Rais John Magufuli akimuapisha Naibu Katibu Mkuu, wizara ya katiba na sheria, Amon Mpanju leo ikulu jijini Dar es Salaam. Picha na Anthony Siame
Dar es Salaam. Rais John Magufuli leo amewaapisha makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
Zoezi hilo lilihusisha makatibu wakuu 29 na naibu makatibu wakuu 21 ambao uteuzi wake ulitangazwa na Rais Magufuli mapema wiki hii.
Baada ya kuapishwa, watendaji hao wa serikali walisaini hati za uadilifu katika juhudi za Serikali ya awamu ya tano kukuza utu, uwazi, uwajibikaji na kuwajengea wananchi imani kwa uongozi wa umma.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema zoezi la watendaji wa Serikali kusaini fomu za ahadi ya uadilifu litakuwa endelevu na kwamba viongozi wengine wote watakaoteuliwa watasaini hati hizo.
Alisema wakurugenzi, wakuu wa mikoa na wilaya wateule nao watasaini fomu hizo ili kuhakikisha fedha za Serikali zinazotolewa kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo zinatumika kwa maslahi ya umma.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema watendaji hao wa Serikali watafanyiwa semina elekezi jijini Dar es Salaam kuanzia saa nne asubuhi kesho ili kuwapa dira ya utendaji unaotarajiwa kutoka kwao.
No comments :
Post a Comment