dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, January 23, 2016

Magufuli anogesha Arusha kwa kombati za kijeshi


Rais John Magufuli akisalimiana na wananchi wa Kisongo nje kidogo ya Jiji la Arusha waliojitokeza kumsalimia wakati akielekea Monduli kwa ajili ya kufunga zoezi la Onyesha Uwezo wa Medani. Picha na Ikulu

By Filbert Rweyemamu na Mussa Juma, Mwananchi
Arusha. Rais John Magufuli, jana alisababisha mitaa kadhaa ya Arusha kufungwa alipokuwa akielekea Chuo cha Maofisa wa Jeshi (TMA) Monduli, huku akiwa amevalia mavazi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Dk Magufuli anakuwa Rais wa pili wa Tanzania kuvaa mavazi ya kijeshi baada ya Rais wa Kwanza, Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliyevaa mavazi hayo alipowatembelea wapiganaji waliokuwa mstari wa mbele wakati wa Vita ya Kagera mwaka 1979.
Rais Magufuli alikuwa akienda Monduli ambako leo  anatarajiwa kuwatunukia nishani, maofisa wa JWTZ ikiwa ni mara yake ya kwanza akiwa Amiri Jeshi Mkuu.
Licha ya kuwa Arusha ni ngome ya upinzani, mamia ya wananchi walijitokeza kumsalimia kiongozi huyo tangu alipokuwa akitoka kwenye makazi yake jijini hapa.
Kutokana na kuzoeleka akiwa katika mavazi ya kiraia, picha za Dk Magufuli akiwa kwenye kombati, zilizagaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii na kupokewa kwa hisia tofauti.
 “Mimi naangalia simuoni, nikashangaa kuona amevaa gwanda, he! Rais kavaa gwanda…,” alisikika akisema mama mmoja aliyekuwa akihangaika kutaka kumwona.
Umati wa watu ulisababisha msongamano uliodumu kwa takribani saa mbili katikati ya jiji na kusababisha foleni kubwa katika barabara inayokwenda Manyara, Mara, Singida, Dodoma na kwenye hifadhi za Taifa.
Alipofika Ngarenaro na Unga Limited wananchi, baadhi wakiwa na mabango, walizuia msafara wake zaidi ya mara ya tano. Rais alichukua mabango hayo na kuyasoma kisha kuwapa wasaidizi wake.
“Nawashukuruni sana watu wa Arusha, mmeonyesha mapenzi makubwa kwangu, nami sitaacha kuwapenda, uchaguzi umekwisha sasa ni kuchapa kazi tu, uwe wewe ni wa  Chadema au CCM mimi ni Rais wa wananchi wote,” alisema.
Wananchi wengi walilazimika kutumia pikipiki zilizokuwa zikipita kandokando kutokana na barabara kufungwa huku wananchi na maofisa wa usalama waliokuwa wakisimamia usalama huku wengine wakitembea kwa miguu umbali mrefu.
Mkazi wa Kwamrombo, Daniel Elisa alisema hamasa iliyoonyeshwa na wananchi ni ishara ya kuunga mkono utendaji wake wa kazi hususan katika utoaji wa elimu bure na kudhibiti matumizi ya fedha za umma.
Atangaza ajira jeshini
Akiwa TMA, Rais Magufuli aliagiza kuajiriwa askari zaidi ya 800 ambao jana walishiriki na kuonyesha uwezo wa medani  za kijeshi.
Akizungumza baada ya kushuhudia mazoezi hayo ya kijeshi, ambayo yalishirikisha askari wa JWTZ, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na mgambo, Rais Magufuli alisema ameridhishwa na uwezo mkubwa wa walioshiriki mazoezi hayo.
“Nimefurahi sana kuona zoezi hili kwa mara ya kwanza na naagiza wale wote waliofanikisha kuajiriwa na jeshi,  nimeambiwa mpo 800 mpaka1,000 lakini pia nitashirikiana nanyi kuhakikisha masilahi yenu yanaboreshwa sambamba na kufufua Kambi ya Nyumbu,” alisema.
Alisema historia ya nchi, inaonyesha jinsi JWTZ ilivyo imara katika kuhakikisha nchi inakuwa na ulinzi wa kutosha kwenye mipaka sambamba na kushiriki kulinda amani katika nchi mbalimbali.
Rais Magufuli alimuagiza Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi na Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue kuandaa mkakati wa kuhakikisha kunakuwa na kiwanda maalumu cha kutengeneza sare za jeshi.
Alisema atashirikiana na jeshi kujenga uchumi wa nchi akisema askari hawahitaji kamisheni ya asilimia 10  au kuiba hata kama watashirikiana na raia.
Awali, Mkuu wa Majeshi, Jenerali Devis Mwamunyange alisema jeshi lake linaendelea kuhakikisha nchi inakuwa na amani na utulivu na kwenda kisasa zaidi.

No comments :

Post a Comment