Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, January 24, 2016

Magufuli atunisha msuli

jk*Atamba nchi iko salama, hakunamwenye jeuri ya kuleta chokochoko
*Aahidi neema kwa wanajeshi kufufua kambi ya Nyumbu
NA ELIYA MBONEA, MONDULI, MTANZANIA.
AMIRI Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais John Magufuli, amesema nchi ipo salama na hakuna mtu yeyote mwenye uwezo wala jeuri ya kuleta chokochoko.
Amesema Jeshi la Ulinzi (JWTZ) liko imara na linatekeleza majukumu yake ya kulinda mipaka ya nchi kwa uhakika na pia linashiriki kazi ya kulinda amani katika nchi zenye migogoro.
Rais Magufuli alitoa kauli hiyo jana, katika kambi ya Jeshi ya Mbuni iliyoko Wilaya ya Monduli, mkoani Arusha, wakati akizungumza na makamanda na wapiganaji wa kambi hiyo baada ya kuikagua.
Ikiwa mara yake ya kwanza kuzungumza na makamanda na wapiganaji ndani ya kambi ya jeshi, huku akiwa amevaa mavazi ya kijeshi, Rais Magufuli alisema hata wanasiasa wamekuwa wakijivunia kazi ya ulinzi na usalama inayofanywa na wanajeshi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, hivyo kuwepo haja ya kulinda maslahi ya wapiganaji hao.
“JWTZ lipo imara kuhakikisha nchi yetu inakuwa na ulinzi na usalama mipakani, niwahakikishie Watanzania tupo salama na hakuna mtu anayeweza kutuletea chokochoko.
“Wanasiasa nao wamekuwa wakijivunia ulinzi na usalama wa wanajeshi wetu na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, hivyo nitahakikisha maslahi yao yanalindwa,” alisema Rais Magufuli.
Alisema Jeshi linafanya kazi nzuri na kubwa, hivyo Serikali itahakikisha inaboresha hali ya wanajeshi pamoja na kufufua kambi ya Nyumbu, iliyopo Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani.
Rais Magufuli, ambaye yuko katika ziara ya kikazi mkoani Arusha, leo anatarajiwa kuwavisha nishani maofisa wa Jeshi katika Chuo cha Kijeshi cha TMA, kilichopo Monduli.
Akizungumzia vitendea kazi vya jeshi, alisema Serikali imedhamiria kuendelea kuliwezesha JWTZ kwa kuboresha na kulipatia vifaa vya kisasa vinavyoendana na mabadiliko ya teknolojia duniani.
Aidha, Magufuli aliwaagiza Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, ambao ameambatana nao katika ziara hiyo kuandaa mpango wa kuanzishwa kwa kiwanda cha kutengeneza sare za Jeshi. Mbali na viongozi hao, kiongozi mwingine aliye katika ziara hiyo ya Rais Magufuli ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama (CDF), Jenerali Davis Mwamunyange.
Akizungumza katika tukio hilo, Waziri Mwinyi alimshukuru Rais Magufuli kufanya ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali katika kambi hiyo na kupata fursa ya kuona zana mpya na za kisasa za JWTZ.
“Tunaamini Serikali itaendelea kuboresha vitendea kazi, yakiwamo maslahi ya askari, hususan katika kuwawezesha kuendelea kupata mbinu tofauti za kisasa katika masuala ya kivita.
Kabla ya kuondoka kambini hapo, Rais Magufuli aliagiza uongozi wa jeshi kuwapatia ajira vijana zaidi ya 800 walioshiriki zoezi la kijeshi aliloonyeshwa lililotambulika kwa jina la ‘onyesha uwezo wa medani.’
Kauli hii ya Rais Magufuli imekuja ikiwa ni siku chache baada ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja ya Kitaifa ya Zanzibar (SUK), Maalim Seif Sharif Hamad, kumtaka Amri Jeshi Mkuu huyo kutotumia wadhifa wake huo kutuma wapiganaji Zanzibar pindi amani itakapovunjika.
Maalim Seif, ambaye alikuwa akizungumzia hali ya kisiasa visiwani Zanzibar, alimuomba Rais Magufuli kuingilia kati mzozo wa kisiasa ulioibuka baada ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana, baada ya kubaini kuwepo kwa kasoro kadhaa kabla ya jana kutangaza kuwa uchaguzi wa marudio utafanyika Machi 20, mwaka huu.
Wakati ZEC ikitangaza tarehe ya marudio ya uchaguzi huo, Maalim Seif amekwishaeleza msimamo wake na Chama cha Wananchi (CUF), kinachoungwa mkono na vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wa kususia marudio ya uchaguzi huo.
Kwa upande mwingine, Chama Cha Mapinduzi na SUK, kwa nyakati tofauti vimekuwa vikisisitiza kuwa vitashiriki uchaguzi wa marudio.

No comments :

Post a Comment