Mwishoni mwa mwaka jana, serikali ilitoa mwongozi wa elimu ya msingi (shule ya msingi mpaka kidato cha nne) kuwa wazazi watatakiwa kununua sare za shule na michezo, madaftari, kalamu, chakula kwa wanafunzi wa kutwa na kugharamia matibabu ya watoto wao.
Ilisema, watatakiwa pia kulipia nauli ya kwenda shule na kurudi kwa wanafunzi wa kutwa na wa bweni wakati wa likizo, kununua magodoro, shuka, vifaa vya usafi binafsi kwa wanafunzi wanaosoma shule za bweni na wanaoishi katika hosteli zinazotumiwa na serikali.
Hali shuleni, ruvuma
Mkoani Ruvuma, baadhi ya wanafunzi wanaosoma katika shule ya Sekondari ya Kutwa ya Nandembo iliyopo wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma, walifukuzwa kwa madai ya kushindwa kuwasilisha michango.Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wanafunzi hao wanaoishi hosteli iliyojengwa eneo la shuleni hapo kutokana na kuishi mbali na shule, walisema walifukuzwa kutokana na wazazi wao kushindwa kuchangia michango ya chakula, kusagia nafaka na michango ya kulipa mpishi.
Kwa mujibu wa wanafunzi hao, kila mtoto ambaye amechaguliwa kusoma katika shule hiyo akiwa anatokea vijiji jirani, anatakiwa kuchangia debe nne za mahindi, moja la mpunga, kilo 30 za maharage, kilo mbili za chumvi, lita mbili za mafuta, Sh.10,000 kwa ajili ya kusagia mahindi na Sh. 5,000 za kumlipa mpishi wa shule hiyo.
Wanafunzi Waziri Seifu, Kadiri Ally na Fadhili Rajabu kutoka katika Kijiji cha Muhuwesi wanaosoma kidato cha pili katika shule hiyo walisema kuwa wanarudi nyumbani wakiwa hawana matumaini ya kurejea tena shuleni kuendelea na masomo yao kwa kuwa wazazi wao hawatawapatia michango hiyo hasa kwa kipindi hiki ambacho makwao wanakabiliwa na upungufu wa chakula.
Akizungumzia tukio hilo Mkuu wa shule hiyo, Mary Ndunguru, alikiri kuwarudisha baadhi ya wanafunzi hao ili wakachukue chakula majumbani kwao kwa madai kuwa hali hiyo imetokana na shule yake kutokuwa na uwezo wa kuwahudumia watoto hao kwa kuwapatia chakula siku za masomo yao.
Afisa Elimu wa Shule za Sekondari Wilayani Tunduru, Ally Mtamila, alisema ofisi yake kwa kushirikiana na ya mkurugenzi mtendaji wa halamshauri ya wilaya hiyo, walikwishapeleka taarifa za maelekezo kwa madiwani, waratibu elimu kata, yaliyowataka kufanya mikutano ya kufafanua maelekezo ya serikali juu ya utoaji wa elimu bure.
Mtamila aliendelea kufafanua kuwa kwa mujibu wa maelekezo hayo kutoka Tamisemi, fedha walizopokea kwa ajili ya utekelezaji wa elimu bure, katika maelekezo ya fedha hizo za Rais Magufuli, hakuna maelekezo yanayowataka kuwahudumia wanafunzi wa kutwa chakula.
322 MBOZI WAKOSA MADARASA
Jumla ya wanafunzi 322 wa shule nne za sekondari waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu katika Wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya, hawataanza masomo na wenzao kufuatia shule zao kukosa vyumba vya madarasa.
Ofisa Elimu Sekondari Wilaya yai Mbozi, Honsana Nshullo, alisema majina ya wanafunzi hao yamefichwa, mpaka pale wananchi watakapomaliza ujenzi wa vyumba vya madarasa ndipo yatakapotolewa, ili waanze masomo na kuwataka madiwani katika maeneo husika kuharakisha ukamilishaji wa vyumba hivyo mapema ili wanafunzi hao waanze masomo haraka baada ya kufanya usaili wa pili.
Alizitaja shule hizo na idadi ya wanafunzi kuwa ni pamoja na Kilimampimbi wanafunzi 40 (chumba kimoja cha darasa kinahitajika), Nalyelye wanafunzi 88 (vyumba viwili vya madarasa), Mlowo wanafunzi 64 (vyumba viwili vya madarasa) na Insani wanafunzi 88 (vyumba viwili) na kwamba katika shule hii hakuna mwanafunzi hata mmoja aliyechukuliwa.
Aidha, Nshullo alisema pamoja na kwamba serikali imefuta ada na michango mingine kwa wanafunzi lakini wazazi watakuwa na wajibu wa kuhakikisha watoto wanapata chakula cha mchana na mahitaji mengine kama vile sare, daftari na kalamu.
Manispaa ya Dodoma
Uongozi wa Shule ya Sekondari Mbabala iliyopo Manispaa ya Dodoma, umedaiwa kutoza Sh. 500,000 kwa mwaka kwa kila mwanafunzi anayelala shuleni (boarding).
Akizungumza na Nipashe, Mkuu wa shule hiyo, Gaitan Mwatenga, alikiri shule kutoza fedha hizo na kudai shule hiyo si ya bweni bali ina hosteli kwa wazazi wanaotaka watoto wakae shuleni hulipa fedha hizo.
Alisema kiasi cha Sh. 250,000 hutozwa kwa kila mwanafunzi anayekaa hosteli kwa muhula na kwa mwaka mzazi anatakiwa kulipa Sh. 500,000.
“Mimi sina bweni hapa, nina hosteli na shule zenye hosteli kwa hapa Manispaa ya Dodoma ni Mbabala, Mpunguzi na Hombolo yaani huwa kuna nafasi kidogo za hosteli kwa yule anayetaka kuja kukaa anakuja lakini anatakiwa kutoa fedha hizo kwa ajili ya gharama ya chakula, wapishi, matroni, kuni na vitu vingine,”alisema mkuu huyo na kufafanua kuwa bodi ya shule ndiyo iliyopanga kiwango hicho ambacho ni sawa na mwanafunzi kutumia Sh.1,500 kwa siku.
Akifafanua suala hilo, Afisa Elimu mkoani hapa, Juma Kaponda, alikiri shule hiyo kutoza fedha hizo na kudai kuwa ni kwa ajili ya hosteli sio bweni.
Alisema kinachozungumzwa kwenye elimu bure ni kwa maana ya gharama za uendeshaji na si bure kwa maana ya gharama za mtoto.
Mwamko hafifu Simiyu
Katika Shule ya Sekondari Simiyu, iliyoko Kata ya Malambo, Halmashauri ya Mji wa Bariadi, hadi juzi hakukuwapo mwanafunzi yeyote ambaye alifika kwa ajili ya kujiandikisha kuanza kidato cha kwanza.
Mmmoja wa walimu wa shule hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake kwa madai kuwa si msemaji wa shule, alisema hakukuwa na mwanafunzi yeyote ambaye amerejesha fomu zilizochukuliwa kwa ajili ya kujiunga na masomo shuleni hapo.
“Shule hii inatakiwa kupokea wanafunzi 220 na ambao wamechukua fomu mpaka sasa ni zaidi ya 100, lakini hadi leo (juzi) hakuna hata mmoja ambaye amerejesha fomu kwani mimi ndiye napokea fomu hizo,” alisema.
Pia katika Shule ya Sekondari Kidinda, kata ya Bariadi, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Shija Mayunga, alisema wamepokea wanafunzi watatu tu ambao alisema walifika na fomu pamoja na mahitaji muhimu kwa ajili ya kuanza masomo.
“Mwitikio bado mdogo sana mpaka sasa tumepokea wanafunzi watatu tu na hapa hatuoni dalili za kupokea wanafunzi wengine lakini tuna matumaini hadi kufika mwishoni mwa wiki hii wanafunzi wanaweza kuongezeka,” alisema.
Mayunga alisema shule hiyo inatakiwa kupokea wanafunzi 253 na kuonyesha kushangazwa na wazazi kushindwa kuwapeleka wanafunzi shule wakati serikali imetangaza elimu bure kuanzia chekechea hadi kidato cha nne.
Katika Shule ya Sekondari Biashara, kata ya Sima, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mathias Joseph, alisema hadi juzi saa 6:40 mchana walikuwa wamepokea wanafunzi 29 kati ya 337 wanaotakiwa kuripoti shuleni hapo kuanza kidato cha kwanza.
Alisema mwitikio wa wazazi kupeleka wanafunzi shule ni mdogo ikilinganishwa na matarajio yao baada ya serikali kuondoa michango ikiwamo ada.
Mwongozo wa elimu Bure
Mwongozo wa elimu bure uliotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, elimu msingi bila malipo, serikali ilikuwa igharamikie utayarishaji na uendeshaji wa mitihani ya kitaifa, uthibiti ubora wa shule, ruzuku ya uendeshaji wa shule ikiwamo ulinzi, umeme, maji na ununuzi wa chaki na karatasi pamoja na vifaa vingine vya kufundishia na kujifunzia.
Serikali pia itagharamikia kununua vitabu, kemikali na vifaa vya maabara, samani yakiwamo madawati, vifaa vya michezo, matengenezo ya mashine na mitambo pamoja na kujenga na kukarabati miundombinu ya shule.
Majukumu ya wazazi
Kwa mujibu wa mwongozo huo, wazazi wanatakiwa kununua sare za shule na michezo, vifaa vya kujifunzia vikiwamo madaftari na kalamu, chakula kwa wanafunzi wa kutwa na kugharamia matibabu kwa watoto wao.
Imeandaliwa na Anceth Nyahore, Simiyu, Bosco Nyambege, Mbozi, Stevie Chindiye, Tunduru na Augusta Njoji, Dodoma
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment