimwa,” alisema Mtulia.
Mtulia alisema kesi hiyo iliyosajiliwa Desemba 28, 2015 itasimamiwa na wakili Abubakar Salim na kuwataka wakazi wa Kinondoni kujitokeza kuifuatilia.
Mratibu wa wenyeviti wa mitaa 18 inayoguswa na bomoabomoa hiyo, Godwin Cathberth alisema Serikali ingesitisha kuvunja nyumba hizo ili wakae chini na kuzungumza.
Alisema viongozi wa mitaa hawakupata taarifa rasmi za kuhamishwa kama ambavyo Serikali hufanya mawasiliano yake.
“Wanasema sisi tuhame ghafla tu wakati Serikali imejenga miundombinu ya gharama kubwa, kama kituo cha mabasi yaendayo kasi na moja ya majengo ya hospitali ya (Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili) Moi. Inapenda watumishi wake au wagonjwa wafe na mafuriko?” alisema Cathberth.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba alisema hadi jana walikuwa hawajapokea zuio lolote la mahakama, hivyo operesheni hiyo itaendelea.
kama ilivyotangazwa awali.
Alisema shauri kama hilo lilishapelekwa mahakamani miaka ya nyuma na mahakama ikaamua wahame na tayari kwa wiki kadhaa zilizopita watu wengi wameondoka wenyewe kama inavyotakiwa.
Alisema katika utekelezaji wa sheria ya usimamizi wa mazingira, mipango miji na misitu, Serikali haitamuonea mtu na uhakiki ulishafanywa kabla ya uamuzi wa kuwaondoa.
“Watu wote wanaoishi katika maeneo yasiyostahili wana taarifa ya muda mrefu kuwa wanatakiwa kuhama, si tu kwa sababu ya kukidhi sheria, bali kwa ajili ya kuokoa maisha yao pale mvua zinaponyesha,” alisema.
“Mbunge kama anawapenda watu wake, atawasaidia kuhama siyo kubaki katika maeneo ambayo uhai wao upo hatarini,” alisema Makamba.
No comments :
Post a Comment