dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, January 19, 2016

Machozi yangu hayajafutika, najua nitakufa-Rehema

Mwathirika wa bomoabomoa eneo la Mkwajuni Dar es Salaam, Rehema akimfariji mwenzake Aziza, baada ya kufiwa na mtoto katika eneo hilo hivi karibuni. Wengine ni watoto wa Rehema. Picha na Tumaini Msowoya
By Tumaini Msowoya, Mwananchi
Haikuwa rahisi kuvumilia wingu la simanzi lililokuwa limewagubika wanawake wawili, waliokuwa wamekumbatiana wakilia kwa uchungu.
Moyo uliniuma niliposikia maneno ya wanawake hao wakiliwazana. Kila mmoja alimliwaza mwenzake akimtaka avumilie yale anayopitia, kwa kusema ipo siku yote yatakwisha. Ni mapito tu.
Mwanamke mmoja ni mjamzito wa miezi minane na wiki tatu. Huyu wa pili amefiwa na mtoto aliyekuwa na umri wa miezi miwili na nusu,(Luffi Ibrahim), baada ya kupata ugonjwa wa kichomi kutokana na baridi ya usiku.
Wanawake hawa wote wanaishi kwenye kibanda kidogo cha mabati kilichojengwa juu ya kifusi cha nyumba zilizokumbwa na operesheni ya bomoabomoa, eneo la Mkwajuni katika Bonde la Mto Msimbazi, Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Operesheni hiyo iliyokuwa ikienndeshwa na kuzipitia zaidi ya nyumba 700 zilizojengwa kwenye bonde hilo kinyume cha sheria.
Wapo waliofanikiwa kuondoka lakini wengine hawakuweza kufanya hivyo kutokana na ugumu wa maisha na kwamba hawakupewa taarifa ya kuwapo kwa bomoa bomoa hiyo.
Hali ni mbaya zaidi kwa watoto hasa walio na umri chini ya miaka mitano na wanawake wajawazito.
Kauli za wanawake zinaonyesha wamekata tamaa ya kuishi. Hawana matumaini tena. Kwa hakika wanahitaji msaada wa haraka.
Mjamzito, Rehema Rajab (25) na rafiki yake Aziza Motto ambaye alifiwa na mtoto Januari 11, na kuzikwa katika makaburi ya Mwananyamala, kila mmoja anaona dunia chungu kutokana na magumu wanayopitia maishani mwao kwa sasa.
“Sina hakika kama nitaishi muda mrefu kwa kuwa hakuna nuru yoyote mbele yangu. Najua nitakufa tu, nateseka na ujauzito huu ambao siku yoyote natarajia kujifungua, sijui itakuwaje! Sina pesa wala mahali pa kuishi na mtoto atakayezaliwa,” anasema Rehema.

Siku alipovunjia nyumba
Rehema anasema wakati akinywa chai nyumbani kwao, Desemba 17, mwaka jana ghafla alisikia sauti za watu wakipiga kelele kuashiria kuna jambo linaendelea kwenye mtaa wao.
“Nilipotoka niliona tingatinga likiwa limewekwa tayari kwa kuanza kubomoa nyumba. Tuliamrishwa tutoe vitu vyote ndani ili nyumba zibomolewe,” anasema.
Anasema alianza kutoa vitu nje ili aviokoe, lakini kila alipotoa kimoja na kwenda kukifuata cha pili, vibaka waliokuwa wamevamia eneo hilo walimuibia.
Rehema ambaye anaishi na wazazi wake ambao ni wazee eneo la Mkwajuni anasema mpaka tingatinga lilipofika kwenye eneo hilo hawakuwa na taarifa yoyote kuhusu kuvunjiwa nyumba yao.
Hata hivyo, hakufanikiwa kutoa vitu vyote na kwamba vingine vilifinyangwa na tingatinga.
“Hapakuwa na taarifa kama watakuja kubomoa nyumba yetu, ilikuwa ghafla, sikuweza kuokoa kitu chochote,” anasema na kuongeza:
“Moyo ulianza kwenda mbio, niliteseka na sikujua nini cha kufanya wala wapi pa kwenda, wala sikujui itakuwaje. Niliishia kulia, mpaka leo machozi yangu hayajafutika,” anasema.

Maisha juu ya kifusi
Kibanda anachoishi na familia yake hakifai kwa afya ya mjamzito na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, alionao Rehema.
“Wazazi wangu ni vikongwe, mimi mjamzito na wanangu ni wadogo. Sisi sote Serikali huwa inasema tunakipaumbele, lakini hakika haitutambui hata kidogo. Ni mateso usiku kucha mchana kutwa,” anasema.

Chakula
Rehema anasema mara kadhaa wamekuwa wakilala na njaa kwa kutokuwa na fedha kununulia chakula.
“Binafsi sijawahi kushiba tangu nianze maisha haya, sijui mwanangu huko tumboni atakuwa na afya gani kwani mama yake nimekonda,” anasema.
Anasema kuna wakati amekuwa akiishiwa nguvu na kulazimika kushinda akiwa amelala kutokana na njaa.

Afya yake
Rehema anasema wakati wowote anatarajia kujifungua na kwamba muda mwingi hujisikia maumivu mwilini, bila kuwa na msaada wowote tangu wabomolewe nyumba yao.
“Nakosa lishe na haya mazingira ninayoishi hayanifai kutokana na ujauzito nilionao. Hakika sijui kabisa kesho yangu kama nitakuwa hai au lah,” anasema.
Hata hivyo, anasema hofu yake ipo kwa watoto wake wawili mmoja akiwa na miaka miwili na miwngine miaka sita, anaoishi nao kwenye kibanda hicho.
Anasema licha ya Serikali kuwa na sera zinazojali afya ya wajawazito na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, maisha yao kwenye bonde hilo yanaonyesha kuwa Serikali haijawajali.
“Serikali wakati inabomoa nyumba ilijua kuna wajawazito na watoto, tunahitaji msaada wa hali na mali ili tunusuru viumbe hawa wa Mungu,” anasema na kuongeza:
“Kama nikijifungua na kuja kuishi eneo hili na kichanga, sitarajii uhai wa muda mrefu, naweza kumpoteza mwanangu kama ilivyomtokea rafiki yangu ambaye bomoabomoa imegharimu uhai wa mtoto wake.”

Mawazo yake baada ya kujifungua
Kuna vitu ambavyo mjamzito hutakiwa kuwa navyo ikiwa ni maandalizi wakati na baada ya kujifungua.
Mbali na fedha, mjamzito hupaswa kuandaa vifaa vya kujifungulia kama beseni, nguo na vitu vingine.
Hata hivyo, kwa Rehema huenda ikawa ni ndoto kuvipata.
“Sina hela yoyote, kila nachopata nawalisha watoto na wazazi wangu. Sina kitu, hakika maisha yangu yapo mikononi mwa Mungu. Watanzania wenzangu chonde saidieni kuokoa kiumbe huyu aliye tumboni mwangu,” anasema.

Mume amkimbia
“Hakika sijui mume wangu yupo wapi, tangu tubomolewe sijawahi kumuona tena na hapo ndiyo uchungu wangu unaongezeka. Sina msaada na siwezi kumtuhumu kuwa amenitelekeza na watoto kwa sababu bado mapema. Pengine alichanganyikiwa akaondoka,” anasema Rehema.

Aziza na kifo cha mtoto wake
Wakati wote mwandishi alipokuwa akizungumza na Rehema, kando Aziza alikuwa akiendelea kulia na kuomboleza kwa uchungu kwa kufiwa na mtoto wake.
Anasema Saa 12 jioni ya Januari 11, ghafla mtoto wake alianza kuumwa na kumpeleka Hospitali ya Mwananyamala, jijini Dar es Salaam kwa matibabu ambako alilazwa baada ya kuelezwa na madaktari kwamba anasumbuliwa na kichomi.
Licha ya madaktari kuhangaika kumtibu, mtoto huyo Luffi Ibrahim aliaga dunia ilipofika saa 5 usiku.
“Mwanangu wa pekee alikufa huku nikimuona, kama ningekuwa naishi kwenye nyumba yetu iliyobomolewa mtoto wangu asigepoteza maisha. Kuishi kwenye banda kumegharimu uhai wa mwanangu, inauma sana,” anasema Aziza akilia.
Anasema hakubahatika kupata mtoto mapema na kwamba, mtoto huyo alizaliwa Novemba 5, mwaka jana siku ambayo Rais John Magufuli aliapishwa.

Msiba
Aziza na wanawake wenzake wanaoishi Mkwajuni hawakuwa na uwezo wala nyumba kwa ajili ya kufanyia shughuli za msiba. “Tulijikusanya eneo la Hospitali ya Mwananyamala tukalia na tukaenda kumzika mtoto kwenye makaburi ya Mwananyamala. Mwanangu amezikwa kinyonge sana,” anasema.
Aziza anasema alichukuliwa na wenzake akahifadhiwa kwenye nyumba nzuri kwa siku mbili baada ya msiba, kisha kurejeshwa kwenye kibanda chake ambako mtoto wake, aliugua kichomi kutokana na baridi kali nyakati za usiku.

Maisha baada ya kufiwa
Wanawake hao wawili wanasaidiana katika maisha yao.
“Kila nikitazama eneo nililokuwa namlaza mwanangu, machozi hunitoka, sina cha kufanya zaidi ya kumsaidia mwenzangu ambaye siku nyingi atajifungua,” anasema.
Aziza ndiyo msaada uliobaki kwa Rehema. “Hali yake ikibadilika basi huwa nakimbia huku na kule kutafuta msaada ili mradi maisha yanakwenda, nina uchungu wa kufiwa na mwenzangu hali yake ndiyo hiyo,” anasema

Wito kwa Serikali
Wanawake hao wanaiomba Serikali kujenga tabia ya kufanya tathmini kabla ya kutekeleza mpango wowote hata kama wananchi wanatuhumiwa kuvunja sheria.
Aziza anadai kwenye bonde hilo hapakufanywa tathmini ya madhara yanayoweza kutokea baada ya bomoabomoa hiyo.
Hata hivyo anasema wanasubiri hatma ya mahakama kuhusu nyumba zilizobomolewa kwenye eneo hilo.

No comments :

Post a Comment