Toleo la 440
13 Jan 2016
KITENDO cha Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha, kutoa tamko lisilo halali kikatiba na kisheria la kuufuta Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar pamoja na matokeo yake kumeitumbukiza Zanzibar katika mzozo mkubwa wa kikatiba na kisheria. Aidha, kitendo hicho kimeifedhehesha sana Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mbele ya Jumuiya za kikanda na kimataifa.
Mzozo huo pia umeiweka Zanzibar katika njia panda sio tu kwa hali ya sasa lakini kwa mustakbala wake wa baadaye na kuirejesha nyuma sana katika jitihada za kujenga umoja wa kitaifa unaozingatia misingi ya utawala wa sheria, demokrasia na mfumo wa utawala bora.
Kubwa zaidi, mzozo huo umeleta fadhaa kubwa sana kwa wananchi wa mirengu yote ya kisiasa. Uchumi na ustawi wa Zanzibar nao umeathirika sana. Wananchi wako taaban huku hali ya maisha ikizidi kuwa ngumu na bidhaa zikipanda bei kwa kasi wakati mzunguko wa fedha ukiwa umepotea.
Katika hali hii, hapana budi juhudi za kuutatua mzozo huu zikamilishwe kwa haraka kwa kuzingatia misingi ya kikatiba, kisheria na pia mustakabali utaowafanya wananchi wa Zanzibar waamini kwamba mfumo uliopo wa kikatiba, kiutawala na kisheria ambao umechukua muda kuujenga unaweza kufanya kazi na pale penye kasoro unaweza kuimarishwa hatua kwa hatua kama ambavyo tumekuwa tukifanya kwa miaka kadhaa sasa.
Uhalali wa Mwenyekiti wa Tume kufuta Uchaguzi.
Mbali ya kwamba kitendo cha Mwenyekiti wa Tume kimedhihirika kuwa ni njama za wazi za kisiasa ambazo zilipangwa na kutekelezwa na Mwenyekiti wa Tume, vyombo vya ulinzi na viongozi wa kisiasa ambao sasa wanamtetea, uamuzi wa Mwenyekiti wa Tume kufuta uchaguzi hauna uhalali wowote kwa sababu zifuatazo:
Uchaguzi Kukamilika: Uchaguzi wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ulishakamilika. Kwa upande wa uchaguzi wa Rais nao ulishakamilika isipokuwa hatua ya kutangaza matokeo ambayo nayo kwa mujibu wa sheria ilitakiwa iwe imeshakamilika.
Kama ilichelewa ilicheleweshwa makusudi na Mwenyekiti katika juhudi zake za kutafuta visingizio vya kuharibu uchaguzi ili mshindi halali asitangazwe. Tume haina mamlaka ya kuahirisha, kutengua matokeo au kufuta uchaguzi uliokwisha kamilika. SHERIA YA UCHAGUZI imeeleza wazi mamlaka ya Tume baada ya kazi ya kuhesabu kura kukamilika.
Mamlaka pekee ni ya kurudia kuhesabu kura kwa majimbo yote au kwa Jimbo moja iwapo itaridhika kwamba ipo sababu ya msingi ya kufanya hivyo. Kifungu cha 42(2) cha Sheria ya Uchaguzi imeeleza wazi juu ya uwezo huo wa Tume. Kuipa mamlaka Tume kutengua uchaguzi uliokwisha kamilika ni sawa na kuingilia kazi za mhimili wa Mahkama.
Hata Mahkama yenyewe inafungwa na Sheria ya Uchaguzi. Kifungu cha 123 kimeeleza watu ambao wanaweza kuhoji matokeo ya uchaguzi baada ya kutangazwa na Returning Officer.
Mwenyekiti wa Tume au Tume hawamo katika orodha ya wanaoweza kuhoji uchaguzi baada ya kutangazwa matokeo. Aidha, chini ya Sheria ya Ukomo, Mahkama haiwezi kusikiliza tu shauri lolote lazima izingatie muda unaokubalika kusikiliza shauri;
Mamlaka ya Mwenyekiti: Ni wazi kuwa Mwenyekiti alivunja Katiba. Alikwenda kinyume na kifungu cha 119(1) cha Katiba na alikiuka kifungu cha 119(10) cha Katiba juu ya utaratibu wa Tume kufanya maamuzi kwa kuamua kufuata uchaguzi bila ya kuitisha kikao cha Tume wala kushauriana na Tume.
Kifungu cha 119(1) cha Katiba ya Zanzibar kinaeleza muundo wa Tume ambayo imeshirikisha wadau wakuu wa uchaguzi na watu wengineo huru. Kifungu cha 119(10) kinaweka utaratibu wa Tume kufanya maamuzi na kimeeleza kwa maelezo ya wazi kama ifuatavyo:
“Kiwango cha mikutano ya Tume ya Uchaguzi ni Mwenyekiti au Makamo Mwenyekiti na Wajumbe wanne na kila uamuzi wa Tume ni lazima uungwe mkono na Wajumbe walio wengi.”
Ni dhahiri kuwa Katiba imesisitiza suala la maamuzi ya Tume kufanywa kwa kupitia vikao na uamuzi kufanywa baada ya kuungwa mkono na Wajumbe walio wengi. Katiba imetumia daraja mbili za msisitizo kwa kutumia neno “kila” (maamuzi ya Tume) na neno “lazima”.
Kwa kufanya maamuzi peke yake, Mwenyekiti alipaswa achukuliwe hatua na Rais ya kusimamishwa, kuchunguzwa na akipatikana na kosa kufukuzwa chini ya vifungu vya 119(6), (7) na (8) vya Katiba;
Mamlaka ya Tume: Ingawa Mwenyekiti aliitisha kikao Novemba Mosi na kuitaka Tume ihalalishe kitendo chake cha kufuta matokeo, lakini Tume haina mamlaka ya kuhalalisha kitendo chochote kinachokiuka Katiba au Sheria.
Tume ingeweza kuhalalisha jambo ambalo kwanza Mwenyekiti mwenyewe ana mamlaka nalo na Tume ina mamlaka nalo kulifanya lakini pengine taratibu tu hazikukamilika.
Kwa vile Tume haina mamlaka ya kuhalalisha jambo ambalo ni kinyume na Katiba na Sheria, kitendo cha Tume kutaka kuhalalisha kitendo cha Mwenyekiti cha kufuta uchaguzi uliokwisha kamilika ni batili;
Udanganyifu na Ubatili wa Tangazo Rasmi la Kufuta Uchaguzi: Kama nilivyotangulia kueleza kwamba tarehe 6 Novemba, Mwenyekiti wa Tume alitoa Tangazo Namba 130 katika Gazeti rasmi la Serikali kufuta uchaguzi. Tangazo hilo lina udanganyifu wa wazi na kasoro nyengine kadhaa za kisheria kama ifuatavyo:
Udanganyifu: Tangazo linaeleza kwamba ni uamuzi wa Tume ya Uchaguzi uliofanywa tarehe 28 Oktoba. Kuna ushahidi usio na shaka kwamba tarehe 28 Oktoba, Tume ya Uchaguzi haikukutana kabisa hata kwa njia isiyo rasmi kwa vile Mwenyekiti hakwenda katika kituo cha kutoa matokeo ya uchaguzi seuze kukutana rasmi kwa mujibu wa Katiba na kutoa maamuzi kama Katiba inavyoelekeza;
Migongano: Tamko la Mwenyekiti alilolitoa tarehe 28 Oktoba kupitia vyombo vya habari vya ZBC lilieleza wazi kuwa anafuta uchaguzi na matokeo yake yote. Hata hivyo, Tangazo katika Gazeti Rasmi linaeleza kuwa amefuta matokeo ya uchaguzi. Huu ni mgongano mkubwa ambao una maswali mengi bila majibu;
Athari ya mambo yote haya ni ukiukwaji mkubwa na wa wazi wa Katiba ambao hauwezi kutetewa au kuhalalishwa kwa kutambua ufutwaji usio halali wa uchaguzi unaodaiwa kufanywa na Mwenyekiti wa Tume.
Hoja ya Kurudiwa Uchaguzi
Hoja ya kurudiwa uchaguzi ambayo imeshikiwa bango na Chama cha Mapinduzi, Zanzibar ni ya kutafuta manufaa ya kisiasa baada ya Chama cha Mapinduzi kushindwa katika uchaguzi.
Mbali ya matokeo ya uchaguzi ya Urais wa Zanzibar ambayo yanaonyesha wazi kuwa CCM imeshindwa kwa kura nyingi sana kwa kiwango na uzoefu wa Zanzibar, hata kura za Urais wa Jamhuri ya Muungano kwa upande wa Zanzibar zinaonyesha hivyo hivyo na kwa hiyo kuthibitisha kuwa CCM ilipoteza uchaguzi huo. Kwa muhtasari matokeo ya Urais wa Muungano kwa upande wa Zanzibar ni kama yafuatavyo:
MGOMBEA KURA HALALI ASILIMIA
DR. JOHN POMBE MAGUFULI 194,317 46.5%
EDWARD NGOYAYE LOWASSA 211,033 50.50%
IDADI YA KURA HALALI 417,882
Matokeo ya kura za Ubunge, Uwakilishi na Udiwani yote yanaonyesha CCM imeshindwa kwa idadi ya kura za walio wengi (popular votes). CCM imeweza kupata viti sawa na CUF katika uwakilishi na ubunge kwa sababu ya mbinu zilizotumika katika ukataji wa majimbo.
Hivyo, kimsingi Hoja ya kurudia uchaguzi haina msingi na haiwezekani kutekelezwa kwa sababu kadhaa. Miongoni mwa sababu hizo ni pamoja na zifuatazo:
a) Kukosekana Uhalali wa Msingi wa Kurejea Uchaguzi
Kama ilivyoelezwa awali kwamba hatua ya Mwenyekiti wa Tume kufuta uchaguzi haikuwa halali na ina kasoro nyingi za kikatiba na kisheria. Kurejea uchaguzi ni sawa na kuhalalisha kitendo batili alichofanya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi. Aidha ni kuweka “precedent” mbaya kwamba uchaguzi unaweza kufutwa kwa sababu zozote zile japo kama sio halali.
Kiini cha mzozo uliozushwa katika uchaguzi ni uamuzi batili wa Mwenyekiti wa Tume. Kurejea uchaguzi bila kupatia ufumbuzi juu ya uhalali wa uamuzi wa Mwenyekiti ni sawa na kuhalalisha kitendo cha Mwenyekiti na kutoa ruhusa kuwa huko mbele anaweza kufanya tena kitendo kama hicho au Tume inaweza kufanya kitendo kama hicho.
Hii ni kujenga msingi wa kuwa na chaguzi zisizokwisha na mizozo isiyo na mwisho. Lazima mipaka ya Mwenyekiti na Tume iwekwe bayana ili hapo baadaye ijulikane nini ukomo wa mamlaka yao.
Kujenga Imani ya Wapiga Kura
Uchaguzi ni wa wapiga kura na sio wa vyama au wagombea. Lazima wapiga kura waridhishwe kuwa uchaguzi ulikuwa na tatizo la kiasi cha kuufanya matokeo yake yasionyeshe dhamira na uamuzi wa wapiga kura. Hadi sasa hakuna mwelekeo unaonyesha kuna ukweli katika tuhuma za kasoro za uchaguzi.
Moja ya madai ya CCM ni kwamba eti Pemba watu waliopiga kura walikuwa ni zaidi ya walioandikishwa lakini ukweli ni kwamba takriban watu 29,000 walioandikishwa hawakupiga kura kisiwani humo.
Katika mazungumzo yanayoendelea Ikulu, Zanzibar baina ya viongozi, CCM imetakiwa mara kadhaa kuleta ushahidi wa tuhuma zake kwamba kulikuwa na hujuma lakini imeshindwa kufanya hivyo. Matamko ya Waangalizi wa Uchaguzi na namna tuhuma za kasoro za uchaguzi zilivyoibuliwa na Mwenyekiti wa Tume haziwezi kuwashawishi wapiga kura kwamba kulikuwa na kasoro katika uchaguzi.
Hoja ya kurudiwa uchaguzi inaonekana wazi kuwa ni ajenda ya kisiasa ya chama kilichoshindwa. Hali hii ni sababu tosha ya kuleta fujo iwapo hatua yoyote ya kurudia uchaguzi itachukuliwa.
Changamoto za Kuunda Tume Mpya ya Uchaguzi
Ni dhahiri kuwa uchaguzi wa Zanzibar umehujumiwa na Mwenyekiti wa Tume kwa sababu ya sindikizo la kisiasa. Kwa vyovyote vile yeye hafai tena kuendelea kuiongoza Tume hiyo katika kazi yoyote ya Tume iliyobaki. Ni lazima akae pembeni.
Kurejea uchaguzi ni sawa na kuihukumu Tume nzima kuwa ina makosa wakati makosa hayo yalifanywa na mtu mmoja tu. Hivyo, kwa vyovyote vile, kama uchaguzi utarudiwa, haitawezekana kwa Tume iliyopo na Sekretarieti kusimamia uchaguzi wa marudio. Kufanya hivyo ni mgongano mkubwa wa maamuzi kwamba Tume iliyokiri kuharibu uchaguzi isimamie tena uchaguzi wa marudio.
Hivyo, kama Tume na Sekretarieti itabidi iondoke na kuunda Tume na Sekretarieti mpya, bado kutakuwa na changamoto kubwa zaidi ya kuunda Tume mpya ya uchaguzi. Miongoni mwa changamoto kubwa ni kama zifuatazo:
Kuondolewa Wajumbe waliopo: kwa mujibu wa kifungu cha 119(6),(7) na (8) cha Katiba, Wajumbe wa Tume wana kinga ya kutoondolewa katika nafasi yao isipokuwa kwa kufuata utaratibu maalum sawa na ule wa kumuondoa Jaji wa Mahakama Kuu (Security of Tenure).
Njia nyingine nyepesi ni kwa mjumbe kujiuzulu kwa hiari yake. Hii ni changamoto kubwa hasa kwa kuzingatia kwamba wajumbe wanaamini kwamba hawakufanya makosa yoyote na aliyefanya makosa tena kwa makusudi anajulikana lakini analindwa kwa maslahi ya kisiasa;
Muda wa kujenga uwezo wa kiutendaji na wa kitaasisi
Hata kama changamoto zilizotajwa hapo juu zitapatiwa ufumbuzi, changamoto kubwa ni ile ya muda utaohitajika kujenga uwezo wa kiutendaji kwa Sekretarieti na wasaidizi wao katika ngazi ya Mikoa na Wilaya na Wajumbe wa Tume ili waweze kusimamia uchaguzi kwa ufanisi wa viwango vinavyokubalika.
Changamoto nyingine ni ya muda utaohitajika wa Tume kuhakiki na kujiridhisha na daftari la wapiga kura ambayo ndio nyenzo kuu ya uchaguzi. Kwa vyovyote vile muda utaohitajika kwa Tume mpya kujiandaa hadi kufanya uchaguzi mwengine kwa kiwango cha chini kabisa ni angalau mwaka mmoja.
Suala muhimu ni kwamba nchi itawezaje kwenda wakati hakuna Baraza la Wawakilishi wala hakuna Baraza la Mapinduzi. Kutokuwepo kwa Baraza la Mapinduzi kwa maana ya mawaziri kutaathiri sana utendaji kwa vile mawaziri wana mamlaka makubwa ya kisheria chini ya sheria mbali mbali kama vile za fedha hivyo kutokuwepo kwao au uwepo wao usiokuwa halali kisheria kuna athari kubwa katika utendaji wa Serikali. Changamoto kubwa zaidi ni suala la bajeti ya Serikali ambayo ni lazima iandaliwe na ipitishwe ndani ya muda maalum.
Njama za kuhujumu utafutaji wa haki
Wakati Dk. Ali Mohamed Shein akikwepa kwa makusudi kuitisha kikao cha kupokea taarifa ya mazungumzo hayo, tumegundua kwamba lengo halisi ni kuisindikiza Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kutangaza tarehe ya uchaguzi wa marudio ili baadaye itolewe hoja kwamba suala hilo limeshaamuliwa.
Tunazo taarifa za uhakika kwamba Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imetakiwa kukutana tarehe 14 Januari, 2016 kwa lengo la kutangaza tarehe ya uchaguzi wa marudio ambao unatajwa kuwa umepangwa ufanyike tarehe 28 Februari, 2016.
Hitimisho
Zanzibar imepita katika siasa za dhoruba na machafuko kwa zaidi ya miaka 50. Dhoruba na machafuko hayo yalifikia hadi kugharimu maisha ya watu. Ni kwa sababu ya kuchoshwa na siasa za aina hiyo na migogoro isiyokwisha ndiyo maana mwaka 2009, mimi na Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Amani Karume, tulichukua maamuzi ya kijasiri ya kuleta MARIDHIANO ambayo yaliituliza Zanzibar.
Kila mmoja wetu ni shahidi kwamba kwa miaka sita iliyopita Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipumua kujibu hoja zisizokwisha kuhusu hali ya kisiasa Zanzibar na badala yake tukawa tunapongezwa kwa kuleta maridhiano na kuanzisha muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Hatukutegemea kwamba baada ya kazi ile kubwa, sasa kutazuka kikundi cha viongozi waliopewa dhamana ya kuwaunganisha watu wafanye kazi ya kuyabomoa Maridhiano yetu na kuturudisha kwa nguvu kule tulikotoka. Watu hawa hawapaswi kupewa nafasi kufanikisha dhamira yao hiyo ovu.
Na Wazanzibari hawatowapa nafasi hiyo. Ni kwa sababu hiyo tumeamua kuzungumza na Watanzania na kuwajuvya haya ili kuzuia nchi yetu isivurugwe na kurudishwa tulikotoka.
Tunaamini kwamba ufumbuzi wa mgogoro uliopo lazima uzingatie Katiba, Sheria na misingi ya utawala bora. Mapendekezo yaliyotolewa hapo juu ndio njia pekee ya kuutatua mzozo huo kwa kuzingatia misingi iliyotajwa.
Utatuzi wowote nje ya hapo utakuwa ni wa nguvu na wa utashi wa kisiasa ambao hautaleta ufumbuzi endelevu na badala yake unaweza kuwa sababu ya mzozo mkubwa ambao hautaweza kutatuliwa kwa miaka mingi ijayo. Tumuombe Mwenyezi Mungu tusifike huko.
Mimi na wenzangu tumefanya kazi ya ziada kuwatuliza wananchi wa Zanzibar na kuwataka watoe nafasi kwa mazungumzo yanayoendelea huku kuwahakikishia kwamba suluhisho lolote litakalofikiwa litaheshimu maamuzi yao ya kidemokrasia waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015.
Tumefanya hivyo kwa kutambua wajibu wetu kama viongozi kuhakikisha kwamba Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inabaki kuwa salama. Ni bahati mbaya sana kwamba wengine wanauchukulia uungwana na ustaarabu wetu kwamba labda ni dalili ya udhaifu na wanadhani labda wanaweza kutuburuza. Kwa hilo, nawaambia wazi kwamba WASAHAU.
Nataka niwahakikishie kwamba sisi si dhaifu ila tunaongozwa na uzalendo na mapenzi kwa nchi yetu na wananchi wenzetu. Lakini uzalendo huo huo na mapenzi hayo hayo kwa nchi yetu na wananchi wenzetu yanatutaka tusimame kuitetea na kuilinda Katiba na Sheria za nchi yetu, haki za raia na maamuzi yao ya kidemokrasia.
Zanzibar kuna tatizo kubwa ambalo halipaswi kuendelea kupuuzwa. Wakati umefika kwa mamlaka zinazohusika kutokwepa wajibu wao kwa wananchi wa Zanzibar.
Mimi na wenzangu, kama viongozi twenye dhamana kwa wananchi wa Zanzibar ambao walitupa ridhaa yao, tunawahakikishia kwamba tutakuwa tayari kushirikiana nao kuitetea haki yao na maamuzi yao ya kidemokrasia kwa nguvu zetu zote.
Hii ni sehemu ya hotuba ya Katibu Mkuu wa CUF, Seif Shariff Hamad, aliyoitoa kwa waandishi wa habari juzi Jumatatu, Januari 11, 2016, jijini Dar es Salaam. Hamad pia ndiye alikuw mgombea urais wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2015.
- See more at: http://raiamwema.co.tz/maalim-seif-kwanini-napinga-kurudiwa-uchaguzi#sthash.LKP6eHC5.dpuf
No comments :
Post a Comment