Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, January 3, 2016

Kauli ya RC Tanga kuhusu njaa ifanyiwe kazi

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mwantunu Mahiza.
Katika toleo la gazeti hili la jana, ukurasa wa 12 kulikuwa na habari iliyokuwa na kichwa kisemacho “wilaya tatu hatarini kukumbwa na njaa”. Wilaya hizo ni za mkoani Tanga ambazo ni Korogwe, Handeni na Kilindi.
Katika habari hiyo, mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mwantunu Mahiza anazungumzia tishio hilo la njaa akisema kukosekana kwa mvua za kutosha mwaka huu, kuna hatari ya kuufanya mkoa huo, maarufu kwa kilimo, kukumbwa na njaa.
Mwantunu mbali na kuwataka wananchi wa wilaya hiyo kutoingia tamaa ya kuuza vyakula vyao, pia aliwakemea wafanyabiashara kuwa wasitumie shida hiyo kupandisha bei za vyakula na hivyo kuwafanya wananchi waishi kwa shida.
Anasema hivi sasa tayari kuna dalili zote za wilaya hiyo kukumbwa na njaa na hivyo kunahitajika tahadhari kubwa.
Wilaya hizo tatu ni sehemu tu ya wilaya zilizo hatarini kukumbwa na njaa, hasa kutokana na ukweli kwamba kumekuwapo mabadiliko makubwa ya hali ya hewa, ambayo yamesababisha mvua kuchelewa au kutokuwa za kutosha, kitu ambacho ni hatari kwa kilimo.
Mkoa wa Dodoma ni kati ya sehemu ambazo zimeripotiwa kuwa kwenye tishio la njaa, wakati eneo kama Isimani ambalo lilikuwa linajulikana kwa uwezo wake wa kuzalisha mazao mengi, tayari liko kwenye hali mbaya ya chakula ambayo inatishia usalama wa wananchi.
Wakati mvua zilizonyesha hazikuwa za kutosha kwenye baadhi ya maeneo, bado kuna tishio la mvua za El Nino kwenye maeneo mengine, jambo ambalo linazidi kuweka tishio la njaa kutokana na tabia ya mvua hizo kuacha mazao yakiwa yameharibika, kama hakukufanyika jitihada za kutosha kukabiliana na hali hiyo.
Ni jambo jema kwamba Mahiza ameanza kuzungumzia tishio hilo mapema na kuwataka wananchi watekeleze jukumu lao la kutouza vyakula ovyo na kutogeuza tishio la baa la njaa kuwa mradi wa kulangua bei za vyakula.
Kilichobakia baada ya tamko hilo la Mahiza, ambaye pia aliahidi kuwasiliana na ofisi ya Waziri Mkuu kuomba msaada wa chakula, ni jitihada za Serikali kukabiliana na tishio hilo la njaa kwa wilaya hizo tatu, mkoa na Taifa kwa ujumla.
Pamoja na viongozi wapya wa Serikali, yaani mawaziri na naibu wao kuanza kazi kwa nguvu, hatujaona suala hili likizungumzwa kwa mapana kulingana na ukubwa wake. Na wakati mwingine inaonekana kama hakuna tishio la njaa kwa kuwa bado halizungumzwi kama ajenda maalumu ya kuhakikisha wananchi hawaathiriki na tatizo la njaa.
Akiwa Jimbo la Iramba Magharibi, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan aliahidi kuwa hakuna Mtanzania atakayekufa kwa njaa.
Alisema hayo wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu.
Hata hivyo, hatuoni juhudi za makusudi zikichukuliwa kukabiliana na hali hiyo, kiasi kwamba Mahiza analazimika kuita waandishi wa habari na kuwaeleza tatizo lilivyo kubwa.
Tunapenda kushauri kuwa Serikali, na hasa watu waliopewa jukumu la kukabiliana na majanga kama ya njaa, watajitokeza na kuueleza umma wamejipangaje ili kuwaondoa hofu wananchi walio kwenye maeneo yenye tishio la njaa.
Wananchi wanahitaji kujua Serikali yao imejipangaje na pia wao wafanye nini, ili kushirikiana na Serikali kuepusha uwezekano wa njaa kuathiri maisha yao.
Na hii itafanikiwa tu iwapo wahusika watajitokeza kama mkuu huyo wa mkoa wa Tanga alivyofanya na kuueleza umma tishio la njaa ni kubwa kiasi gani, nini kinafanyika kukabiliana nalo na hivi sasa kifanyike nini.
/Mwananchi.

No comments :

Post a Comment