Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, January 24, 2016

Maaskofu wampa rungu Magufuli

Askofu Amos Kinyunyu wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Dodoma
 MAASKOFU na wachungaji wa makanisa mbalimbali nchini wamebariki kasi ya Rais John Magufuli na kuahidi kuendelea kumwombea ili aendelee kutumbua majipu ya ufisadi na rushwa ambayo yamelitafuna taifa kwa muda mrefu.

Waliyasema hayo jana kwa nyakati tofauti kwenye mikoa mbalimbali nchini wakati wa ibada ya sikukuu ya Krismas, ikiwa ni kumbukumbu ya kuzaliwa Yesu Kristu, iliyosherehekewa duniani kote na waumini wa dini ya kikristu.

Askofu Amos Kinyunyu wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Dodoma, alisema kasi ya Magufuli inaridhisha na inatoa matuimaini kwa Watanzania hivyo wanapaswa kuzidi kumuombea ili apate nguvu ya kuendelea kuwatumikia Watanzania wa hali ya chini.
 
Alisema Kanisa litaendelea kumuombea ili aweze kufanya kazi anayoendelea kufanya sasa hivi kwani hata vitabu vitakatifu vinataka usawa katika uchumi wa kipato kwa kila mtu.“Tunawaomba Watanzania tuzidi kumuombea Rais wetu ili kasi aliyonayo aendelee nayo hivyo hivyo kwani Mungu anapenda haki katika maisha pamoja na uchumi uliosawa na rais wetu ameonyesha kwamba ni mtu anayewajali sana watu wenye kipato kidogo,” alisema Askofu Kinyunyu.
 
“Wakati mwingine hii kauli ya hapa kazi tu hata sisi viongozi wa dini inatuogopesha maana inahitaji ujasiri sana, lakini asiogope; aendelee na mwendo huo huo na Mungu ataendelea kumlinda na kumwongoza,” alisema.
Naye Mchungaji kiongozi wa Kanisa la Tanzania Assembles of God (CCC), Miuji Dodoma, Samson Mkuyi alisema utawala wa Rais Magufuli unaonekana kuwa ni jibu la Watanzania wengi ambao walikuwa wamekata tamaa pamoja na kanisa.
Mchungaji Mkuyi alisema wanafurahishwa na utendaji kazi wake hasa kwenye kurejesha maadili kazini, ikizingatiwa kuwa kanisa linataka maadili ya kiroho na kimwili.
 
“Tulianza kuyaomba haya miaka mitano sisi kama kanisa... Tunamwambia Magufuli asiogope kwani Mungu yupo pamoja na yeye, sisi tunaendelea kumuombea ili mungu aendelee kumpa ulinzi,” alisema.
 
Kwa upande wake, Askofu la Kanisa la Anglikani Central Tanganyika Dayosisi ya Kati, Dk Dickson Chilongani aliwataka watanzania kumuombea Rais Magufuli pamoja na Baraza lake la Mawaziri ili waweze kuwafanyia kazi watanzania.
“Rais aliahidi kutumbua majipu yaliyojificha na ameyatumbua kweli, na sisi katika hili tutaendelea kumuombea ili aweze kuyayatumbua zaidi na kuwafanya watendaji wafanye kazi ya kuwatumikia wananchi,” alisema
 
Naye Mchungaji Emmaus Mwamakula wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Mashariki na Pwani, ametumia sherehe za Krisamas kumpongeza Rais Magufuli kwa utendaji wenye kasi; unaogusa kero za wananchi wa kawaida ambao walikuwa wamekata tamaa.
 
Alisema kanisa linampongeza Magufuli kwa juhudi zake za kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi zinatumika ipasavyo na kuwapa tumaini jipya Watanzania wa hali ya chini.
 
“Katika sikukuu hii nampongeza Rais lakini pia natoa wito kwa Watanzani kuendelea kudumisha amani ya nchi yetu,” alisema Mwamakula.
 
Askofu wa Kanisa la PHAM Kanda ya Kati, Julias Bundala alielezea furaha yake kwa uongozi wa Rais Magufuli na kuahidi kuwa Kanisa lake litaendelea kumwombea ili aweze kutimiza majukumu yake ipasavyo.
 
Alisema kazi inayofanywa na Magufuli imewafurahisha Watanzania wengi na hata wa mataifa ya nje, hivyo kuna kila sababu ya kumtia nguvu ili asilegeze kamba kwenye mapambano dhidi ya ufisadi nchini.
 
“Tunamwomba Mungu amtie nguvu, amwezeshe Rais wetu Dk. John Magufuli ili tuweze kuendelea vizuri na kazi zake ili atutumikie watanzania na hatimaye nchi iweze kuondokana na umaskini,” alisema Askofu huyo.
 
“Ninawatakia heri ya Krismas watanzania wote na tuitumie siku ya leo vizuri kumuomba Mungu, kuiombea nchi yetu na pia kumuombea Rais wetu ambaye ameanza kazi zake kwa nguvu na kwa kasi ili kasi hiyo iheshimike kila mahali.
“Watanzania tubadilike sasa, tuachane na mambo ya rushwa, ufisadi, matumizi ya madawa ya kulevya.”
 
Msaidizi wa Askofu wa Kanisa la Kiinjili na Kiluteli Tanzania (KKKT), Chediel Lwiza aliwataka watanzania kuendelea kuiombea serikali ili amani iliyopo idumu na wananchi wafanye kazi zao bila bugudha.
 
Alisema migogoro ya wakulima na wafugaji inayoendelea nchini itaisha ikiwa tu Watanzania watatimiza wajibu wao wa kutunza mazingira na kudumisha upendo.
 
Askofu Lwiza alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam katika Ibada ya kumbukumbu ya kuzaliwa Yesu Kristu iliyofanyika katika Kanisa la KKKT la Azania Front.
 
Katika mahubiri yake, Askofu Lwiza alisema wakulima na wafugaji wanauwana wenyewe kwa wenyewe na kusahau kwamba wao ndio chanzo cha mafarakano hayo kwa kutotimiza wajibu wao wa kutunza mazingira.
 
Alisema wakati Mungu akiiumba ulimwengu kazi aliyompa Adamu ni kutunza na kuhifadhi mazingira, agizo ambalo limepuuzwa na kizazi cha sasa.
 
Alisema uharibifu mkubwa wa mazingira umesababisha maji kuwa bidhaa adimu katika Jiji la Dar es Salaam, huku maeneo mengine yakikumbwa na mafuriko.
Pia Askofu Lwiza aligusia suala la ubaguzi wa dini na kueleza kuwa kuna vikundi vingi vinavyohusika na ugaidi ambavyo  vimevaa vazi la dini.
Alisema vikundi hivyo vimekuwa vikisababisha vifo vya watu wakiwemo wanawake na watoto ambao hufanyiwa unyama kabla ya kuuawa.
 
Naye Mwadhama Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo ameitaka jamii kutoamini kuwa watu wenye uwezo kifedha ndiyo wanaweza kuleta mabadiliko katika jamii, bali hata watu wa kawaida wanaweza kubadili jamii kisiasa na kiuchumi.
 
Pengo aliyasema hayo juzi usiku katika Kanisa la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam kwenye ibada ya mkesha wa sikukuu ya Krismasi, akisisitiza kuwa huo ni ujumbe mkubwa katika kumbukumbu za miaka 2000 tangu kuzaliwa kwa kristo.
 
Alisema kundi ambalo jamii haliwapi kipaumbele linaweza kufanya mabadailiko makubwa tofauti na dhana iliyopo katika jamii kuwa watu walio na kipato huweza kuleta mabadiliko iwapo hawataionea aibu kazi yao katika kutekeleza majukumu yao.
 
Aidha, Kardinali Pengo aliwataka wachungaji kulinda kondoo wao kila mmoja kwa nafasi yake, ili kuiinua jamii na taifa kwa ujumla kwani watu walio tayari kufanya kazi usiku na mchana ndiyo wanaotakiwa na Watanzania wasiogope kufanya hivyo kwasababu Mungu atawajalia Neema.
 
“Tunapaswa kuchunga kondoo wetu kila mtu katika nafasi yake ili wawe salama watu ambao jamii huwadharau hali yao wanaweza kuleta mabadiliko watu wasiionee aibu kazi yao watekeleze majukumu yao na kufikisha ujumbe,” alisema Kardinali Pengo na kuongeza.
 
“Ili tuweze kuijenga nchi yetu kiuchumi na kisiasa, lindeni makundi yenu wachungaji wote na Mwenyezi Mungu atujalie hayo sisi  wachungaji katika kulinda makundi yetu, msijiskie  vibaya,” alisema Kardinali Pengo. 
 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment