*Atengua uteuzi wa kipande
Jonas Mushi na Shaban Matutu, Dar es Salaam
KASI ya Rais John Magufuli imeendelea baada ya kuhamia katika Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Hivi sasa alichokifanya ni kutengua uteuzi na kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, Dickson Maimu na wenzake wanne.
Hatua hiyo ya Rais Magufuli imetekelezwa siku chache baada ya kufuta uteuzi wa Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Dk. Feisail Issa, ambaye ilidaiwa alitaka kupigana na Mkuu wa Mkoa huo, Magesa Mulongo.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema Rais amechukua hatua hiyo baada ya kupata taarifa ya matumizi ya Sh bilioni 179.6 kiasi ambacho alisema ni kikubwa ikilinganishwa na kazi iliyofanywa na NIDA.
Mbali na Maimu, waliosimamishwa kazi ni Mkurugenzi wa TEHAMA, Joseph Makani, Ofisa Ugavi Mkuu, Rahel Mapande, Mkurugenzi wa Sheria, Sabrina Nyoni na Ofisa Usafirishaji, George Ntalima.
“Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa kuanzia leo (jana), baada ya utenguzi huo, Maimu na wenzake wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi,” alisema Balozi Balozi Sefue.
Alisema Rais Magufuli amekuwa akipokea malalamiko ya wananchi kuhusiana na kasi ndogo ya utoaji wa vitambulisho vya Taifa licha ya kiasi kikubwa cha fedha kilichotumika.
Kutokana na hatua hiyo mkuu huyo wa nchi amezielekeza mamlaka mbalimbali za uchunguzi na ukaguzi zifanye uchunguzi na ukaguzi wa namna fedha hizo zilivyotumika.
“Rais amezielekeza Mamlaka ya Udhiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) wafanye ukaguzi maalum wa ununuzi, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali afanye ukaguzi maalum wa hesabu za NIDA, ikiwamo ukaguzi wa ‘value for money’ (thamani ya fedha zilizotumika na vitambulisho vilivyotolewa) baada ya kuthibitisha idadi halisi ya vitambulisho vilivyotolewa hadi sasa.
“Rais vile vile ameelekeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ifanye uchunguzi kujiridhisha kama kulikuwa na vitendo vya rushwa au la,” alisema.
Mchakato wa mradi wa vitambulisho vya Taifa ulianza mwaka 1972 ambako sheria ya vitambulisho hivyo ilitungwa mwaka 1986 na mwaka 1995 tenda ya kwanza ikatangazwa ambayo hata hivyo haikufanikiwa.
Mwaka 2004 upembuzi yakinifu ulifanyika na Febuari mwaka 2007 ushauri ukakubaliwa na kuiteua kampuni ya Gotham kuwa mshauri mwelekezi wa mradi huo.
Wakati wa kutangaza tenda ya utengezaji wa vitambulisho vya Taifa, zaidi ya kampuni 140 ziliomba tenda hiyo na Kampuni ya Iris Corporation Bhd ya Malaysia ilishinda tenda kwa kufanya kazi hiyo kwa zaidi ya Sh bilioni 200.
KIPANDE ‘OUT’
Rais Dk. Magufuli pia ametengua uteuzi wa Madeni Kipande kabla hajathibitishwa kwenye cheo cha Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi kutokana na utendaji kazi usioridhisha.
Balozi Sefue alisema uteuzi wa Kipande umetenguliwa kabla muda wake wa majaribio haujaisha wa miezi sita kwa vile amebainika kuwa na utendaji mbovu.
Kipande alihamishiwa Mkoa wa Katavi baada ya aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta kumsimamisha kazi katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ambako alikuwa Mkurugenzi Mkuu. Alisimamishwa kutokana na tuhuma mbalimbali za ubadhirifu.
MAHADHI ATEULIWA BALOZI
Wakati huohuo, aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwenye Serikali ya Awamu ya Nne, Mahadhi Juma Maalim, ameteuliwa kuwa Balozi wa kwanza wa Tanzania nchini Kuwait, kutokana na uamuzi wa Serikali kufungua ofisi ya ubalozi katika nchi hiyo rafiki.
MABALOZI WARUDISHWA
Katibu Mkuu Kiongozi pia alisema jana kuwa Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kianda na Kimataifa, kuwarejesha nyumbani mara moja mabalozi wawili ambao mikataba yao imeisha.
“Leo hii (jana) mabalozi hao wanatakiwa kukabidhi kazi kwa mafisa wakuu au waandamizi ambao wako chini yao,” alisema Balozi Sefue.
Aliwataja mabalozi hao kuwa ni Dk. Batilda Buriani, aliyeko Tokyo Japan na Dk. James Msekela, aliyeko Rome, Italia.
Alisema pia Rais Magufuli amemrejesha nyumbani Balozi wa Tanzania aliyeko London, Uingereza, Peter Kallaghe. Amerejeshwa Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa ambako atapangiwa kazi nyingine.
Alisema hatua hiyo imesababisha kuwa na vituo sita vya balozi za Tanzania ambavyo vimeachwa wazi.
Alivitaja vituo hivyo kuwa ni London baada ya kurejea nchini kwa Balozi Kallaghe, Brussels Ubelgiji, baada ya aliyekuwa Balozi Kamala kuchaguliwa kuwa Mbunge, Rome, Italia, kufuatia kuisha kwa mkataba wa Dk. James Msekela.
MAELEKEZO KWA WATUMISHI
Balozi Sefue amewataka viongozi na watumishi wa umma kubadilika kwa dhati katika utendaji wao na kuwa waadilifu huku akiagiza watumishi wote kuvaa majina yao wanapokuwa kazini.
“Nachukua nafasi hii kuwahimiza viongozi wote katika utumishi wa umma na watumishi wote wa umma, kubadilika kwa dhati katika utendaji wao na uadilifu wao, alisema Sefuo na kuongeza:
“Kuanzia sasa watumishi wote wa umma wavae majina yao iwe rahisi kwa mwananchi kumtambua anayemhudumia na hivyo kumsifu mtumishi wa umma anayewahudumia kwa weledi, uaminifu na kwa wakati, na kumtolea taarifa yule anayefanya mambo ya ovyo,” alisema.
VIGOGO WANG’OLEWA
Tangu Rais Magufuli alipoapishwa Novemba 5, mwaka jana Serikali yake imewaondoa kazini takribani vigogo 100 wa Serikali ya awamu ya nne.
Hatua hiyo inaelezwa ni miongoni mwa mkakati wa kuzika mfumo wa Serikali ya awamu ya nne ambao baadhi ya vigogo walikuwa wakifanya mambo holela na kusahau wajibu wao kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Hatua hizo za nidhamu kwa idadi kubwa ya watumishi wa Serikali, inaonyesha kuwa kila siku kuna wastani wa vigogo wawili watendaji wa juu ambao wamejikuta wakifutwa kazi kwa sababu mbalimbali ikiwamo kutumia madaraka vibaya na hata kuisababishia hasara Serikali.
Fagio hilo linajumuisha watumishi wa Serikali waliosimamishwa kazi kutoka kwenye taasisi mbalimbali pamoja na wajumbe wa bodi ambazo zimevunjwa.
Asilimia kubwa ya vigogo waliosimamishwa kazi walichukuliwa hatua na Rais mwenyewe na wengine Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa huku wawili kati yao wakiwajibishwa na mawaziri husika katika wizara wanazoongoza.
Taasisi ya Ocean Road
Juzi, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alimsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dk. Diwani Msemo kupisha uchunguzi na kubaini iwapo kuna mgongano wa masilahi ulioathiri utendaji wa taasisi chini yake.
DART
Naye Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene, alikwisha kutangaza kumsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART), Asteria Mlambo.
RELI
Mwaka jana, Rais Dk. John Magufuli alitangaza kufuta uteuzi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO), Benhadard Tito na kuvunja bodi yake ya wajumbe wanane na ile ya Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) yenye wajumbe wanane pia.
Ilidaiwa kuwa TRL iliagiza mabehewa ya mizigo 274 mabovu huku yakiligharimu taifa Sh bilioni 220.
TAKUKURU
Desemba 16, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa,(Takukuru), Dk. Edward Hosea, baada ya kujiridhisha kuwa alishindwa kushughulia rushwa kwenye bandari ya Dar es Salaam.
Mbali na Dk. Hosea, watumishi wengine wanne wa Takukuru walisimamishwa kazi kwa kukiuka agizo la rais, kwa kusafiri kwenye nje ya nchi bila kibali maalumu.
RUNGU MUHIMBILI
Novemba 9, ikiwa ni siku chache baada ya kuapishwa, Rais Dk Magufuli alifanya ziara ya kushitukiza kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kukuta mashine ya MRI na CT-Scan hazifanyi kazi jambo lililomfanya avunje bodi ya wadhamini ya hospitali hiyo iliyokuwa na wajumbe 11.
Pia alimsimamisha kazi Dk. Hussein Kidanto aliyekuwa akikaimu nafasi ya ukurugenzi wa hospitali hiyo na kumrudisha Wizara ya Afya na Ustawi wa Jami.
TRA na PTA
Novemba 27, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alifanya ziara ya kushtukiza bandari ya Dar es Salaam na kubaini kuwa makontena 329 yalitolewa bandarini bila kulipiwa kodi na kusababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 80.
Aliwasimamisha kazi vigogo kadhaa, wakiwamo maofisa 12, wengine wakiwa ni wajumbe wa bodi iliyovunjwa.
Kutokana na ubadhirifu wa Sh 16 bilioni kwenye Shirika la Reli Tanzania (TRL), Rais Magufuli pia alitangaza kutengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Shaban Mwinjaka.
TANESCO
Desemba 6 mwaka jana, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), liliWAsimamisha maofisa saba kwa kile kilichodaiwa kwamba ni kutokana na makosa mbalimbali ukiwamo wizi na ubadhirifu.
/MTANZANIA.
No comments :
Post a Comment