Agizo hilo lililtolewa jana Ikulu jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, wakati wa semina iliyowahusiha watendaji hao wa wizara kabla ya kwenda kwenye ofisi zao kufuatia kuapishwa na Rais Jon Magufuli juzi.
Aidha, Sefue aliwaambia wateule hao kuwa hawapaswi kuwa na kigugumizi wakati wa kuchukua maamuzi dhidi ya watumishi wazembe.
“Haikubaliki kwa mtumishi aliyefanya makosa katika sehemu moja ya kazi, kuhamishiwa katika sehemu nyingine badala ya kuchukuliwa hatua palepale alipo," alisema na kueleza zaidi:
"Na wala serikali haitarajii kuona mnakua na kigugumizi katika kuchukua hatua dhidi ya watumishi watakaokuwa na makosa."
Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu kutoka wizara zote za serikali ya awamu ya tano walikutana jana katika ukumbi wa mikutano wa Ikulu kwa ajili ya kupata semina elekezi iliyoongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Sefue.
Balozi Sefue, alisema semina hiyo ni ya kikazi zaidi na kwamba lengo la serikali ni kuhakikisha Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu hao ambao waliapishwa juzi wanatekeleza wajibu wa kusimamia utendaji kazi wa serikali vizuri.
Balozi Sefue alielekeza kuwa kila Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu anapaswa kutambua kuwa nafasi yake ni ya maamuzi, hivyo serikali inatarajia kuona kuwa daima anafanya maamuzi kwa usahihi na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazomuongoza katika majukumu yake.
Aidha, Balozi Sefue alionya kuwa serikali ya awamu ya tano inawatarajia viongozi hao kuwa wasimamizi wazuri wa fedha za umma na kwamba haitarajii kuwepo kwa hati za ukaguzi wa mahesabu zenye kasoro.
Balozi Sefue aliongeza kuwa Makatibu Wakuu hao na Naibu Makatibu Wakuu ni mamlaka ya nidhamu katika wizara zao, hivyo wanapaswa kusimamia majukumu yao ipasavyo.
Katika kampeni za uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Rais Magufuli aliahidi kuwa akiingia Ikulu atakomesha utaratibu wa ovyo wa kuhamisha watumishi walioharibu kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Rais Magufuli ambaye kwa wakati huo alikuwa mgombea urais wa CCM, alisema kwenye serikali yake mtumishi atayeharibu sehemu moja atakuwa ameharibu maisha yake yote.
“Unakuta mtumishi ameharibu hapa Kibondo, anahamishiwa Moshi… kwenye serikali yangu mtu akiharibu hapa Kibondo basi ameharibu maisha yake yote, Tanzania inawasomi wengi wazalendo ambao wanaweza kulitumikia vyema taifa lao,” alisema Magufuli wakati huo.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment