Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombare Mwiru, amesema atampima na kuzungumzia utendaji wa Rais wa tano, John Magufuli atakapotimiza siku 100 Ikulu.
Dk. Magufuli leo ametimiza siku 59 tangu kuapishwa kushika madaraka hayo Novemba 5, mwaka jana na ameshafanya mambo makubwa yaliyompa sifa kem kem kitaifa na kimataifa.
Akizungumza na Nipashe jana, Kingunge ambaye mwishoni mwa mwaka jana alikihama chama alichokiasisi cha CCM na kukitumikia kwa zaidi ya miaka 60, alisema kwa kawaida watu hupimwa utendaji wao wa kazi zinapofika siku 100.
Hivyo alimtaka mwandishi avute subira hadi siku hizo zitakapofika.
Kingunge ambaye alikuwa na kadi namba 8 CCM kabla ya kujiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi kumpigia kampeni aliyekuwa mgombea wa Chadema kwenye Uchaguzi Mkuu, Edward Lowassa, alisema ni mapema mno kujadili utendaji wa serikali ya Magufuli.
“Jamani nadhani ni mapema mno, msiwe na haraka nitatoa maoni yangu kuhusu utendaji wake muda huo utakapofika. Kwa sasa mwacheni afanye kazi zake msimwingie ingilie," alisema Kingune ambaye amewahi kushika nyadhifa nzito nzito serikalini.Dk. Magufuli leo ametimiza siku 59 tangu kuapishwa kushika madaraka hayo Novemba 5, mwaka jana na ameshafanya mambo makubwa yaliyompa sifa kem kem kitaifa na kimataifa.
Akizungumza na Nipashe jana, Kingunge ambaye mwishoni mwa mwaka jana alikihama chama alichokiasisi cha CCM na kukitumikia kwa zaidi ya miaka 60, alisema kwa kawaida watu hupimwa utendaji wao wa kazi zinapofika siku 100.
Hivyo alimtaka mwandishi avute subira hadi siku hizo zitakapofika.
Kingunge ambaye alikuwa na kadi namba 8 CCM kabla ya kujiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi kumpigia kampeni aliyekuwa mgombea wa Chadema kwenye Uchaguzi Mkuu, Edward Lowassa, alisema ni mapema mno kujadili utendaji wa serikali ya Magufuli.
"Kwani nyinyi mna haraka gani mpaka mnataka nitoe maoni yangu leo?" Aliuliza. "Bado ni mapema sana kumpima.”
Kingunge alisisitiza kuwa ni vyema Magufuli akaachwa afanye kazi zake kwa sasa.
Oktoba 4, mwaka jana, Kingunge alitangaza rasmi kujiengua ndani ya chama hicho, akisema alifanya hivyo kutokana na kile alichoamini kuwa CCM haifanyi yale yaliyoasisiwa na kujengewa misingi bora na waasisi wake.
Wakati akitangaza uamuzi huo, Kingunge alisema hakusudii kujiunga na chama chochote cha siasa nchini bali atakuwa mtanzania huru, lakini muda si mrefu akaungana na Ukawa kumnadi Lowassa.
Mwanasiasa huyo ambaye sehemu kubwa ya maisha yake alikuwa CCM, alisema wananchi wanataka mabadiliko na wasipoyaona ndani ya chama hicho watayatafuta nje ya chama, ikiwa ni nukuu ya nasaha maarufu ya Baba wa Taifa, hayati Julius Nyerere aliyowahi kuitoa enzi za uhai wake.
Mara baada ya kuapishwa Novemba 5, Rais Magufuli alianza na kasi ya kubana matumizi ili kuhakikisha serikali inapata fedha za kuendesha miradi mbalimbali kama elimu, afya na ujenzi wa miundombinu.
Miongoni mwa mambo ambayo yamempa sifa Rais Magufuli ni pamoja na kufuta shamra shamra za sherehe za Uhuru zilizokuwa zifanyike tarehe 9, Desemba na kuamuru Sh. bilioni nne zilizokuwa zitumike kwenye sherehe hizo kupanua barabara ya Morocco-Mwenge, Dar es alaam.
Pia aliagiza zaidi ya Sh. milioni 200 zilizokuwa zitumike kwa ajili ya vinjwaji na viburudisho kwenye hafla ya kuzindua Bunge zitumike kununulia vitanda katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), ambapo vitanda 300 vilipatikana kutokana na fedha hizo.
Rais Magufuli pia aalianza zoezi la 'utumbuaji majipu' katika sekta ya fedha, mkazo ukiwa zaidi katika kuzuia ukwepaji kodi katika Mamlaka ya Mapato (TRA) na Mamlaka ya Bandari (TPA) zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango na Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Dk. Magufuli aliweka rekodi ya aina yake kwa serikali kumudu kukusanya mapato yaliyofikia Sh. trilioni 1.3 ndani ya mwezi mmoja tangu aingie madarakani.
Tayari Magufuli amewasimamisha kazi vigogo kadhaa waandamizi serikalini kwa kushindwa kwenda na kasi anayoitaka akiwemo Kamishna Mkuu wa Mamalaka ya Mapato Nchini (TRA), Rished Bade ambaye bado anachunguzwa pamoja na vigogo wengine saba ambao walikamatwa na polisi na kufikishwa mahakamani.
Kadhia iliyosababishwa kusimamishwa kazi kwa vigogo hao akiwemo Kaimu Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa, Tiagi Masamaki ilitokana na kutolewa kwa makontena 329 katika bandari kavu bila kulipiwa ushuru.
Magufuli pia alivunja Bodi ya Mamlaka ya Bandari (TPA) na kutengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mhandisi Profesa Joseph Msambichaka na kumsimamisha kazi Katibu Mkuu wa iliyokuwa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi, Shaaban Mwinjaka.
Rais Magufuli pia alitengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hoseah, kwa kile kilichoelezwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue kwamba Rais hajaridhishwa na utendaji wa taasisi hiyo.
Serikali ya Dk. Magufuli pia ilimsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO), Benhadard Tito ili kupisha uchunguzi wa kutokana na ukiukwaji mkubwa wa taratibu za manunuzi, uliobainika katika mchakato wa utoaji wa zabuni ya ujenzi wa Reli ya Kati.
Aidha, tangu aingie madarakani mwaka jana, Rais Magufuli ameongoza kwa staili tofauti, ikiwa ni pamoja na kujichimbia Ikulu ya Magogoni akifanya kazi bila kusafiri nje ya nchi wala mikoani.
Katika hali inayoonyesha utendaji wa Rais Magufuli ni wa ufuatiliaji wa karibu, juzi alifuta utaratibu wa protokali uliokuwa umetangazwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue na kuagiza itumike njia yake, wakati wa hafla ya kuapisha Makatibu Wakuu na Makatibu Wasaidizi wapya wa wizara mbalimbali aliowateua hivi karibuni.
Makatibu wakuu na manaibu wao walifika Ikulu kwa ajili ya shughuli ya kuapishwa kushika nafasi zao na baadaye kusaini kiapo cha uadilifu kilichoongozwa na Naibu Kamishna wa Maadili, Waziri Kipacha.
Mara baada ya Kamishna huyo kusoma kiapo hicho kwa niaba ya makatibu wakuu na manaibu hao, Katibu Mkuu Kiongozi aliwataka makatibu wakuu na manaibu hao kila mmoja asaini katika hati aliyopewa.
Utaratibu huo uliotangazwa na Balozi Sefue ulionekana kutomridhisha Rais Magufuli ambaye katika hali ambayo haikutarajiwa, aliinuka kutoka sehemu aliyokuwa amekaa na kutoa utaratibu tofauti.
“Hapana huwezi kula kiapo kwa niaba ya mtu mwingine wakati wenyewe wote wapo hapa, kila mmoja aape kwa mdomo wake mwenyewe na kusaini," alisema Rais Magufuli na kutoa angalizo:
"Kama kuna mmoja wao hajakubalina na kifungu kwenye hati hii tutajuaje?
“Kama yupo Katibu Mkuu au Naibu Katibu Mkuu anayeona kuwa hataweza kutekeleza mojawapo ya vifungu vilichopo katika hati hiyo ya maadili akae pembeni atuache wengine tuendelee.”
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment