Chama cha Wananchi CUF Wilaya ya Tanga kimetangaza rasmi msimamo wake wa kutomtambua Meya wa Jiji la Tanga, Mhina Mustaph maarufu kwa jina la Seleboss na kwamba hakitaruhusu madiwani wa Chama hicho na wa umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA kwa ujumla kushiriki vikao atakavyoviitisha.
Aidha umoja huo wa katiba ya wananchi UKAWA umepanga kuwasilisha malalamiko yao kwa Waziri ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kumtaka kumuajibisha Mkurugenzi wa halmashauri ya Jiji la Tanga, Daud Mayeji kwa kuvuruga uchaguzi wa umeya na kuitia hasara serikali.
Akizungumza na NIPASHE, Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Tanga, Rashid Jumbe alieleza kuwa msimamo wa vyama vinavyounda umoja wa katiba ya wananchi UKAWA wa kutomtambua Seleboss upo palepale mpaka uchaguzi
huo utakaporudiwa ama kutangazwa mshindi halali wa nafasi hiyo.
Jumbe ambaye alikuwa akizungumzia kuvurugika kwa uchaguzi wa meya wa Jiji la Tanga uliofanyika Desemba 19 mwaka jana, alisema serikali kupitia Tamisemi ni vema ikatoa tamko la nini kifanyike kuhusiana na matokeo hayo ya udanganyifu ambayo yalimpa ushindi mgombea umeya wa
Chama cha Mapinduzi CCM.
“Tunamtaka Waziri mwenye dhamana kumuajibisha Mkurugenzi wa Jiji la Tanga kwa kufanya udanganyifu wa kumtangaza mgombea wa CCM huku akijua siyo mshindi halali wa uchaguzi huo…..vinginevyo hakutakuwa na
vikao vya baraza mpaka kieleweke” alisema Jumbe.
Alieleza kuwa wanachohitaji ni haki kwa kuwa madiwani wa umoja wa katiba ya wananchi hawamtambui Mhina kama meya kwani ushindi wake umegubikwa na hila na dhuruma na kwamba kwa matokeo hayo halmashauri haitafanya vikao vyovyote kutokana na CCM kutotimia akidi ya
wajumbe.
Alieleza kuwa baraza la madiwani la halmashauri hiyo CCM ina madiwani 17 ambao ni wajumbe halali na umoja wa katiba ya wananchi UKAWA inamadiwani 20 na kwamba kwa matokeo hayo CCM hawawezi kuendesha baraza na kuunda kamati.
Alisema kutokana na hali hiyo wanaiomba serikali kuhakikisha uchaguzi wa Umeya Jiji la Tanga unarudiwa ili kuwatendea haki wananchi wanaosubiri miradi mbalimbali ianze kutekelezwa kutokana na kuwepo kwa vikao vya mabaraza ya madiwani na uundwaji wa kamati ambazo mpaka sasa
hakuna kamati hata moja iliyokwisha undwa.
SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment