Aliyekuwa mgombea wa uraisi wa Chadema Edward Lowassa aahidi kuwa bado atagombea uraisi mwaka 2020 na ashaanza mipango hiyo.
*Awataka wabunge wa Ukawa wadai Katiba mpya
NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM, MTANZANIA.
ALIYEKUWA mgombea urais kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambaye aliungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, amesema anajipanga upya kushinda urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.
Lowassa aliweka wazi dhamira yake hiyo, jijini Dar es Salaam jana alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara wanaomwunga mkono wanaojulikana kama Timu Mabadiliko wa Soko la Kariakoo ambao walitaka kusikia kauli na hatima yake kisiasa baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu mwaka jana.
Lowassa ambaye alipata kuwa waziri mkuu, alisema bado hajakata tamaa ya kuwaongoza Watanzania, licha ya vizingiti kadhaa alivyowekewa vikiwamo vya kumzuia kufanya ziara za kuwashukuru wananchi waliompigia kura nchi nzima.
“Wale walio na nia ya kutaka kujua mustakabali wangu kisiasa nawaambia kwamba pamoja na kuwepo kwa mambo ya kutaka kunikatisha tamaa, lakini sitakata tamaa na nipo tayari kuwania urais na kushinda kwa kipindi kijacho cha mwaka 2020.
“Niko fiti na morali yangu iko juu naiona kazi hiyo ndiyo kwanza imeanza najua kama Mungu amepanga nitakuwa rais wa Tanzania niko tayari kuanzia sasa na ninaamini tutashinda kama tulivyoshinda katika uchaguzi uliopita Oktoba 25, “alisema Lowassa.
Kiongozi huyo aliwataka wananchi nao pia kutokata tamaa ya kupata mabadiliko ya kweli kwa sababu yuko tayari kugombea hata mara tano ili apate haki yake kwa sababu anaamini kwa nguvu za Mwenyezi Mungu atakuja kuwa rais wa Tanzania.
“Sitakuwa kiongozi wa kwanza kuwania mara tano kwani yupo rais mmoja wa Marekani aliyewahi kuwania zaidi ya mara nne na alipogombea mara ya tano alifanikiwa kupata urais, mwingine ni rais wa Senegal Abdoulaye Wade,” alisema Lowassa.
Katika mkutano huo, Lowassa pia alizungumzia sababu za kutochukua hatua za kuwaruhusu wanachama na wafuasi wake kuingia barabarani kwa maandamano kudai ushindi.
Kwa mujibu wa Lowassa, hatua hiyo ilichangiwa na dhamira yake ya kutaka kulinda amani ya nchi.
“Matokeo yaliwashangaza wengi nikiwamo mimi mwenyewe, hali iliyosababisha wengi kuniomba nitoe kauli ya kuingia mitaani, lakini nikatumia busara kuwatuliza kwani ningewaruhusu wangechinjana lakini sikutaka kuingia Ikulu kwa kumwaga damu.
“Nawashukuru Watanzania kwa kuwa watulivu na kunisikiliza ombi langu lililowezesha Tanzania kuendelea kuwa na amani kwani sikuwa tayari kuona inavurugika kwa muda mfupi wakati imedumu tangu tulipopata uhuru kwa sababu ya kwenda Ikulu,’ alisema.
Lowassa alisema pamoja na kupokonywa ushindi wake, lakini anaamini vyama vya upinzani vimetoa changamoto kubwa kwa CCM na serikali ya awamu ya tano ambao wameamua kutumia baadhi ya sera zilizokuwa kwenye ilani yao ya uchaguzi.
“CCM wanatakiwa kuwa waungwana pindi wanapo nakili Ilani za Chadema, wanatakiwa kusema ukweli pindi wanapoichukua sera ya chama kama ile ya elimu bure kwa kuwa si jambo baya kwa sababu wanatimiza yale tuliyokuwa tukitaka kuwafanyia Watanzania,” alisema Lowassa.
Katiba mpya
Lowassa alitoa wito kwa wabunge wa Ukawa kutumia vikao vya Bunge la 11 kudai Katiba mpya ambayo itasaidia kuendesha uchaguzi huru na wa haki.
“Matatizo mengi ya chaguzi zetu yamekuwa yakichangiwa na Katiba ambayo imekuwa ikizuia kuhoji matokeo ya kura za urais mahakamani,” alisema Lowassa.
Mgogoro wa kisiasa Zanzibar
Kuhusu mgogoro unaoendelea kati ya CCM na CUF visiwani Zanzibar Lowasa alisema msimamo wa Ukawa ni kwamba Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imalizie kutangaza mshindi wa urais wa visiwa hivyo.
“Msimamo wangu katika mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar hauna tofauti na ule uliotolewa na CUF wa kutaka mshindi atangazwe na si msimamo unaopigiwa chapuo na CCM wanaotaka kurudiwa kwa uchaguzi,” alisema.
Bango la ubaguzi
Akizungumzia bango lenye ujumbe wa ubaguzi kuelekea kilele cha Sherehe za Mapinduzi hivi karibuni, Lowasaa alibeza namna CCM ilivyoomba radhi kuhusiana na bango hilo akisema radhi hiyo ilipaswa kuombwa na kiongozi mwenye nafasi ya juu.
“CCM inatakiwa kumtumia mtu mwenye cheo cha juu wa chama hicho kuomba radhi kwa bango hilo la kibaguzi kuliko kumtumia mtu wa mipasho kufanya hivyo,” alisema.
Lowassa, alisema hatua hiyo ingewasaidia CCM kuondokana na dhana iliyojengeka kwamba chama hicho kinaunga mkono sera za kibaguzi.
Hivi karibuni bango linalodaiwa kuandaliwa na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Zanzibar lilikuwa na ujumbe unaosomeka “Machotara Hizbu, Zanzibar ya Waafrika”.
Ujumbe wa bango hilo umezua mjadala mkubwa, huku baadhi ya watu wakihoji maandalizi yake na wengine wakidai kuwa ni ushahidi kuwa CCM inapalilia mbegu mbaya ya ubaguzi.
No comments :
Post a Comment