Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amri Jeshi Mkuu, Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi wa Monduli, hawapo pichani .Picha kwa hisani ya mtandao.
Dar es Salaam. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetoa ufafanuzi kuhusu mavazi ya kijeshi ambayo Rais John Magufuli alivaa juzi wakati akienda Chuo cha Maofisa wa Jeshi cha Monduli (TMA) mkoani Arusha.
Dk Magufuli alivaa vazi hilo lenye mabaka ya rangi ya mchanganyiko ya kijani, kahawia nyeusi na nzito, lakini haikuwa na alama za cheo mabegani wala kifuani, jambo lililosababisha mjadala mkubwa hasa kwenye mitandao ya kijamii.
Kilichokuwa kikihojiwa zaidi ni sababu za kutoa alama hizo wakati akiwa kwenye taasisi ambayo utambuzi wa cheo hutegemea nishani hizo.
Msemaji wa JWTZ, Kanali Ngemela Lubinga alisema jana kuwa hakukuwa na tatizo lolote kwa Rais Magufuli kuvalia mavazi hayo bila alama za vyeo na wala kuyatumia wakati akihutubia wananchi.
Kanali Lubinga alisema Sheria ya Jeshi ya Mwaka 1966 (National Defence Act) inamhalalisha Rais aliyepo madarakani kuvalia mavazi hayo kwa kuwa ni Amiri Jeshi Mkuu.
Kuhusu magwanda hayo kutoonyesha vyeo, Lubinga alisema tofauti na wanajeshi wengine, sare za Amiri Jeshi Mkuu hazina vyeo wala alama yoyote mabegani.
Juzi, kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii watu walituma picha inayomuonyesha Rais Magufuli katika mavazi hayo sambamba na picha ya Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ambaye gwanda lake lilikuwa na nyota nne.
Pia, picha hizo ziliwaonyesha viongozi wa zamani, Mwalimu Julius Nyerere, Samora Machel wa Msumbiji na Kenneth Kaunda wa Zambia wakiwa wamevalia magwanda ya kijeshi, lakini ambayo hutumiwa kwenye shughuli za kawaida.
Picha nyingine zilimuonyesha Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Barack Obama (Marekani) na Paul Kagame wa Rwanda wakiwa kwenye magwanda hayo.
Kuhusu kuvalia mavazi hayo wakati akihutubia wananchi uraiani, Lubinga alisema alilazimika kuhutubia wakati akiwa njiani kuelekea chuo hicho cha kijeshi cha Monduli.
“Watanzania waelewe kwamba kitendo cha Rais kuvalia mavazi ya kijeshi si cha ajabu kwa sababu alikuwa kwenye shughuli za kijeshi na nafasi yake ya Amiri Jeshi Mkuu inampa haki hiyo,” alisema.
Alisema Rais alikuwa anakwenda kwenye majukumu ya kijeshi, lakini kutokana na watu kumtaka kwa kumfungia barabara, alilazimika kusimama na kuzungumza nao kukata kiu.
“Baada ya msafara wake kusimamishwa wakati akielekea Chuo cha Maofisa wa Jeshi, haikuwezekana kurudi ili abadilishe mavazi ndipo arudi kuzungumza nao, ikalazimika azungumze na wananchi wake akiwa katika mavazi hayo,” alisema Kanali Lubinga.
No comments :
Post a Comment