Ahmed Rajab
Toleo la 441
20 Jan 2016
Viroja vilivyoshuhudiwa Zanzibar wiki iliyopita vinatufanya tusichoke kuonya na kuwahimiza wenye nguvu za kulazimisha mambo Visiwani humo wachukuwe hatua kwa haraka kabla ya nchi kutumbukia katika nakama.
Ninayasema haya kwa sababu siamini kuwa Rais John Magufuli na serikali yake ya Muungano hawana ubavu katika siasa za Zanzibar. Wala siamini kwamba chama chake hakina uwezo wa kuwadhibiti viongozi wake wa Visiwani ambao kwa matamshi na vitendo vyao wanahatarisha amani si ya Zanzibar peke yake bali ya Tanzania nzima.
Hivyo viroja ninavyovitaja ni pamoja na yale mabango yaliyokuwa na maneno ya kibaguzi na yaliyokuwa yamebebwa na wakereketwa wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wakati wa kilele cha matembezi yao ya kuadhimisha Mapinduzi ya 1964.
Moja ya mabango hayo lilisema hivi: “Machotara Hizbu. Zanzibar ni ya Waafrika.” Tafsiri ya hayo ni kwamba watu waliochanganya damu ni Mahizbu, yaani wafuasi wa chama cha Hizbul Watan (Nationalist Party), kilichopinduliwa Januari 1964, kwa hivyo hawatakiwi Zanzibar kwani Zanzibar ni ya Waafrika. Bango linapowataja “Waafrika” lina maana ya watu weusi.
Maneno hayo yanatisha na kuhuzunisha. Yanatisha kwa sababu yanaashiria shari na yanahuzunisha kwa sababu si maneno unayoyaratiji kuyasikia katika mwaka 2016, na hasa katika nchi inayojigamba kuwa ati haina ukabila.
Kichekesho ni kwamba maneno hayo yalichomoza katika sherehe za kuadhimisha Mapinduzi ambayo moja ya malengo yake rasmi ni kuuondoka ukabila na ubaguzi wa kila aina.
Lazima tuwe wakweli tunavyoizungumzia kashfa hii. Ukweli ni kwamba vijana waliobeba mabango hayo walikuwa na ujasiri wa kuzianika chuki zao za kikabila na ujinga wao mbele ya ulimwengu kwa sababu wanaamini kwa dhati ya kuwa hizo ndizo fikra za viongozi wao.
Wamekwishawasikia baadhi ya viongozi wao, wa Zanzibar na hata wa Bara, wakiendesha siasa za kikabila na kupalilia chuki wakiwa kwenye majukwaa hasa katika kipindi kilichokaribia Uchaguzi Mkuu wa 2015. Kanda za video za hotuba hizo bado zinasambazwa.
Aidha, kwa muda sasa wamekuwa wakisoma matamshi ya kibaguzi na yenye kupalilia chuki za kikabila kwenye lile bango lililo mbele ya maskani maarufu ya CCM ya Kisonge, Michenzani, Unguja.
Katika nchi zenye ustaarabu wa kutovumilia ubaguzi wa aina hiyo, polisi ingelikuwa imekwishawachukulia hatua wanasiasa wenye kuchochea chuki za kikabila pamoja na wakereketwa wenye kuandika maandishi ya uchochezi. Sio Zanzibar. Huko daima ni wapinzani wenye kushukiwa kufanya makosa. Ni wao tu wenye kukamatwa pamoja na mashekhe wao.
Wale wafanyao kweli vitendo vya jinai za kisiasa huwa hawagusiki kwa sababu ni wa chama fulani na polisi hawawezi kuwaingilia.
Hizo ni miongoni mwa sababu zilizowapa nguvu wakereketwa wa UVCCM wajitokeze hadharani na ujinga wao. Hao vijana wasingelithubutu kujiaibisha kama walivyojiaibisha lau hizo zisingelikuwa fikra za wahafidhina wanaowaongoza huko Zanzibar. Kuna fununu kwamba vijana hao walitiwa mori wafanye waliyoyafanya na wahafidhina fulani ambao ndio wenye kushika hatamu ndani ya chama chao.
Ndiyo maana Makamu Mwenyekiti wa CCM Dk Ali Mohamed Shein na Makamu Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan wasiweze kuwakemea au kuulani ubaguzi wa kikabila katika hotuba zao. Badala yake Shein aliwapungia mkono vijana hao walipokuwa wanapita mbele yake. Kama huko si kuwa pamoja nao, na kukubaliana na hisia zao, basi ni nini?
CCM-Taifa baadaye ilifanya uungwana wa kuomba radhi baada ya kuwaona Watanzania wameshtushwa na hisia hizo za kibaguzi. Lakini kuomba radhi tu hakutoshi. Lazima waliohusika na uovu huo wachukuliwe hatua, tena kwa haraka. La si hivyo, watakuja kujuta wengi.
Inafaa tujikumbushe kwamba yale mauaji ya kimbari yaliyotokea Ujerumani (1941-1945) na katika maeneo yaliyokuwa yakitawaliwa na Ujerumani yaalianza vivi hivi kwa matamshi ya kibaguzi ya Adolf Hitler. Kwa mtizamo wake Hitler, yeyote yule aliyekuwa si mzungu safi basi mtu huyo hakustahiki sifa ya ubinadamu.
Chuki zake kubwa zilikuwa dhidi ya Wayahudi. Kila aliloliona kuwa ni ovu aliwatupia Wayahudi. Wao, kwa mfano, ndio waliosababisha utawala wa Milki ya Ujerumani ukashindwa vitani (1914-1918). Aliiona falsafa ya Umarx kuwa ni itikadi ya Kiyahudi ambayo itapelekea idadi ya binadamu duniani ipunguwe. Kwa hivyo, alihoji Hitler, lazima Wayahudi waangamizwe.
Aliendelea kuhoji kwamba wafanyakazi wa Kijerumani walilazimishwa wawaunge mkono Wasoshalisti na, kwa hivyo, aliamini kwamba lazima nguvu na propaganda zitumiwe kuwalazimisha hao wafanyakazi wauache msimamo wao wa kuwaunga mkono wasoshalisti.
Hitler, kwa ufupi, alikuwa ni fatani mkubwa. Kazi yake ikawa kuwafitinisha wananchi, kama wafanyavyo baadhi ya viongozi wa CCM-Zanzibar na hata wa Bara. Kufikia miaka ya kati ya 1930, fitina za chuki za kikabila ziliwaingia vya kutosha Wajerumani na wengi wao wakaanza kuchukiana. Yaliyofuatia baadaye baada ya Hitler kushika madaraka ya nchi ndiyo hayo mauaji ya kimbari. Takriban watu milioni 11 waliuliwa pamoja na watoto milioni moja wa Kiyahudi.
Hii leo tunaviona viji-Hitler vikichomoza ndani ya CCM-Zanzibar. Vinapita vikibeba mabango ya kibaguzi mbele ya viongozi wa kitaifa, wa chama cha CCM na serikali ya CCM, na hakuna miongoni mwao hao viongozi aliyethubutu kuonyesha ujasiri na uungwana wa kuwakemea.
Lakini ya nini kwenda mbali kwa masafa na wakati kujikumbusha athari za siasa za kibaguzi? Haina haja ya kuiangalia Ujerumani ya zama za Hitler.
Tuyaangalie yaliyojiri katika historia ya hivi karibuni ya majirani zetu wa Rwanda. Tujikumbushe waliyokuwa wakiyafanya Wahutu walio wengi Rwanda dhidi ya wananchi wenzao wa Kitutsi.
Wao walikuwa na jeshi lao la mgambo la “Interahamwe” lililokuwa likiungwa mkono na serikali iliyokuwa ikiongozwa na Wahutu. Interehamwe maana yake “wale wanaofanya kazi pamoja” au “wanaopigana pamoja” yaani wanaoua pamoja.
Mauaji yao yalisababisha vifo vya Watutsi wasiopungua laki nane. Maelfu ya Wahutu waliokuwa wakiyapinga mauaji hayo nao pia waliuliwa.
Zanzibar kuna “mazombi” na “Janjaweed” makundi ambayo mara baada ya mara hufyetuka na kuwashambulia wapinzani. Hadi sasa hakuna aliyefikishwa mahakamani kwa mashambulizi hayo na ndiyo maana wengi wanaamini ya kwamba makundi hayo yameandaliwa na wahafidhina wa CCM.
Baadhi ya wachambuzi, hususan kutoka Bara, wanasema kwamba ushindani wa leo wa kisiasa wa Zanzibar baina ya CCM na CUF ni sawa na ule uliokuwepo zamani baina ya Afro-Shirazi Party (ASP) na Zanzibar Nationalist Party (ZNP au Hizbu). Wao wanasema kwamba Chama cha Wananchi (CUF) ni Hizbu iliyofufuka. Huu ni uzushi mtupu wa kisiasa unaoenezwa kwa makusudi kuwababaisha watu.
Viongozi wote waliokiasisi chama cha CUF walikuwa viongozi wa CCM, waliofukuzwa na chama hicho. Na wote wametokana kwenye matumbo ya kisiasa ya ASP. Hakuna kati yao aliyewahi kuwa mwanachama wa Hizbu na hata kama wangekuwako mmoja au wawili wasingeweza kukifanya chama chao kiwe Hizbu mpya.
Kadhalika wachuguzi hao hao wanasema kwamba chuki za zamani zinarudi Zanzibar. Ukweli lakini ni kwamba zamani hakukuwa na chuki zilizoshtadi kama hizi. Si kwamba hapakuwako chuki lakini chuki hizo zilikuwa zaidi ni za kisiasa si za kikabila.
Hazikuwepo kabla ya Mapinduzi ya 1964 wala hazijakuwako wakati wa utawala wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume.
Hizi chuki ni za sasa na zinapaliliwa na wanasiasa wa chama kimoja wenye nia ya kuitawala Zanzibar milele. Chuki zimezagaa na zinasambazwa na upande mmoja katika medani ya kisiasa ya Zanzibar.
La kustaajabisha ni kwamba wakati wote ushenzi huu unapofanyika Serikali ya Muungano imekaa kimyakana kwamba mambo yote ni shuwari Zanzibar. Wengi wanaamini kwamba kimya hicho si cha bure, kwamba serikali ya Muungano inasubiri kuripuke ili ipate kisingizio cha kupeleka majeshi na izidi kuidhibiti Zanzibar.
Kiroja chengine kilichotokea Zanzibar wiki iliyopita ni matamshi ya kukirihisha ya Balozi Ali Karume. Kwa mtu anayejigamba kuwa ni mwanadiplomasia aliyebobea na aliyeelimishwa Marekani, taifa la kidemokrasia, aliwachafua moyo wengi alipopendekeza kwamba Katiba ya Zanzibar ibadilishwe ili mgombea urais lazima awe anatoka CCM tu.
Kadhalika alisikitisha aliponukuliwa akiwahimiza wapiga kura, ikiwa patafanywa uchaguzi wa marudio, wakichaguwe kwa wingi chama chake cha CCM ili waweze kuibadili Katiba na kuifuta Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Kwa kawaida, matamshi kama haya ni ya kupuuzwa. Lakini inatupasa tuyadhukuru kwa vile yanatolewa katika wakati ambapo hali ya kisiasa ya Zanzibar ni tete na tuseme wazi kwamba hayawezi kusaidia kuleta umoja au kuendeleza demokrasia.
Mbali na hayo, Ali Karume alitushangaza aliposema kuwa Fatma Karume (binti wa kaka yake Rais mstaafu Amani Karume )alimkosea adabu Shein kwa kumkosoa. Haya ni maneno ya mtu anayejiita msomi wa karne ya 21. Alizidikutuacha kinywa wazi alipogusia kwamba kwa kuwa Fatma, ambaye ni wakili, hakusoma chuo alichosoma yeye Ali Karume basi bado hakuelimika.
Lakini hivi ndivyo walivyo baadhi ya wasomi wetu kwani hata Benjamin Mkapa, mwanadiplomasi wa siku nyingi na ambaye baadaye alikuwa Rais wa Tanzania, amewahi kutoa matamshi yasiyolingana na hadhi yake.
Mfano mmoja ni pale alipohojiwa na Tim Sebastian wa BBC katika kipindi cha ‘Hard Talk’ baada ya mauaji ya Pemba 2001. Ilifika hadi Sebastian alimuuliza “inaelekea mheshimiwa umepanda mori ?”Naye akajibu “ndiyo”.
Ukiyasikiliza mahojiano yale ambayo yanapatikana mtandaoni utajiuliza mengi. Pia wakati wa kampeni za uchaguzi wa Oktoba mwaka jana, Mkapa aliwaita wapinzani Tanzania kuwa “malofa na wapumbavu”.
Hainishangazi kwamba Mkapa na wenzake wamekaa kimya, hawasemi kitu kuwakemea wanaourejesha ukabila na ubaguzi katika chama chao. Wanaiacha Zanzibar itote lakini kwa faida ya nani?
- See more at: http://raiamwema.co.tz/kwa-nini-wanaiacha-zanzibar-itote#sthash.iOCUpFsl.dpuf
No comments :
Post a Comment