Toleo la 440
13 Jan 2016
Waliokuja kulijuwa jina lake walilijuwa baada ya kuzisikia ndaro na mbwembwe zake katika maamuzi aliyoyakata na utekelezaji wa baadhi ya maamuzi hayo. Mfano ni zile ziara zake za ghafla za kukagua Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Wizara ya Fedha au amri kadhaa alizotoa zenye lengo la kuyabana matumizi ya fedha za serikali. Miongoni mwa amri hizo ni ile ya kuwazuia mawaziri wasisafiri kwenda nje ya nchi au kupiga marufuku sherehe za kitaifa za kuadhimisha tarehe ya Uhuru wa Tanganyika.
Watanzania wengi wameyafurahia, tena kwa furaha kubwa, maamuzi aliyoyakata Magufuli hususan hayo yenye kubana matumizi ya fedha za umma na yenye kuupiga vita ufisadi.
Juu ya yote hayo, wengi ulimwenguni bado hawamjui hasa Magufuli ni nani na ni kiongozi wa aina gani. Hata kwa Watanzania wengi Magufuli bado ni kitendawili kinachosubiri kuteguliwa. Pengine itachukuwa muda kabla hakijateguliwa kwa sababu bado Magufuli hana nguvu na uzito mkubwa ndani ya chama kinachotawala, Chama cha Mapinduzi (CCM).Labda hatutoweza kumjuwa, kwa uhakika, Magufuli ni nani mpaka kwanza awe na madaraka kutosha ndani ya CCM. Kwa sasa, mikono yake lazima itafungika kidogo ingawa mfumo wa utawala nchini umebadilika na haufuati ule wa nyakati za utawala wa chama kimoja, ambapo chama ndicho kilichokuwa na usemi wa mwisho kuhusu maamuzi ya serikali.
Tangu awe Rais amekata, na kuyatekeleza, baadhi ya maamuzi yake kisinema sinema. Ametenda mambo kana kwamba yeye ni mhusika au mwigizaji mkuu katika tamthili ya anayetambulika kuwa ni mbabe kwa vitendo vyake vya kibabe.
Amewashangaza wengi ndani ya nchi na walio nje ya nchi si kwa hatua alizozichukuwa tu bali hata kwa namna alivyozichukuwa hatua hizo.
Kuna walioshtuka na kuna waliopigwa na bumbuazi kwa hatua hizo. Kadhalika,kuna wanaomuangalia tu wakimtizama atafika wapi. Walio katika kundi hili la mwisho ni pamoja na wale wasiomthamini, wasioamini kwamba Magufuli ana sifa zinazohitajika za kumfanya awe Rais madhubuti anayeweza kutawala kwa hekima.
Hawa pia wanamkosoa wakisema kwamba anafanya mambo kwa papara bila ya kuzingatia athari zitazosababishwa na hizo hatua zake za kikaka-kaka. Mfano mmoja wanaoutoa ni bomoabomoa jijini Dar es Salaam iliyosababisha watu wengi wasiojiweza kukosa makazi.
Kuna wengi waliopata mshtuko mkubwa kwa kuziona nyumba walimokuwa wakiishi zikitiwa alama kwamba zitabomolewa. Bomoabomoa hiyo ambayo haikumuonea mtu huruma imesababisha kifo cha mtu mmoja na mwengine ghafla kupigwa na maradhi ya kiharusi.
Vituko kama hivyo vinazidi kuwapa hoja mahasimu zake Magufuli. Vinaonyesha kwamba bado Magufuli anaelea katika shangwe ya ushindi wake wa uchaguzi wa urais na namna wananchi walivyozisherehekea hatua zake za awali baada ya kuwa Rais.
Matokeo ya hayo ni kwamba baada ya Magufuli, “mbabe mkuu”, kuonekana kwamba anapata sifa na kufurahiwa na kushangiliwa na wananchi wa chini baadhi ya mawaziri wake pamoja na baadhi ya manaibu wa mawaziri wakaanza na wao kumuiga kwa kujifanya nao wababe.
Sasa umeingia huu mtindo wa mawaziri kuwashtukia wafanyakazi wa wizara zao, huku ofisi zao zikiwa tayari zimekwisha viarifu vyombo vya habari kuhusu ziara hizo. Mawaziri huvimbisha mashavu na kujifanya wakali wakikutana na maofisa wa ngazi za juu na za chini za wizara zao.
Kwa vile “Bwana Mkubwa” mpya kafanya, basi na wao pia wanataka waonekana kuwa wanafanya. Hiyo ndiyo njia moja wanayoitumia kujipendekeza kwa Rais. Bila ya shaka, kwa kufanya hizo ziara za kushtukia wamefanikiwa kwa moja: kuwatia hofu na jambajamba watumishi wa wizara zao.
Wanaompinga Magufuli, hata ndani ya chama chake, wanasema kwamba muda si mrefu atalevywa ama na madaraka au na sifa nyingi na namna anavyoshangiliwa. Na akishalewa atalainika na kulegeza kamba.
Dalili tumekwishaanza kuziona kwamba zile nguvu na kasi za siku za mwanzo mwanzo za uongozi wake zinaonyesha kuanza kupwaya. Bado hakuna vigogo waliotiwa mbaroni na kufikishwa mahakamani kwa ufisadi. Sio kwamba hawako lakini wanaendelea kulindwa kama ilivyokuwa kawaida katika awamu mbili zilizopita.
Baadhi ya mawaziri wa awamu ya nne waliojichafulia majina yao kwa utendaji mbovu wa kazi au kwa kuhusishwa na ufisadi ni miongoni mwa mawaziri aliowateua Magufuli. Kwa sababu baadhi ya hatua zilizochukuliwa na serikali ya Magufuli hazikuchukuliwa kwa uangalifu hivi sasa waathirika wa hatua hizo wameifikisha serikali mahakamani.
La kusikitisha zaidi ni kuona kwamba hadi sasa Magufuli hakutamka chochote cha kuwahakikishia wananchi kwamba ule mswada wa Katiba waitakayo na uliozikwa na serikali ya awamu ya nne utafufuliwa na kufikishwa kwao ili waupigie kura ya maamuzi. Suala hili linahuzunisha kwa sababu linathibitisha kwamba ingawa taifa limepata Rais mpya bado chama kinachotawala kinatumia ubabe wake, tena kwa kibri kikubwa, kuwanyima wananchi haki zao za kimsingi.
Kama kweli Magufuli anaupiga vita ubadhirifu wa fedha za umma basi tungemuona anawachukulia hatua za kisheria wale waliosababisha ubadhirifu wa kutumia zaidi ya shilingi bilioni 40 kwa mchakato wa kulipatia taifa Katiba mpya. Tume ya Jaji Joseph Warioba iliyoteuliwa kwa shughuli hiyo ilikamilisha kazi yake kwa kuwasilisha mswada wa Katiba uliopendekezwa na wananchi na ambao baadaye ulitupiliwa mbali kwa kibri na wenye nguvu.
Na kama kweli Magufuli anaupiga vita ubadhirifu wa fedha za umma na anasimamia haki, kama alivyoahidi wakati wa kampeni ya uchaguzi wake, basi tumuone akiingilia kati Zanzibar na kuizuia Tume ya Uchaguzi ya huko (ZEC) isizifuje fedha za umma kwa kuurejelea uchaguzi uliokwishafanywa kwa haki na kwa uwazi na kuthibitishwa na waangalizi wa kimataifa na wa Tanzania.
Kama kweli Magufuli anasimamia utawala bora, anaheshimu sheria na Katiba basi tumuone akiwachukulia hatua wanaoikiuka sheria na kuivunja Katiba ya Zanzibar kwa viroja vyao vya kuufuta uchaguzi wa huko wa Oktoba mwaka jana. Asipowafanya watawala wa Zanzibar wawajibike basi tutathibitisha tu kwamba ama hakuwa mkweli alipotoa ahadi zake wakati wa kampeni ya uchaguzi au ameshindwa nguvu na wahafidhina wa CCM kutoka Bara na Zanzibar.
Miongoni mwa mambo ambayo Magufuli aliyaahidi wakati alipokuwa akiizunguka nchi akipiga kampeni ya kutaka achaguliwe Rais ni kuupiga vita ufisadi, kukomesha ubadhirifu wa fedha za umma, kurejesha nidhamu katika utendaji kazi serikalini na kuwafanya waliopewa dhamana ya uongozi wawajibike.
Hakuna yeyote mwenye akili zake timamu atayeyapinga hayo. Ni muhimu kwamba kwa vile sasa ni Rais azitekeleze ahadi hizo kwani utekelezwaji wake utasaidia kulifanya taifa lipige hatua katika kuusimamisha utawala bora.
Kuzitekeleza ahadi hizo maana yake ni kuzitekeleza kwa ukamilifu siyo vipande vipande. Kuzitekeleza pia kuna maana kwamba Magufuli anapozitekeleza awe anazitekeleza kwa kufuata sheria siyo kwa ubabe na maguvu.
- See more at: http://raiamwema.co.tz/magufuli-hahitaji-shangwe-wala-hofu-kuendesha-nchi#sthash.bBCv2Rrh.dpuf
No comments :
Post a Comment