Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, January 23, 2016

Magufuli atinga ngome ya Lowassa kijeshi

Rais John Magufuli jana alikuwa kivutio cha aina yake kwa maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Arusha waliojitokeza kumpokea barabarabni, baada ya kuonekana akiwa amevalia kombati za kijeshi.
RAIS John Magufuli jana alikuwa kivutio cha aina yake kwa maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Arusha waliojitokeza kumpokea barabarabni, baada ya kuonekana akiwa amevalia kombati za kijeshi.
 
Hii ni mara ya kwanza kwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini kuvalia magwanda ya kijeshi ziarani, hali ambayo iliwafanya wananchi kuzidi kuvutiwa na kiongozi huyo. Katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, Mgombea wa Chadema na aliyekuwa Waziri Mkuu katika serikali ya awamu ya nne, Edward Lowassa alipata ushindi wa kishindo katika mkoa huo aliozaliwa dhidi ya Rais Magufuli. Rais Magufuli alivalia mavazi hayo wakati akielekea kwenye Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi cha Monduli.
 
Akiwa katika ziara yake ya kwanza nje ya mkoa wa Dar es Salaam kikazi tangu aapishwe kuwa Rais wa Tano Novemba 5, mwaka jana watu walifurika katika mitaa mbalimbali kumwona na wakati mwingine kufunga barabara.
 
Baadhi ya wananchi hao waliokuwa wamefurika pembeni mwa barabara jana asubuhi, walijikuta katika mabishano makali kama wanayemwona ni Rais Magufuli, huku wengine wakipinga wakidhani ni mtu tofauti.Hali hiyo ilisababisha watu kusukumana ili kila mmoja amwone kwa karibu, huku wengine wakihangaika kumpiga picha kwa kutumia simu za mkononi. Picha za Rais akiwa kwenye mavazi ya kijeshi zilianza kuzagaa kwenye mitandao ya kijamii jana asubuhi.
 
Wakizungumza katika makundi makundi, wananchi wengi walisema ilikuwa ngumu kumtambua Rais Magufuli kutokana na magwanda hayo hadi pale walipomsogelea na kuona sura yake. Wananchi wengi walijikuta wakishangilia kutokana na Rais kuvaa magwanda hayo yaliyokuwa na maandishi ya jina lake kifuani, wakisema kuwa haijawahi kutokea kwa marais watatu waliomtanguliwa kuvaa vazi kama hilo ziarani. Akizungumza na wananchi hao waliosimamisha msafara wake barabarani mara kadhaa, Rais Magufuli alisema ndani ya CCM kuna majipu ambayo atayatumbua wakati wowote kuanzia sasa kwani bado anaendelea na kazi hiyo na yako mengi pia serikalini.
 
Tangu aingine madarakani, Rais amejipambanua katika kupiga vita ufisadi na ulaji wa rasilimali za nchi, na mpaka sasa amefanikiwa kuokoa zaidi ya Sh. trilioni moja ambazo zingeweza kuwa ama zimeliwa au zimetumika kwa shughuli zisizo za lazima.
 
Kampeni ya utumbuaji majipu ya Rais Magufuli ilianza Bandari ya Dar es Salaam ambako makontena zaidi ya 13,000 ama yalitolewa bila kulipiwa kodi ama kukwepa tozo ya bandari.
 
Katika kampeni hiyo Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Awadh Massawe amevuliwa madaraka yake kuhusiana na sakata hilo la utoaji wa makontena kwenye ICD bila kulipiwa kodi inayokadiriwa kufikia jumla ya Sh. bilioni 680.
 
Jumla ya Sh. bilioni 10.6 katika fedha hizo zilirudishwa na ama wadhamini au kampuni zilizokwepa kodi hiyo kufuatia agizo la serikali la kuwataka wote waliokwepa kodi kulipa bila ya adhabu.
 
Weingine walioathirika na wizi huo uliogunduliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika ziara zake mbili za ghafla mwishoni mwa mwaka jana ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hosea ambaye alifutwa kazi na Rais John Magufuli.
 
Rais pia alimsimamisha kazi ili kupisha uchunguzi Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade.
 
Waziri Mkuu Majaliwa alifanya ziara mbili za ghafla katika Bandari ya Dar es Salaam na kubaini kuwapo kwa ukwepaji kodi wa mabilioni hayo ya fedha.
 
Ukwepaji huo ulitokana na matandao mpana unaohusisha watu mbalimbali wakiwamo wafanyabiashara, maafisa wa TPA, TRA na wa taasisi nyingine za umma. Aidha, katika ziara yake ya jana akiwa amevaa nguo za kijeshi, Rais Magufuli alisema Mkuu wa Mkoa ambaye mwananchi atakufa kwa njaa kwenye eneo lake atakuwa amejifukuzisha kazi. Aliyasema hayo akiwa njiani kuelekea kwenye zoezi la kijeshi wilayani Monduli, katika hitimisho la zoezi la Onesha Uwezo wa Medani, Brigedi ya 303. Akiwa njiani alilazimika kusimama maeneo mbalimbali ili kuzungumza na wananchi waliokuwa wamefurika pembeni mwa barabara kumlaki.
 
Alisema ataendelea kutumbua majipu yanayonuka, yasiyoiva na vipele vidogovidogo vinavyoota kwani hata ndani ya vyama mbalimbali vya siasa, ikiwamo CCM, kuna majipu yanayohitaji kutumbuliwa. “Hata ndani ya Chama cha Mapinduzi nako kuna majipu yanayohitaji kutumbuliwa,” alisema huku akishangiliwa na umati wa wananchi waliokuwa wamejipanga barabarani. Rais Magufuli aliwaomba wananchi wamwamini kuwa yeye ni Rais asiyebagua wananchi kwa itikadi za vyama, hivyo anachoomba ni ushirikiano na wazidi kumwombea ili aweze kutumbua majipu ndani ya vyama pamoja na majipu makubwa na vipele vinavyoanza kuota. 
 
Dk. Magufuli alisimama katika maeneo ya Mount Meru Hotel, Tanki la Maji, Mianzini na Chuo cha Ufundi Arusha ambapo alisisitiza wananchi kuendelea kumwombea ili aweze kuleta Maendeleo na kila mtu anufaike na rasilimali za taifa. Alipofika eneo la Ngarenaro alisimama na kusikiliza kero za wananchi ambapo wananchi walilalamika  manyanyaso wanayopata kwenye Mahakama ya Mwanzo Maromboso, rushwa wanazotozwa hospitali ya Mount Meru na kesi za mirathi kwenye mahakama mbalimbali kuchukua muda mrefu.
 
“Tuna kilio Rais, tunaomba utusaidie Mahakama ya Mwanzo rushwa imekithiri, pia kesi za mirathi zinachukua muda lakini pia rushwa katika hospitali ya Mount Meru, tunaomba baba utusaidie,” alisema mmoja wa wananchi hao aliyekuwa barabarani.
 
Pia Magufuli alisimama eneo la Kona ya Nairobi na kusoma mabango yaliyokuwa yakisema hawana diwani kata ya Unga Limited kwani James Lyatuu aliyechaguliwa Oktoba 25, mwaka jana yupo kichama zaidi na si kwa maslahi ya wananchi. Mabango mengine yalilalamikia kero ya soko la Kilombero, faini zisizo za lazima kutoka kwa askari mgambo wa Jiji pamoja na kamatakamata ya mgambo hao na kuwapeleka mahakamani. Baada ya Magufuli kusoma mabango hayo na kusikiliza kero za wananchi katika maeneo hayo, alisema anaziwasilisha kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix  Ntibenda ambaye alikuwa pamoja na Rais Magufuli kwenye gari lake.
 
“Leo nipo vizuri kikombati na hizi kero mlizozisema kwasababu bado nipo hapa mkoani Arusha nitakaa na RC Ntibenda ili kuhakikisha zinatatuliwa,” alisema. “Nazikabidhi kwake lakini nawaomba mzidi kuniombea ili niweze kuwatumikia katika kipindi hiki.”
 
Aliwashukuru wananchi wa Arusha kwa kujitokeza kwa wingi barabarani na kuongeza kuwa yeye anawasalimia tu, lakini atapanga siku ya kuja kuongea nao katika Mkoa huo wa Arusha.
 
Rais Magufuli mara kadhaa aliwahi kumwambia Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete kwamba amezungukwa na watu ambao si wazuri ndani ya chama hicho.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment