Ni mwaka mwingine, ambao kila Mtanzania amebeba matumaini tofauti na mwenzake.
Wapo wale ambao wanadhani utakuwa ni mwaka wa kawaida, utapita na kumalizika kama ulivyoanza.
Ninatambua kuwapo pia kwa baadhi wanaouangalia kwa hasira kali, hasa wakiangalia mambo ambayo ama wamefanyiwa, rafiki au ndugu zao.
Hao, niliwasemea kwa kiasi kikubwa wiki iliyopita pale nilipogusia suala la bomoa bomoa, ambalo limekuwa likiendelea kwenye maeneo mbalimbali ya nchi yetu.
Nilimweleza rafiki yangu, William Vangimembe Lukuvi, Waziri wa Ardhi kuwatumia vijana wasomi kutoka Chuo Kikuu Ardhi na matawi yake, Morogoro na Tabora ili wakimbize na kuharakisha upimaji wa ardhi yote na hatimaye upatikanaji wa hati.
Nimshauri tena Lukuvi na msaidizi wake, Angelina Mabula waangalie kwa umakini wataalam wa mipango miji, ikiwezekana wawapangie upya kazi na majukumu mapya.
Pale inapowezekana wawahamishe wengine ambao wameishi na kufanya kazi katika miji na mikoa mingi nchini.
Suala hili la mipango miji, lipewe mtazamo mpya kwani linawezekana kuwa ndilo jipu linaloisumbua miji yetu mingi, mikubwa na midogo, kiasi kwamba imejengwa bila mipangilio yoyote, hakuna hati na wala hakuna ofisa wa Serikali aliyeguswa au kusumbuliwa nalo.
Mbali na mipango miji, zipo sheria ninazoaamini wataalam wetu wa sheria kwenye wizara mbalimbali, wakisaidiana na wale wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu (AG), lazima wakae chini na kuzipitia, ikiwezekana ziwasilishwe mapema kwenye vyombo vinavyohusika ili zibadilishwe.
Miongoni mwa sheria hizo ni ile ya ujenzi holela kwenye maeneo ya wazi , kubatilisha matumizi ya ardhi, ambayo imekuwa ikitumiwa vibaya kwa miaka mingi.
Hili la matumizi ya ardhi kubatilishwa kwa amri ya rais, inawezekana kuwa tatizo sugu ambalo lazima liangaliwe upya kisheria, ikiwezekana iwe kwa kila kipande cha ardhi.
Nashauri ardhi iliyoko kwenye maeneo nyeti, yenye madini, taasisi za umma, kama vyombo vya ulinzi na usalama na kadhalika lazima ili ilindwe.
Pia, ujenzi unaofanyika kwenye maeneo vya vyanzo vya maji, hifadhi na maeneo mengine, uliofanyika kwa miaka mingi katika mchi yetu, bila viongozi kushtuka liangaliwe upya.
Wataalam wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi au wale wa ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) kupitia Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lazima waje na mipango, mikakati ya kumaliza tatizo siyo kubomoa kwenye maeneo hayo, ambayo imelalamikiwa na watu.
Jiulize, kwanini lawama hizi leo? Ninajiuliza, zilikuwa wapi mamlaka za umma kwenye awamu zote nne zilizotangulia, kiasi kwamba wanapobanwa waliojimegea ardhi, kisha wajkajenga, je, wasimamizi wa sheria zilizokuwapo walichukuliwa hatua gani?
Suala la ardhi na matumizi yake nililisemea kwa uchungu kwenye toleo la mwisho wa mwezi uliopita, sikutaka leo kulizungumzia unapoanza mwaka 2016.
Huu ni mwaka ambao nimesema tangu awali kuwa utaangaliwa kwa mitazamo tofauti, ingawa ninatambua kuwa kesho, Januari 5, bomoa bomoa inaendelea upya baada ya kusitishwa na Waziri Lukuvi.
Kuhusu mwaka 2016, nilisema wapo ambao watauona mgumu, wakiwamo wafanyabiashara hasa wale ambao wamekuwa wakibanwa walipe kodi zote walizoachiwa kwa mingi bila kulipa.
Tumeona jinsi ambavyo kibano cha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kule bandarini kinavyoendelea kuzaa matunda kwani tumeambiwa kuwa makasha (makontena) zaidi ya 11,000 yamebainika kupitishwa bila kulipa tozo (ada) zinazostahili.
Ninajiuliza, je, wenzetu hasa wale waliokabidhiwa kazi kwenye bandari, viwanja vya ndege, mbuga za wanyama ni wazalendo kiasi gani hasa wanapoachia mali zipite bila kulipiwa kodi au tozo au wanyama wetu kusafirishwa nje ya nchi bila vibali au wakati mwingine wakiwa hai, jambo ambalo ni kinyume cha sheria?
Dhana ya huyu mwenzetu, ilizoeleka katika nchi hii kwa miaka mingi, je, ndiyo ilyowatajirisha wachache, huku wengi wakikondeana kama sindano?
Ninaposema mwenzetu, nina maana kuwa ama kwa itikadi ya kichama au urafiki na viongozi, inaonekana wapo wachache walioachiwa kufanya mambo wapendavyo, ikiwamo biashara na walifanya hivyo kwa miaka mingi, wakajipatia utajiri mkubwa, lakini kodi ambazo zingeiwezesha nchi kusimama, zilisahaulika.
Ninaposema kodi zilisahaulika, sina maana kwamba hazikutozwa, inawezekana kuwa zilikusanywa, lakini ama zikaliwa na wajanja kama fadhila kwa kuwawezesha wakubwa kuingia madarakani au zilikuwa kidogo hazilingani na ukubwa wa biashara.
Dhana ya Chukua Chako Mapema, ambayo imekuwa ikipigiwa kelele na Watanzania wakati mwingine kuhusishwa na chama dola au kilicho madarakani, inawezekana kuwa ndiyo imeifikisha nchi yetu mahali ilipo, ambako wakati mwingine tunaambiwa kuwa nchi imeishiwa fedha, haiwezi kujiendesha.
Jiulize, Serikali na mabavu yake yote pamoja misuli yake, inawezaje kushindwa kujiendesha ikikusanya vyema kodi kutoka kwa walipaji wote wanaostahili?
Je, itaweza kukosa fedha kama zilizokusanywa zimetunzwa vizuri bila kuwekwa kwenye mifuko iliyotoboka na yenye kuvuja, kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwa miaka mingi?
Je, Tanzania ambayo imeitwa kuwa ya asali na maziwa, yapo wapi?
Nilishauri wakati ule kwamba kiongozi wetu ajaye, yaani rais, ambaye kwa sasa ni Dk John Magufuli, awe mkali, asione haya kuwachukulia hatua wabadhirifu wa mali za umma, inapendeza kuona amekuwa muungwana, ameanza kazi akiwabana watu wa Mamlaka ya Mapato (TRA).
Uungwana huo wa Dk Magufuli na timu yake, ambayo imekaribia kukamilika baada ya kuwateua makatibu wakuu na manaibu wao na kuwaapisha kisayansi, inavutia kiasi cha kuufanya mwaka huu, uwe kweli wa kazi.
Kaulimbiu ya Dk Magufuli, ‘Hapa Kazi Tu’, aliyoianzia kule Hazina, mahali ambako wastaafu wengi wamekuwa wakati mwingine wakifia kwenye baraza (korido) wakifuatilia mafao, naamini sasa patakuwa kimbilio la wengi.
Naamini, Dk Magufuli amewaeleza TRA, wabadilike, waache kuwakimbiza walipakodi, waache umangimeza na kauli ambazo zinazuia kulipa kodi kwa hiari, bila shurti.
Ninaamini, Eliachim Maswi, aliyekabidhiwa rungu la kusimamia TRA akiwa kaimu naibu kamishna mkuu atasaidiana na wachapakazi wengine waliopo kwenye chombo hiki kikubwa kinachofanya kazi kwa utashi, weledi, nchi itasonga mbele.
Lakini, lazima TRA mhakikishe watu wanakwenda wenyewe kujisajili au kulipa kodi.
Inaumiza, mtu anapowazuru TRA kwa hiari alipe kodi, anakutana na vikwazo vinavyomkatisha tamaa kiasi cha kufikiria kukwepa kodi, jambo linaloikosesha nchi mapato kwa kiasi kikubwa.
No comments :
Post a Comment