Misaada inayotolewa na wafadhili kupitia vituo vya kulelea watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi nchini yenye thamani ya mabilioni ya shilingi imekuwa ikitafunwa na wajanja kabla ya kuwafikia walengwa, imedaiwa.
Kwa mujibu wa barua ya Kituo cha New Hope Family cha Kigamboni jijini Dar es Salaam kwenda kwa Rais John Magufuli, mabilioni ya fedha katika fedha za misaada hutafunwa na watumishi wa serikali, wadau, kampuni, taasisi pamoja na mashirika.
Hali hiyo, imedai barua hiyo, imeacha watoto wanaolelewa katika kituo hicho wakiendelea kutaabika.
Mbali na kubainisha uwapo wa ufisadi katika fedha za misaada, kituo hicho pia kiliomba kukabibidhiwa eneo lake lenye ukubwa wa ekari nne ili kiliendeleze na kumudu kutoa huduma kwa kundi hilo ndani ya jamii.Mwenyekiti wa kituo hicho, Omari Kombe, katika barua hiyo, alisema kituo hicho kinakabiliwa na changamoto mablimbali lakini kubwa ni ya kutofika kwa misaada mbalimbali ya wahisani.
Aidha, alisema kismingi serikali imekitelekeza kituo hicho tangu mwaka 2012 licha ya changamoto za ukosefu wa fedha, malazi, chakula na mahitaji muhimu kwa watoto hao.
Alisema kituo hicho kilianzishwa 2009 kwa ubia na serikali, lakini baadaye ikawatelekeza. Kombe pia alisema watoto wengi wanaoishi katika mazingira hatarishi watashindwa kujikwamua katika mnyororo wa umaskini kutokana na jamii kutowasaidia.
Badala yake, alisema, jamii imekuwa mstari wa mbele kuwafanyisha biashara ndogo ndogo kama kuuza maji, mahindi, karanga, mihogo na barafu.
Kituo hicho kilianzishwa kikiwa na watoto 20 lakini kwa sasa kina jumla ya wahitaji 36, kati yao 24 ni wanafunzi wa shule za msingi, na wanaishi katika nyumba waliyopangishiwa kupitia ufadhili wa wadau.
Wakati huo huo, Kituo cha New Hope Family cha Kigamboni jijini Dar es Salaam kimeishauri serikali kuteua vituo vinavyojihusisha na malezi hayo kuunda kikosi kazi maalumu cha kudhibiti tatizo la watoto kuzurura ovyo mitaani. Kikosi kazi hicho kitafanya kazi kwa kushirikiana na Jeshi la polisi, Mahakama, Wizara ya Elimu, wizara ya Afya, Wizara ya Mambo ya Ndani na ya Ujenzi, kilisema.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment